Hesabu Mlango 21 Numbers

Hesabu 21:1

Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka.

Hesabu 21:2

Basi Israeli akaweka nadhiri kwa Bwana akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa.

Hesabu 21:3

Bwana akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma.

Hesabu 21:4

Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.

Hesabu 21:5

Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.

Hesabu 21:6

Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.

Hesabu 21:7

Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.

Hesabu 21:8

Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.

Hesabu 21:9

Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.

Hesabu 21:10

Kisha wana wa Israeli wakasafiri, wakapanga marago Obothi.

Hesabu 21:11

Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika jangwa iliyoelekea Moabu, upande wa maawio ya jua.

Hesabu 21:12

Kutoka huko wakasafiri, wakapanga katika bonde la Zeredi.

Hesabu 21:13

Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.

Hesabu 21:14

Kwa hiyo imesemwa katika chuo cha Vita vya Bwana, Wahebu katika Sufa, Na bonde za Arnoni,

Hesabu 21:15

Na matelemko ya hizo bonde Kwenye kutelemkia maskani ya Ari, Na kutegemea mpaka wa Moabu.

Hesabu 21:16

Kutoka huko wakasafiri kwenda Beeri; ni kisima ambacho Bwana alimwambia Musa, Uwakutanishe watu, nami nitawapa maji.

Hesabu 21:17

Ndipo Israeli wakaimba wimbo huu; Bubujika Ee kisima; kiimbieni;

Hesabu 21:18

Kisima walichokichimba wakuu, Ambacho wakuu wa watu wakakifukua, Kwa fimbo za enzi, kwa fimbo zao.

Hesabu 21:19

na kutoka Matana wakaenda Nahalieli; na kutoka Nahalieli wakaenda Bamothi;

Hesabu 21:20

na kutoka Bamothi wakaenda bondeni kwenye konde la Moabu, hata kilele cha Pisga, kielekeacho chini jangwani.

Hesabu 21:21

Kisha Israeli akatuma wajumbe kumwendea Sihoni mfalme wa Waamori, na kusema,

Hesabu 21:22

Nipe ruhusa nipite katika nchi yako; hatutageuka kando kwenda mashambani, wala kuingia katika mashamba ya mizabibu hatutakunywa maji ya visimani; tutakwenda kwa njia kuu ya mfalme, hata tutakapokuwa tumepita mpaka wako.

Hesabu 21:23

Lakini Sihoni hakukubali kumwacha Israeli kupita katika mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, akatoka aende kupigana na Israeli jangwani, akafika mpaka Yahasa; akapigana na Israeli.

Hesabu 21:24

Israeli wakampiga kwa makali ya upanga, na kuimiliki nchi yake, tangu mto wa Arnoni hata mto wa Yaboki, mpaka nchi ya wana wa Amoni; kwa kuwa mpaka wa wana wa Amoni ulikuwa una nguvu.

Hesabu 21:25

Basi Israeli wakaitwaa miji hiyo yote; Israeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, katika Heshboni, na miji yake yote.

Hesabu 21:26

Kwa kuwa Heshboni ulikuwa ni mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akipigana na mfalme wa Moabu wa mbele, na kumpokonya nchi yake yote mkononi mwake, mpaka mto wa Arnoni.

Hesabu 21:27

Kwa hiyo, hao wanenao kwa mithali wasema, Njoni Heshboni, Mji wa Sihoni na ujengwe na kuthibitishwa;

Hesabu 21:28

Maana, moto umetoka Heshboni, Umekuwa Ari ya Moabu, Mwali wa moto umetoka mji wa Sihoni; Wakuu wa mahali palipoinuka Arnoni

Hesabu 21:29

Ole wako Moabu! Umeangamia, enyi watu wa Kemoshi; Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi, Na binti zake waende utumwani, Wamwendee Sihoni mfalme wa Waamori.

Hesabu 21:30

Tumewapigia mishale; Heshboni umepotea mpaka Diboni, Nasi tumeharibu mpaka Nofa, Ifikiliayo Medeba.

Hesabu 21:31

Basi hivyo Israeli akaketi katika nchi ya Waamori.

Hesabu 21:32

Kisha Musa akapeleka watu ili kupeleleza Yazeri, nao wakaitwaa miji yake, wakawafukuza Waamori waliokuwamo.

Hesabu 21:33

Kisha wakageuka na kukwea kwa njia ya Bashani; na Ogu mfalme wa Bashani akaondoka apigane nao huko Edrei, yeye na watu wake wote.

Hesabu 21:34

Bwana akamwambia Musa, Usimche; kwa kuwa nimekwisha mtia mkononi mwako, na watu wake wote, na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni mfalme wa Waamori, aliyeketi Heshboni.

Hesabu 21:35

Basi wakampiga, na wanawe, na watu wake wote, hata wasisaze kwake mtu ye yote; nao wakaimiliki nchi yake.