1 Wafalme Mlango 10 1st Kings

1 Wafalme 10:1

Na malkia wa Sheba aliposikia habari za Sulemani juu ya jina la Bwana, alikuja ili amjaribu kwa maswali ya fumbo.

1 Wafalme 10:2

Akaingia Yerusalemu na wafuasi wengi sana, na ngamia wachukuao manukato, na dhahabu nyingi sana, na vito vya thamani; alipomfikilia Sulemani, akazungumza naye mambo yote aliyokuwa nayo moyoni.

1 Wafalme 10:3

Naye Sulemani akamfumbulia maswali yake yote; wala hakukuwa na neno alilofichiwa mfalme asimwambie.

1 Wafalme 10:4

Naye malkia wa Sheba alipoona hekima yote ya Sulemani, na nyumba aliyokuwa ameijenga,

1 Wafalme 10:5

na chakula cha mezani pake, na watumishi wake walivyokaa, na kusimamia kwao wangoje wake, na mavazi yao, na wanyweshaji wake, na daraja yake ya kupandia mpaka nyumba ya Bwana, roho yake ilizimia.

1 Wafalme 10:6

Akamwambia mfalme, Ndizo kweli habari zile nilizozisikia katika nchi yangu za mambo yako na za hekima yako.

1 Wafalme 10:7

Lakini mimi sikuzisadiki habari hizo, hata nilipokuja na kuona kwa macho yangu; tena, tazama, sikuambiwa nusu; wewe umezidi kwa hekima na kufanikiwa kuliko habari nilizozisikia.

1 Wafalme 10:8

Heri watu wako, na heri watumishi hawa wako, wasimamao mbele yako siku zote, wakisikia hekima yako.

1 Wafalme 10:9

Na ahimidiwe Bwana, Mungu wako, aliyependezwa nawe, ili akuweke juu ya kiti cha enzi cha Israeli; kwa kuwa Bwana amewapenda Israeli milele, kwa hiyo amekufanya kuwa mfalme, ufanye hukumu na haki.

1 Wafalme 10:10

Basi akampa mfalme talanta za dhahabu mia na ishirini, na manukato mengi, mengi sana, na vito vya thamani; wala haukuja tena wingi wa manukato, kama hayo malkia wa Sheba aliyompa mfalme Sulemani.

1 Wafalme 10:11

Tena merikebu za Hiramu, zilizochukua dhahabu kutoka Ofiri, zikaleta kutoka Ofiri miti ya msandali mingi sana, na vito vya thamani.

1 Wafalme 10:12

Mfalme akafanya kwa mia hiyo ya msandali nguzo za nyumba ya Bwana, na za nyumba ya mfalme, na vinubi na vinanda vya hao waimbaji; wala haikuja miti ya msandali kama hiyo, wala haikuonekana, hata leo.

1 Wafalme 10:13

Naye mfalme Sulemani akampa malkia wa Sheba haja yake yote, kila alilotaka, zaidi ya hayo aliyopewa na Sulemani kwa ukarimu wake wa kifalme. Basi, akarudi akaenda zake katika nchi yake, yeye na watumishi wake.

1 Wafalme 10:14

Basi uzani wa dhahabu iliyomfikia Sulemani mwaka mmoja, ndio talanta mia sita sitini na sita,

1 Wafalme 10:15

zaidi ya faida ya wachuuzi, na bidhaa ya wafanya biashara, na ya wafalme wote wa hao waliochanganyika, na ya maliwali wa nchi.

1 Wafalme 10:16

Mfalme Sulemani akafanya ngao mia mbili za dhahabu iliyofuliwa; kila ngao moja ilipata shekeli mia sita za dhahabu.

1 Wafalme 10:17

Na vigao mia tatu vya dhahabu iliyofuliwa; kila kigao kimoja kilipata mane tatu za dhahabu. Mfalme akaviweka katika nyumba ya mwitu wa Lebanoni.

1 Wafalme 10:18

Tena mfalme akafanya kiti cha enzi kikubwa cha pembe, akakifunikiza kwa dhahabu iliyo safi.

1 Wafalme 10:19

Kiti kile kilikuwa na daraja sita, na juu yake kimeviringana nyuma; na mikono huko na huko mahali pa kuketi, na simba wawili wakisimama kando ya hiyo mikono.

1 Wafalme 10:20

Na simba kumi na wawili wamesimama juu ya daraja sita huko na huko; wala hakikufanyika kwa mkono wake katika ufalme wo wote.

1 Wafalme 10:21

Na vyombo vyote vya kunywea vya mfalme Sulemani vilikuwa vya dhahabu, na vyombo vyote vya nyumba ya mwitu wa Lebanoni vilikuwa vya dhahabu iliyosafika; hakuna vya fedha, fedha haikuhesabiwa kuwa kitu siku za Sulemani.

1 Wafalme 10:22

Kwa kuwa mfalme alikuwa na merikebu za Tarshishi baharini pamoja na merikebu za Hiramu; mara moja katika miaka mitatu huja merikebu za Tarshishi, zikileta dhahabu, na fedha, na pembe, na nyani, na tausi.

1 Wafalme 10:23

Basi mfalme Sulemani akawapita wafalme wote wa duniani kwa mali, na kwa hekima.

1 Wafalme 10:24

Ulimwengu wote ukamtafuta Sulemani uso wake, ili waisikie hekima yake, Mungu aliyomtia moyoni.

1 Wafalme 10:25

Wakaleta kila mtu zawadi yake, vyombo vya fedha, na vyombo vya dhahabu, na mavazi, na silaha, na manukato, na farasi, na nyumbu, hesabu yake ya mwaka kwa mwaka.

1 Wafalme 10:26

Sulemani akakusanya magari na wapandao farasi; naye alikuwa na magari elfu na mia nne, na wapandao farasi kumi na mbili elfu, aliowaweka katika miji ya magari, na pamoja na mfalme huko Yerusalemu.

1 Wafalme 10:27

Mfalme akafanya fedha humo Yerusalemu kuwa kama mawe, na mierezi akaifinya kuwa kama mikuyu iliyomo Shefela, kwa kuwa mingi.

1 Wafalme 10:28

Nao farasi aliokuwa nao Sulemani wakaletwa toka Misri; wakapewa wafanya biashara wake mfalme kwa makundi, kila kundi na thamani yake.

1 Wafalme 10:29

Tena gari huja kutoka katika Misri kwa shekeli mia sita za fedha, na farasi mmoja kwa mia hamsini; vivyo watu wakawaletea wafalme wote wa Wahiti, na wafalme wa Shamu, mikononi mwao.