Waamuzi Mlango 5 Judges

Waamuzi 5:1

Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;

Waamuzi 5:2

Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana.

Waamuzi 5:3

Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli.

Waamuzi 5:4

Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji.

Waamuzi 5:5

Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli.

Waamuzi 5:6

Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando.

Waamuzi 5:7

Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.

Waamuzi 5:8

Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli?

Waamuzi 5:9

Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini Bwana.

Waamuzi 5:10

Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.

Waamuzi 5:11

Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya Bwana; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa Bwana waliposhuka malangoni.

Waamuzi 5:12

Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.

Waamuzi 5:13

Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; Bwana alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.

Waamuzi 5:14

Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.

Waamuzi 5:15

Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.

Waamuzi 5:16

Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.

Waamuzi 5:17

Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake.

Waamuzi 5:18

Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.

Waamuzi 5:19

Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha.

Waamuzi 5:20

Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.

Waamuzi 5:21

Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.

Waamuzi 5:22

Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu.

Waamuzi 5:23

Ulaanini Merozi, alisema malaika wa Bwana, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia Bwana, Kumsaidia Bwana juu ya hao wenye nguvu.

Waamuzi 5:24

Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.

Waamuzi 5:25

Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima.

Waamuzi 5:26

Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.

Waamuzi 5:27

Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.

Waamuzi 5:28

Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?

Waamuzi 5:29

Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu.

Waamuzi 5:30

Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka.

Waamuzi 5:31

Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee Bwana.