1 Wafalme Mlango 22 1st Kings

1 Wafalme 22:1

Wakakaa miaka mitatu pasipo vita kati ya Shamu na Israeli.

1 Wafalme 22:2

Ikawa, mwaka wa tatu Yehoshafati mfalme Wa Yuda akamshukia mfalme wa Israeli.

1 Wafalme 22:3

Mfalme wa Israeli akawaambia watumishi wake, Je! Hamjui ya kuwa Ramoth-Gileadi ni yetu? Nasi tumenyamaza tusiitwae mkononi mwa mfalme wa Shamu?

1 Wafalme 22:4

Akamwambia Yehoshafati, Je! Utakwenda nami tupigane na Ramoth-gileadi? Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Mimi ni kama wewe, na watu wangu ni kama watu wako na farasi zangu ni kama farasi zako.

1 Wafalme 22:5

Yehoshafati akamwambia mfalme wa Israeli, Uulize leo, nakusihi, kwa neno la Bwana.

1 Wafalme 22:6

Ndipo mfalme wa Israeli akawakusanya pamoja manabii, kama watu mia nne. Akawaambia Je! Niende juu ya Ramoth-Gileadi kuupiga vita, au ninyamaze? Wakasema Kwea; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.

1 Wafalme 22:7

Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hayupo hapa nabii wa Bwana tena, ili tumwulize yeye?

1 Wafalme 22:8

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Yupo mtu mmoja, ambaye tungeweza kumwuliza Bwana kwa yeye, yaani Mikaya mwana wa Imla; lakini namchukia; kwa sababu hanibashirii mema, ila mabaya. Yehoshafati akasema, La! Mfalme asiseme hivi.

1 Wafalme 22:9

Ndipo mfalme wa Israeli akamwita akida, akamwambia, mlete hima Mikaya mwana wa Imla.

1 Wafalme 22:10

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda walikuwa wakikaa kila mtu katika kiti chake cha enzi, wamevaa mavazi yao, katika sakafu langoni pa Samaria; na manabii wote wakafanya unabii mbele yao.

1 Wafalme 22:11

Na Zedekia mwana wa Kenaana akajifanyia pembe za chuma, akasema, Bwana asema hivi, Kwa hizo utawasukuma Washami, hata waharibike.

1 Wafalme 22:12

Na manabii wote wakasema hivyo kwa unabii, wakisema, Kwea Ramoth-Gileadi, ukafanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.

1 Wafalme 22:13

Na yule mjumbe, aliyekwenda kumwita Mikaya, akamwambia, akasema, Angalia sasa, maneno ya manabii kwa kinywa kimoja husema mema kwa mfalme; neno lako na liwe, nakusihi, kama neno la mmojawapo wao, ukaseme mema.

1 Wafalme 22:14

Mikaya akasema, Kama Bwana aishivyo, neno lile Bwana aniambialo, ndilo nitakalolinena.

1 Wafalme 22:15

Na alipokuja kwa mfalme, mfalme alimwambia, Je! Mikaya, tuende Ramoth-Gileadi kupiga vita, au tunyamaze? Akamwambia, Kwea, ufanikiwe; kwa kuwa Bwana atautia mkononi mwa mfalme.

1 Wafalme 22:16

Mfalme akamwambia, Mara ngapi nikuapishe usiniambie neno ila yaliyo kweli, kwa jina la Bwana?

1 Wafalme 22:17

Akasema, Naliwaona Waisraeli wote wametawanyika milimani, kama kondoo wasio na mchungaji. Bwana akasema, Hawa hawana bwana; na warudi kila mtu nyumbani kwake kwa amani.

1 Wafalme 22:18

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Je! Sikukuambia, hatanibashiria mema, ila mabaya?

1 Wafalme 22:19

Mikaya akasema, Sikia basi neno la Bwana; Nalimwona Bwana ameketi katika kiti chake cha enzi, na jeshi lote la mbinguni wamesimama upande wa mkono wake wa kuume na wa kushoto.

1 Wafalme 22:20

Bwana akasema, Ni nani atakayemdanganya Ahabu, ili akwee Ramoth-Gileadi akaanguke? Basi huyu akasema hivi; na huyu hivi.

1 Wafalme 22:21

Akatoka pepo, akasimama mbele za Bwana, akasema, Mimi nitamdanganya.

1 Wafalme 22:22

Bwana akamwambia, Jinsi gani? Akasema, Nitaondoka, na kuwa pepo wa uongo kinywani mwa manabii wake wote. Akasema, Utamdanganya, na kudiriki pia; ondoka ukafanye hivyo.

1 Wafalme 22:23

Basi angalia, Bwana ametia pepo wa uongo kinywani mwa manabii wako hawa wote; naye Bwana amenena mabaya juu yako.

1 Wafalme 22:24

Ndipo akakaribia Zedekia, mwana wa Kenaana, akampiga Mikaya kofi la shavu, akasema, Roho ya Bwana alitokaje kwangu ili aseme na wewe?

1 Wafalme 22:25

Mikaya akamwambia, Angalia, utaona siku ile utakapoingia katika chumba cha ndani ili ujifiche.

1 Wafalme 22:26

Mfalme wa Israeli akasema, Mchukueni Mikaya, mkamrudishe kwa Amoni mkuu wa mji na kwa Yoashi mwana wa mfalme;

1 Wafalme 22:27

mkaseme, Mfalme asema hivi, Mtieni mtu huyu gerezani, mkamlishe kwa chakula cha shida, na maji ya shida, hata nitakaporudi kwa amani.

1 Wafalme 22:28

Mikaya akasema, Ukirudi kabisa kwa amani, Bwana hakusema kwa mimi. Akasema, Sikieni, enyi watu wote.

1 Wafalme 22:29

Basi mfalme wa Israeli na Yehoshafati mfalme wa Yuda wakakwea mpaka Ramoth-Gileadi.

1 Wafalme 22:30

Mfalme wa Israeli akamwambia Yehoshafati, Nitajibadilisha, na kuingia vitani; lakini wewe uvae mavazi yako. Mfalme wa Israeli akajibadilisha, akaingia vitani.

1 Wafalme 22:31

Basi mfalme wa Shamu alikuwa amewaamuru wakuu wa magari yake thelathini na wawili, akisema, Msipigane na mdogo wala mkuu, ila na mfalme wa Israeli peke yake.

1 Wafalme 22:32

Ikawa wakuu wa magari walipomwona Yehoshafati, wakasema, Huyo ndiye mfalme wa Israeli Wakageuka juu yake ili wapigane naye; naye Yehoshafati akapiga ukelele.

1 Wafalme 22:33

Ikawa, wakuu wa magari walipoona ya kuwa siye mfalme wa Israeli, wakageuka nyuma wasimfuate.

1 Wafalme 22:34

Mtu mmoja akavuta upinde kwa kubahatisha, akampiga mfalme wa Israeli mahali pa kuungana mavazi yake ya chuma; kwa hiyo akamwambia mwendesha gari lake, Geuza mkono wako, unichukue kutoka katika majeshi; kwa kuwa nimejeruhiwa sana.

1 Wafalme 22:35

Pigano likazidi siku ile; mfalme akategemezwa garini mwake, kinyume cha Washami, hata jioni akafa; damu ikatoka katika jeraha yake ndani ya gari.

1 Wafalme 22:36

Ikapigwa mbiu jeshini, jua likichwa, kusema, Kila mtu aende mjini kwake, na kila mtu shambani kwake.

1 Wafalme 22:37

Hivyo akafa mfalme, akachukuliwa Samaria, wakamzika mfalme huko Samaria.

1 Wafalme 22:38

Wakaliosha gari penye birika la Samaria, na mbwa wakaramba damu yake; (basi ndipo walipooga makahaba); sawasawa na neno la Bwana alilolinena.

1 Wafalme 22:39

Na mambo yote ya Ahabu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na nyumba ya pembe aliyoijenga, na miji yote aliyoijenga, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

1 Wafalme 22:40

Basi Ahabu akalala na baba zake; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 22:41

Yehoshafati mwana wa Asa alianza kutawala juu ya Yuda, katika mwaka wa nne wa Ahabu mfalme wa Israeli.

1 Wafalme 22:42

Yehoshafati alikuwa mwenye miaka thelathini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na mitano huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Azuba binti Shilhi.

1 Wafalme 22:43

Akaiendea njia yote ya Asa babaye; wala hakugeuka, akifanya yaliyo mema machoni pa Bwana. Lakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu wakafukiza uvumba katika mahali pa juu.

1 Wafalme 22:44

Yehoshafati akafanya amani na mfalme wa Israeli.

1 Wafalme 22:45

Na mambo yote ya Yehoshafati yaliyosalia, na uthabiti alioufanya, na jinsi alivyopiga vita, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?

1 Wafalme 22:46

Tena mahanithi waliosalia, hao waliosalia siku za Asa baba yake, akawaondoa katika nchi.

1 Wafalme 22:47

Wala hapakuwa na mfalme katika Edomu; naibu alikuwa ndiye mfalme.

1 Wafalme 22:48

Yehoshafati akafanya merikebu za Tarshishi ziende Ofiri kuchukua dhahabu; walakini hazikuenda; kwa maana merikebu zilivunjika huko Esion-geberi.

1 Wafalme 22:49

Ndipo Ahazia mwana wa Ahabu akamwambia Yehoshafati, Watumishi wangu na waende pamoja na watumishi wako merikebuni. Lakini Yehoshafati hakukubali.

1 Wafalme 22:50

Basi Yehoshafati akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze mjini mwa Daudi baba yake; na Yehoramu mwanawe akatawala mahali pake.

1 Wafalme 22:51

Ahazia mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria, katika mwaka wa kumi na saba wa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akatawala miaka miwili juu ya Israeli.

1 Wafalme 22:52

Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, akaiendea njia ya babaye, na njia ya mamaye, na njia ya Yeroboamu mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli.

1 Wafalme 22:53

Akamtumikia Baali, akamwabudu, akamghadhibisha Bwana, Mungu wa Israeli, kwa mfano wa mambo yote aliyoyafanya baba yake.