Waamuzi Mlango 14 Judges

Waamuzi 14:1

Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti.

Waamuzi 14:2

Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe.

Waamuzi 14:3

Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana.

Waamuzi 14:4

Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la Bwana; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli.

Waamuzi 14:5

Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia.

Waamuzi 14:6

Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.

Waamuzi 14:7

Basi akatelemka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana.

Waamuzi 14:8

Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akageuka kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali.

Waamuzi 14:9

Akatwaa asali mikononi mwake akaenda mbele, huku akila alipokuwa akienenda, akawafikilia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba.

Waamuzi 14:10

Basi babaye akamtelemkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa vijana ndivyo walivyokuwa wakifanya.

Waamuzi 14:11

Basi ikawa hapo walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye.

Waamuzi 14:12

Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mwaweza kunionyesha katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo hapo nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini;

Waamuzi 14:13

lakini msipoweza kunionyesha ndipo hapo ninyi mtanipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia.

Waamuzi 14:14

Naye akawaambia, Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu.

Waamuzi 14:15

Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atuonyeshe hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo?

Waamuzi 14:16

Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, nami nikuambie wewe?

Waamuzi 14:17

Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili.

Waamuzi 14:18

Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali? Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba? Naye akawaambia, kwamba hamkulima na mtamba wangu,Hamngekitambua kitendawili changu.

Waamuzi 14:19

Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.

Waamuzi 14:20

Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.