1 Wafalme Mlango 15 1st Kings

1 Wafalme 15:1

Mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yeroboamu mwana wa Nebati, Abiya alianza kutawala juu ya Yuda.

1 Wafalme 15:2

Miaka mitatu akatawala huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.

1 Wafalme 15:3

Akaziendea dhambi zote za babaye, alizozifanya kabla yake; wala moyo wake haukuwa mkamilifu na Bwana, Mungu wake, kama moyo wa Daudi babaye.

1 Wafalme 15:4

Walakini kwa ajili ya Daudi, Bwana, Mungu wake, akampa taa humo Yerusalemu, amwinue mwanawe baada yake, na kuufanya imara Yerusalemu;

1 Wafalme 15:5

kwa sababu Daudi alifanya yaliyo mema machoni pa Bwana, wala hakukosa katika yote aliyomwamuru, siku zote za maisha yake, isipokuwa katika habari ya Uria, Mhiti.

1 Wafalme 15:6

Basi kulikuwa na vita kati ya Rehoboamu na Yeroboamu siku zote za maisha yake.

1 Wafalme 15:7

Na mambo yote ya Abiya yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Kulikuwa na vita kati ya Abiya na Yeroboamu.

1 Wafalme 15:8

Abiya akalala na baba zake, wakamzika mjini mwa Daudi. Akatawala Asa mwanawe mahali pake.

1 Wafalme 15:9

Mwaka wa ishirini wa Yeroboamu mfalme wa Israeli, Asa alianza kutawala juu ya Yuda.

1 Wafalme 15:10

Akatawala miaka arobaini na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Maaka, binti Absalomu.

1 Wafalme 15:11

Basi, Asa akafanya yaliyo mema machoni pa Mungu, kama alivyofanya babaye Daudi.

1 Wafalme 15:12

Akawafukuza mahanithi katika nchi, akaziondoa sanamu zote walizozifanya baba zake.

1 Wafalme 15:13

Hata na Maaka, mamaye, akamwondolea daraja yake asiwe malkia, kwa kuwa amefanya sanamu ya kuchukiza kwa Ashera; basi Asa akaikata sanamu yake akaiteketeza penye kijito cha Kidroni.

1 Wafalme 15:14

Lakini mahali pa juu hapakuondoshwa; ila moyo wake Asa ulikuwa mkamilifu kwa Bwana siku zake zote.

1 Wafalme 15:15

Akavileta vile vitu alivyovitakasa baba yake, na vile alivyovitakasa yeye mwenyewe, katika nyumba ya Bwana, fedha; na dhahabu, na vyombo.

1 Wafalme 15:16

Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.

1 Wafalme 15:17

Kisha, Baasha mfalme wa Israeli akaondoka juu ya Yuda, akaujenga Rama, ili asimwache mtu ye yote kutoka wala kuingia kwa Asa mfalme wa Yuda.

1 Wafalme 15:18

Ndipo Asa akazitwaa fedha zote na dhahabu zilizosalia katika hazina za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akazitia mikononi mwa watumishi wake; mfalme Asa akawatuma kwa Ben-hadadi, mwana wa Tabrimoni, mwana wa Hezioni, mfalme wa Shamu, aliyekaa Dameski, akasema,

1 Wafalme 15:19

Tumepatana mimi nawe, na baba yangu na baba yako; angalia, nimekuletea zawadi, fedha na dhahabu; basi nenda, uyavunje mapatano yako na Baasha mfalme wa Israeli, ili aniondokee mimi.

1 Wafalme 15:20

Naye Ben-hadadi akamsikiliza mfalme Asa, akawatuma wakuu wa majeshi yake juu ya miji ya Israeli, akapiga Iyoni, na Dani, na Abel-beth-maaka na Kinerothi yote, na nchi yote ya Naftali.

1 Wafalme 15:21

Ikawa Baasha aliposikia habari hiyo akaacha kuujenga Rama, akaenda akakaa Tirza.

1 Wafalme 15:22

Ndipo mfalme Asa akatangaza kwa Yuda pia; asiachiliwe mtu; nao wakayachukua mawe ya Rama na miti yake, aliyoijengea Baasha; naye mfalme Asa akajenga kwa vitu hivyo Geba wa Benyamini na Mispa.

1 Wafalme 15:23

Na mambo yote ya Asa yaliyosalia, na nguvu zake zote, na yote aliyoyafanya, na miji aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda? Lakini alipokuwa mzee alikuwa na ugonjwa wa miguu.

1 Wafalme 15:24

Asa akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake. Na Yehoshafati mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 15:25

Nadabu mwana wa Yeroboamu alianza kutawala juu ya Israeli, mwaka wa pili wa Asa mfalme wa Yuda, akatawala juu ya Israeli miaka miwili.

1 Wafalme 15:26

Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya baba yake, na kosa lake alilowakosesha Israeli.

1 Wafalme 15:27

Basi Baasha wa Ahiya, wa mbari ya Isakari, akamfanyia fitina; Baasha akampiga huko Gibethoni ulio wa Wafilisti; kwani Nadabu na Israeli wote walikuwa wakiuhusuru Gibethoni.

1 Wafalme 15:28

Mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda Baasha akamwua, akatawala mahali pake.

1 Wafalme 15:29

Ikawa mara alipotawala, akawapiga nyumba yote ya Yeroboamu. Hakumwachia Yeroboamu mwenye pumzi ye yote, hata alipomharibu sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mtumishi wake Ahiya, Mshiloni;

1 Wafalme 15:30

kwa sababu ya makosa yake Yeroboamu aliyoyakosa, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; kwa sababu ya chukizo lake alilomchukiza Bwana, Mungu wa Israeli, hata kumghadhibisha.

1 Wafalme 15:31

Basi mambo yote ya Nadabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

1 Wafalme 15:32

Kulikuwa na vita kati ya Asa na Baasha mfalme wa Israeli siku zao zote.

1 Wafalme 15:33

Katika mwaka wa tatu wa Asa mfalme wa Yuda, Baasha mwana wa Ahiya alianza kutawala juu ya Israeli wote huko Tirza, akatawala miaka ishirini na minne.

1 Wafalme 15:34

Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana akaiendea njia ya Yeroboamu, na kosa lake ambalo kwa hilo aliwakosesha Israeli.