Hesabu Mlango 28 Numbers

Hesabu 28:1

Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,

Hesabu 28:2

Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.

Hesabu 28:3

Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea Bwana; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.

Hesabu 28:4

Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;

Hesabu 28:5

pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.

Hesabu 28:6

Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto.

Hesabu 28:7

Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia Bwana katika mahali hapo patakatifu.

Hesabu 28:8

Na mwana-kondoo wa pili utamsongeza wakati wa jioni; kama ile sadaka ya unga iliyosongezwa asubuhi, na kama sadaka yake ya kinywaji, ndivyo utakavyoisongeza, ni sadaka ya kusongezwa kwa moto, ni harufu ya kupendeza kwa Bwana.

Hesabu 28:9

Tena katika siku ya Sabato watasongezwa wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, pamoja na sehemu ya kumi mbili za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji;

Hesabu 28:10

hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila Sabato, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

Hesabu 28:11

Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;

Hesabu 28:12

pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng'ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja;

Hesabu 28:13

na sehemu ya kumi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwana-kondoo; kuwa sadaka ya kuteketezwa ya harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

Hesabu 28:14

Tena sadaka zake za vinywaji zitakuwa nusu ya hini ya divai kwa ng'ombe, na sehemu ya tatu ya hini kwa kondoo mume, na robo ya hini kwa mwana-kondoo; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika miezi yote ya mwaka.

Hesabu 28:15

Tena mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa Bwana itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

Hesabu 28:16

Tena, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, ni pasaka ya Bwana.

Hesabu 28:17

Siku ya kumi na tano ya mwezi huo patakuwa na sikukuu; mkate usiotiwa chachu utaliwa muda wa siku saba.

Hesabu 28:18

Siku ya kwanza patakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;

Hesabu 28:19

lakini mtaisongeza sadaka kwa njia ya moto, sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu;

Hesabu 28:20

pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta; mtasongeza sehemu ya kumi tatu kwa ng'ombe mmoja, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume;

Hesabu 28:21

na sehemu ya kumi moja utasongeza kwa kila mwana-kondoo, wale wana-kondoo saba;

Hesabu 28:22

tena mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.

Hesabu 28:23

Mtasongeza wanyama hao zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, iliyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.

Hesabu 28:24

Mtasongeza sadaka kwa mfano huu kila siku muda wa siku saba, chakula cha sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana; itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.

Hesabu 28:25

Na siku ya saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi.

Hesabu 28:26

Tena katika siku ya malimbuko, hapo mtakapomsongezea Bwana sadaka ya unga mpya katika sikukuu yenu ya majuma mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;

Hesabu 28:27

lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba;

Hesabu 28:28

pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng'ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume,

Hesabu 28:29

na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo, wa wale wana-kondoo saba;

Hesabu 28:30

na mbuzi mume mmoja, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.

Hesabu 28:31

Zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, mtasongeza wanyama hao (watakuwa wakamilifu kwenu), pamoja na sadaka zake za vinywaji.