Waamuzi Mlango 12 Judges

Waamuzi 12:1

Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako.

Waamuzi 12:2

Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao.

Waamuzi 12:3

Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, Bwana naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami?

Waamuzi 12:4

Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, mnaokaa kati ya Efraimu, na kati ya Manase.

Waamuzi 12:5

Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La;

Waamuzi 12:6

ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu.

Waamuzi 12:7

Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.

Waamuzi 12:8

Baada yake huyo, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.

Waamuzi 12:9

Alikuwa na wana thelathini; na binti thelathini akawapeleka waende mahali pengine, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba.

Waamuzi 12:10

Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.

Waamuzi 12:11

Baada yake huyo, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi.

Waamuzi 12:12

Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.

Waamuzi 12:13

Baada yake huyo, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli.

Waamuzi 12:14

Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wana-punda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane.

Waamuzi 12:15

Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.