Hesabu Mlango 10 Numbers

Hesabu 10:1

Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,

Hesabu 10:2

Jifanyie tarumbeta mbili za fedha; utazifanya za kazi ya ufuzi; nawe utazitumia kwa kuwaita mkutano wakutane, na kwa kusafiri kwao yale makambi.

Hesabu 10:3

Na hapo watakapozipiga hizo tarumbeta, mkutano wote utakukutanikia wewe, hapo mlangoni pa hema ya kukutania.

Hesabu 10:4

Nao wakipiga tarumbeta moja tu ndipo wakuu, walio vichwa vya maelfu ya Israeli, watakukutanikia wewe

Hesabu 10:5

Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha sana, marago yaliyoko upande wa mashariki yatasafiri. Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha ya pili, marago yaliyoko upande wa kusini watasafiri;

Hesabu 10:6

watapiga sauti ya kugutusha kwa ajili ya safari zao.

Hesabu 10:7

Lakini mkutano utakapokutanishwa pamoja mtapiga, lakini hamtapiga sauti ya kugutusha.

Hesabu 10:8

Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta; nazo zitakuwa kwenu ni amri ya milele katika vizazi vyenu vyote.

Hesabu 10:9

Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu.

Hesabu 10:10

Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Hesabu 10:11

Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi.

Hesabu 10:12

Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani.

Hesabu 10:13

Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa.

Hesabu 10:14

Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake.

Hesabu 10:15

Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari.

Hesabu 10:16

Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni.

Hesabu 10:17

Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele.

Hesabu 10:18

Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.

Hesabu 10:19

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai.

Hesabu 10:20

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli.

Hesabu 10:21

Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao.

Hesabu 10:22

Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi.

Hesabu 10:23

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri.

Hesabu 10:24

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni.

Hesabu 10:25

Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai.

Hesabu 10:26

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani;

Hesabu 10:27

Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani.

Hesabu 10:28

Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele.

Hesabu 10:29

Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo Bwana amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa Bwana ametamka mema juu ya Israeli.

Hesabu 10:30

Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe.

Hesabu 10:31

Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho.

Hesabu 10:32

Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote Bwana atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo.

Hesabu 10:33

Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa Bwana safari ya siku tatu; na sanduku la agano la Bwana likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika.

Hesabu 10:34

Na wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini.

Hesabu 10:35

Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee Bwana, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao.

Hesabu 10:36

Tena hapo liliposimama, akasema, Ee Bwana, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.