1 Wafalme Mlango 20 1st Kings

1 Wafalme 20:1

Basi, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya jeshi lake lote; nao walikuwapo wafalme thelathini na wawili pamoja naye, na farasi, na magari: akakwea akauhusuru Samaria, akaupiga vita.

1 Wafalme 20:2

Akatuma wajumbe kwa Ahabu mfalme wa Israeli, mjini, akamwambia, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi.

1 Wafalme 20:3

Fedha yako na dhahabu yako ni zangu mimi; na wakezo na wanao, walio wema, ni wangu.

1 Wafalme 20:4

Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Ni kama ulivyosema, bwana wangu, mfalme; mimi ni wako, na vyote nilivyo navyo.

1 Wafalme 20:5

Wajumbe wakarudi tena, wakasema, Ndivyo asemavyo Ben-hadadi, Hakika nimetuma kwako kusema, Fedha yako, na dhahabu yako, na wake zako, na wanao, utanitolea mimi;

1 Wafalme 20:6

lakini kesho kama wakati huu nitatuma kwako watumwa wangu, ili watazame-tazame nyumba yako na nyumba za watumwa wako; na itakuwa kila kipendezacho machoni pako watakitia mikononi mwao,na kukichukua.

1 Wafalme 20:7

Ndipo mfalme wa Israeli, akawaita wazee wote wa nchi, akasema, Angalieni, nawaomba, mwone, kwamba huyu ataka madhara; maana ametuma kwangu kutaka wake zangu na watoto wangu; na fedha yangu na dhahabu yangu, sikumkatalia.

1 Wafalme 20:8

Wakamwambia wazee wote na watu wote, Usisikie, wala usikubali.

1 Wafalme 20:9

Kwa hiyo akawaambia wale wajumbe wa Ben-hadadi, Mwambieni bwana wangu mfalme, Kila uliyotuma kumtakia mtumwa wako kwanza, nitafanya, ila neno hili siwezi kulifanya. Basi wajumbe wakaenda zao, wakamrudishia maneno hayo.

1 Wafalme 20:10

Ndipo Ben-hadadi akatuma kwake, akasema, Miungu wanifanyie hivi na kuzidi, yakiwa mavumbi ya Samaria yatatosha makonzi ya watu wote walio miguuni pangu.

1 Wafalme 20:11

Mfalme wa Israeli akajibu, akasema, Mwambieni, Avaaye asijisifu kama avuaye.

1 Wafalme 20:12

Ikawa, Ben-hadadi alipolisikia neno hilo, naye alikuwa akinywa, yeye na wafalme, mabandani, aliwaambia watumwa wake, Jipangeni. Wakajipanga juu ya mji.

1 Wafalme 20:13

Na tazama, nabii akamjia Ahabu mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Je! Umeona makutano haya yote walio wengi? Angalia, nitawatia leo mkononi mwako; nawe utajua ya kuwa ndimi Bwana.

1 Wafalme 20:14

Ahabu akanena, Kwa nani? Akasema, Bwana asema hivi, Kwa vijana wa maliwali wa majimbo. Ndipo akanena, Ni nani atakayepanga vita? Naye akajibu, Ni wewe.

1 Wafalme 20:15

Ndipo akawaandika vijana wa maliwali wa majimbo, nao walikuwa mia mbili thelathini na wawili; kisha baada ya hao akawaandika watu wote, wana wa Israeli wote, nao walikuwa elfu saba.

1 Wafalme 20:16

Wakatoka wakati wa adhuhuri. Lakini Ben-hadadi alikuwa akinywa hata kulewa mabandani, yeye na wale wafalme thelathini na wawili waliomsaidia.

1 Wafalme 20:17

Wakatoka wale vijana wa maliwali wa majimbo wakitangulia; na Ben-hadadi akatuma watu, nao wakamwambia, Wako watu wametoka katika Samaria.

1 Wafalme 20:18

Akasema, Kwamba wametoka kwa amani, wakamateni wa hai; au kwamba wametoka kwa vita, wakamateni wa hai.

1 Wafalme 20:19

Basi wakatoka mjini hao vijana wa maliwali wa majimbo, na jeshi nyuma yao.

1 Wafalme 20:20

Wakapiga kila mmoja mtu wake; Washami wakakimbia, na Israeli wakawafuatia; Ben-hadadi mfalme wa Shamu akaokoka amepanda farasi, pamoja na wapandao farasi.

1 Wafalme 20:21

Mfalme wa Israeli akatoka, akawapiga farasi na magari, akawapiga Washami pigo kubwa.

1 Wafalme 20:22

Naye yule nabii akamjia mfalme wa Israeli, akamwambia, Enenda, kusanya nguvu zako, ujue, na kuangalia ufanyavyo; kwa maana mwakani mfalme wa Shamu atakuja juu yako.

1 Wafalme 20:23

Basi watumwa wake mfalme wa Shamu wakamwambia, Mungu wao ni mungu wa milima; ndiyo sababu ya kutushinda sisi; lakini na tupigane nao katika nchi tambarare, na hakika tutawashinda wao.

1 Wafalme 20:24

Ufanye neno hili; uwaondoe hao wafalme, kila mtu atoke mahali pake, ukaweke majemadari mahali pao.

1 Wafalme 20:25

Kisha ujihesabie jeshi, kama jeshi lililokupotea, farasi kwa farasi na gari kwa gari; nasi tutapigana nao katika nchi tambarare, na bila shaka tutawashinda. Akaisikiliza sauti yao, akafanya kama hivyo.

1 Wafalme 20:26

Basi ikawa mwakani, Ben-hadadi akawahesabu Washami, akakwea mpaka Afeki ili apigane na Israeli.

1 Wafalme 20:27

Wana wa Israeli nao wakahesabiwa, wakapewa vyakula, wakaenda kupigana nao; wakatua wana wa Israeli mbele yao kama vikundi viwili vya wana-mbuzi; bali Washami wakaijaza nchi.

1 Wafalme 20:28

Akaja yule mtu wa Mungu, akamwambia mfalme wa Israeli, akasema, Bwana asema hivi, Kwa sababu Washami wamesema, Bwana ni Mungu wa milima wala si Mungu wa nchi tambarare; basi nitawatia makutano haya yote walio wengi mkononi mwako, nanyi mtajua ya kuwa ndimi Bwana.

1 Wafalme 20:29

Wakatua kuelekeana muda wa siku saba. Ikawa siku ya saba vikapangwa vita; wana wa Israeli wakawapiga miongoni mwa Washami siku moja watu mia elfu waendao kwa miguu.

1 Wafalme 20:30

Lakini waliosalia wakakimbia mpaka Afeki, mjini; na ukuta ukaanguka juu ya watu ishirini na saba elfu waliosalia. Ben-hadadi naye akakimbia, akaingia mjini, katika chumba cha ndani.

1 Wafalme 20:31

Watumwa wake wakamwambia, Angalia sasa, tumesikia ya kuwa wafalme wa nyumba ya Israeli ni wafalme wenye rehema; tafadhali, tuvae magunia viunoni, na kamba vichwani, tumtokee mfalme wa Israeli; labda atakuokoa roho yako.

1 Wafalme 20:32

Basi wakajifungia magunia viunoni, na kamba vichwani, wakamjia mfalme wa Israeli, wakasema, Mtumwa wako Ben-hadadi asema Roho yangu, nakusihi, iishi. Akasema, Je! Yu hai bado? Ni ndugu yangu yeye.

1 Wafalme 20:33

Wale watu wakaangalia sana, wakafanya haraka kulishika neno hilo kama ni nia yake, wakasema, Ndugu yako, Ben-hadadi. Akasema, Haya! Nendeni mkamlete. Ndipo Ben-hadadi akamtokea, naye akampandisha garini.

1 Wafalme 20:34

Na Ben-hadadi akamwambia, Miji ile baba yangu aliyomnyang'anya baba yako nitairudisha; nawe utajifanyia njia huko Dameski, kama baba yangu aliyoifanya huko Samaria. Ahabu akasema, Nami nitakuacha kwa mapatano haya. Akafanya mapatano naye, akamwacha.

1 Wafalme 20:35

Basi, mtu mmoja wa wana wa manabii akamwambia mwenzake kwa neno la Bwana, Nipige, nakusihi. Akakataa yule kumpiga.

1 Wafalme 20:36

Akamwambia, Kwa sababu hukuisikiliza sauti ya Bwana, angalia, mara ukitoka kwangu simba atakuua. Na mara alipotoka kwake, simba alimwona, akamwua.

1 Wafalme 20:37

Ndipo akaona mtu mwingine, akasema, Nipige, nakusihi. Yule mtu akampiga, hata kumpiga na kumtia jeraha.

1 Wafalme 20:38

Basi yule nabii akaenda akamngoja mfalme njiani, amejibadilisha kwa kilemba juu ya macho yake.

1 Wafalme 20:39

Ikawa mfalme alipopita, alimwita mfalme; akasema, Mtumwa wako aliingia katikati ya pigano; na tazama, mtu mmoja akanigeukia akaniletea mtu, akaniambia, Umlinde mtu huyu; akipotea kwa njia yo yote, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, au utatoa talanta ya fedha.

1 Wafalme 20:40

Ikawa mtumishi wako alipokuwa akitenda haya na haya, yule akaenda zake. Mfalme wa Israeli akamwambia, Ndivyo itakavyokuwa hukumu yako; umejihukumu mwenyewe.

1 Wafalme 20:41

Akafanya haraka akakiondoa kilemba machoni mwake, mfalme wa Israeli akamtambua kuwa ni mmoja wao manabii.

1 Wafalme 20:42

Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa sababu umemwachilia atoke mkononi mwako mtu niliyemweka ili aangamizwe kabisa, roho yako itakuwa mahali pa roho yake, na watu wako mahali pa watu wake.

1 Wafalme 20:43

Mfalme wa Israeli akaenda nyumbani kwake na moyo mzito, mwenye hasira, akaja Samaria.