Hesabu Mlango 30 Numbers

Hesabu 30:1

Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana.

Hesabu 30:2

Mtu atakapomwekea Bwana nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake.

Hesabu 30:3

Tena mtu mke atakapomwekea Bwana nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake;

Hesabu 30:4

babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika.

Hesabu 30:5

Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na Bwana atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza.

Hesabu 30:6

Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia;

Hesabu 30:7

na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika.

Hesabu 30:8

Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na Bwana atamsamehe

Hesabu 30:9

Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake.

Hesabu 30:10

Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo,

Hesabu 30:11

na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika.

Hesabu 30:12

Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na Bwana atamsamehe.

Hesabu 30:13

Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua.

Hesabu 30:14

Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake.

Hesabu 30:15

Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe.

Hesabu 30:16

Hizi ndizo amri, ambazo Bwana alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, ali nyumbani mwa babaye.