Hesabu Mlango 23 Numbers

Hesabu 23:1

Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.

Hesabu 23:2

Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.

Hesabu 23:3

Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima.

Hesabu 23:4

Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.

Hesabu 23:5

Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.

Hesabu 23:6

Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.

Hesabu 23:7

Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli.

Hesabu 23:8

Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?

Hesabu 23:9

Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.

Hesabu 23:10

Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.

Hesabu 23:11

Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa.

Hesabu 23:12

Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?

Hesabu 23:13

Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko.

Hesabu 23:14

Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.

Hesabu 23:15

Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule.

Hesabu 23:16

Bwana akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi.

Hesabu 23:17

Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana amenena nini?

Hesabu 23:18

Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori;

Hesabu 23:19

Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?

Hesabu 23:20

Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua.

Hesabu 23:21

Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.

Hesabu 23:22

Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati.

Hesabu 23:23

Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!

Hesabu 23:24

Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.

Hesabu 23:25

Balaki akamwambia Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa.

Hesabu 23:26

Lakini Balaamu akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno Bwana atakalolisema sina budi kulitenda?

Hesabu 23:27

Kisha Balaki akamwambia Balaamu, Haya, njoo sasa, nikupeleke mahali pengine; labda Mungu ataridhia kwamba unilaanie watu hao huko.

Hesabu 23:28

Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini yake.

Hesabu 23:29

Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.

Hesabu 23:30

Basi Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume juu ya kila madhabahu.