1 Wafalme Mlango 17 1st Kings

1 Wafalme 17:1

Basi Eliya Mtishbi, wa wageni wa Gileadi, akamwambia Ahabu, Kama Bwana, Mungu wa Israeli, aishivyo, ambaye ninasimama mbele zake, hakutakuwa na umande wala mvua miaka hii, ila kwa neno langu.

1 Wafalme 17:2

Neno la Bwana likamjia, kusema,

1 Wafalme 17:3

Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.

1 Wafalme 17:4

Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.

1 Wafalme 17:5

Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani.

1 Wafalme 17:6

Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.

1 Wafalme 17:7

Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.

1 Wafalme 17:8

Neno la Bwana likamjia, kusema,

1 Wafalme 17:9

Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.

1 Wafalme 17:10

Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.

1 Wafalme 17:11

Alipokuwa akienda kuleta, akamwita akasema, Niletee, nakuomba, kipande cha mkate mkononi mwako.

1 Wafalme 17:12

Naye akasema, Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, sina mkate, ila konzi ya unga katika pipa, na mafuta kidogo katika chupa; nami ninaokota kuni mbili ili niingie nijipikie nafsi yangu na mwanangu, tuule tukafe.

1 Wafalme 17:13

Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao.

1 Wafalme 17:14

Kwa kuwa Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile Bwana atakapoleta mvua juu ya nchi.

1 Wafalme 17:15

Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi.

1 Wafalme 17:16

Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa kinywa cha Eliya.

1 Wafalme 17:17

Ikawa, baada ya hayo, mwana wake yule mwanamke, bibi wa nyumba ile, akaugua; ugonjwa wake ukazidi hata akawa hana pumzi tena.

1 Wafalme 17:18

Akamwambia Eliya, Nina nini nawe, Ee mtu wa Mungu? Je! Umenijia ili dhambi yangu ikumbukwe, ukamwue mwanangu?

1 Wafalme 17:19

Akamwambia, Nipe mwanao. Akamtoa katika kifua chake, akamchukua juu chumbani mle alimokaa mwenyewe, akamlaza kitandani pake.

1 Wafalme 17:20

Akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, je! Umemtenda mabaya mjane huyu ninayekaa kwake hata kumfisha mwanawe.

1 Wafalme 17:21

Akajinyosha juu ya mtoto mara tatu, akamwomba Bwana, akanena, Ee Bwana, Mungu wangu, nakusihi, roho ya mtoto huyu imrudie ndani yake tena.

1 Wafalme 17:22

Bwana akaisikia sauti ya Eliya; na roho ya mtoto ikamrudia, akafufuka.

1 Wafalme 17:23

Eliya akamtwaa mtoto, akamchukua toka orofani mpaka chini ya nyumba ile, akampa mama yake. Eliya akanena, Tazama, mwanao yu hai.

1 Wafalme 17:24

Mwanamke akamwambia Eliya, Sasa najua ya kuwa wewe ndiwe mtu wa Mungu, na ya kuwa neno la Bwana kinywani mwako ni kweli.