Hesabu Mlango 11 Numbers

Hesabu 11:1

Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.

Hesabu 11:2

Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.

Hesabu 11:3

Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao.

Hesabu 11:4

Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule?

Hesabu 11:5

Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;

Hesabu 11:6

lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.

Hesabu 11:7

Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola.

Hesabu 11:8

Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya.

Hesabu 11:9

Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.

Hesabu 11:10

Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika.

Hesabu 11:11

Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu?

Hesabu 11:12

Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao?

Hesabu 11:13

Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula.

Hesabu 11:14

Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda.

Hesabu 11:15

Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.

Hesabu 11:16

Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe.

Hesabu 11:17

Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.

Hesabu 11:18

Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula.

Hesabu 11:19

Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini;

Hesabu 11:20

lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?

Hesabu 11:21

Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima.

Hesabu 11:22

Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha?

Hesabu 11:23

Bwana akamwambia Musa, Je! Mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo.

Hesabu 11:24

Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya Bwana; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema.

Hesabu 11:25

Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena.

Hesabu 11:26

Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini.

Hesabu 11:27

Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.

Hesabu 11:28

Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.

Hesabu 11:29

Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.

Hesabu 11:30

Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.

Hesabu 11:31

Kisha upepo ukavuma kutoka kwa Bwana, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi.

Hesabu 11:32

Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote.

Hesabu 11:33

Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za Bwana ziliwaka juu ya watu, Bwana akawapiga watu kwa pigo kuu mno.

Hesabu 11:34

Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani.

Hesabu 11:35

Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.