Hesabu Mlango 22 Numbers

Hesabu 22:1

Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko.

Hesabu 22:2

Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori.

Hesabu 22:3

Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.

Hesabu 22:4

Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.

Hesabu 22:5

Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi.

Hesabu 22:6

Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.

Hesabu 22:7

Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.

Hesabu 22:8

Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu.

Hesabu 22:9

Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe?

Hesabu 22:10

Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,

Hesabu 22:11

Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.

Hesabu 22:12

Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.

Hesabu 22:13

Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.

Hesabu 22:14

Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi.

Hesabu 22:15

Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza.

Hesabu 22:16

Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie;

Hesabu 22:17

maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa.

Hesabu 22:18

Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.

Hesabu 22:19

Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi.

Hesabu 22:20

Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.

Hesabu 22:21

Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.

Hesabu 22:22

Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.

Hesabu 22:23

Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani.

Hesabu 22:24

Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.

Hesabu 22:25

Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili.

Hesabu 22:26

Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto.

Hesabu 22:27

Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake.

Hesabu 22:28

Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?

Hesabu 22:29

Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.

Hesabu 22:30

Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!

Hesabu 22:31

Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi.

Hesabu 22:32

Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu,

Hesabu 22:33

punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.

Hesabu 22:34

Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena.

Hesabu 22:35

Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.

Hesabu 22:36

Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.

Hesabu 22:37

Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi?

Hesabu 22:38

Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.

Hesabu 22:39

Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi.

Hesabu 22:40

Balaki akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye.

Hesabu 22:41

Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.