1 Wafalme Mlango 18 1st Kings

1 Wafalme 18:1

Ikawa baada ya siku nyingi, neno la Bwana likamjia Eliya, katika mwaka wa tatu, kusema, Enenda, ukajionyeshe kwa Ahabu; nami nitaleta mvua juu ya nchi.

1 Wafalme 18:2

Basi Eliya akaenda ili ajionyeshe kwa Ahabu. Na njaa ilikuwa nzito katika Samaria.

1 Wafalme 18:3

Ahabu akamwita Obadia, aliyekuwa juu ya nyumba yake; (na huyu Obadia alikuwa mwenye kumcha Bwana sana;

1 Wafalme 18:4

kwa kuwa ikawa, Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana, Obadia akatwaa manabii mia, akawaficha hamsini hamsini katika pango, akawalisha chakula na kuwapa maji).

1 Wafalme 18:5

Ahabu akamwambia Obadia, Pita katika nchi, kwenye chemchemi zote za maji, na vijito vyote; labda tutapata majani, tuwahifadhi hai farasi na nyumbu, tusipate hasara ya hao wanyama wote.

1 Wafalme 18:6

Basi wakaigawanya nchi, ili wapite katika nchi yote; Ahabu akaenda zake njia moja peke yake, na Obadia akaenda zake njia nyingine peke yake.

1 Wafalme 18:7

Na Obadia alipokuwa njiani, kumbe! Eliya akakutana naye. Akamtambua, akaanguka kifudifudi, akanena, Je! Ni wewe, bwana wangu Eliya?

1 Wafalme 18:8

Akamjibu, Ni mimi. Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

1 Wafalme 18:9

Akamwambia, Nimekosa nini, hata unitie mimi mtumishi wako mkononi mwa Ahabu, aniue?

1 Wafalme 18:10

Kama Bwana, Mungu wako, aishivyo, hakuna taifa wala ufalme ambao bwana wangu hakutuma watu wakutafute; na waliposema, Hayupo, akawaapisha ule ufalme, na taifa, ya kwamba hawakukuona.

1 Wafalme 18:11

Nawe sasa wasema, Enenda, umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo.

1 Wafalme 18:12

Na itakuwa, mara mimi nikiondoka kwako, roho ya Bwana atakuchukua uende nisikojua; nami nitakapokwenda kumwambia Ahabu, naye asipokuona, ataniua, lakini mimi mtumishi wako namcha Bwana tangu ujana wangu.

1 Wafalme 18:13

Je! Bwana wangu hakuambiwa nilivyofanya hapo Yezebeli alipowaua manabii wa Bwana? Jinsi nilivyowaficha manabii wa Bwana, watu mia, hamsini hamsini katika pango, nikawalisha chakula na kuwapa maji?

1 Wafalme 18:14

Nawe sasa wasema, Enenda umwambie bwana wako, Tazama, Eliya yupo; basi, ataniua.

1 Wafalme 18:15

Eliya akasema, Kama Bwana wa majeshi aishivyo ambaye ninasimama mbele zake, hakika nitajionyesha kwake leo.

1 Wafalme 18:16

Basi, Obadia akaenda zake amwone Ahabu, akamwambia; naye Ahabu akaenda kumlaki Eliya.

1 Wafalme 18:17

Ikawa, Ahabu alipomwona Eliya, Ahabu akamwambia, Je! Ni wewe, Ewe mtaabishaji wa Israeli?

1 Wafalme 18:18

Naye akajibu, Si mimi niliyewataabisha Israeli; bali ni wewe, na nyumba ya baba yako, kwa kuwa mmeziacha amri za Bwana; nawe umewafuata mabaali.

1 Wafalme 18:19

Basi sasa upeleke watu, unikusanyie jamii ya Israeli katika mlima wa Karmeli, na wale manabii wa Baali mia nne na hamsini, na wale manabii wa Ashera mia nne, walao chakula mezani pa Yezebeli.

1 Wafalme 18:20

Basi, Ahabu akapeleka watu kwa wana wa Israeli wote, akawakusanya manabii pamoja katika mlima wa Karmeli.

1 Wafalme 18:21

Naye Eliya akawakaribia watu wote, akanena, Mtasita-sita katikati ya mawazo mawili hata lini? Bwana akiwa ndiye Mungu, mfuateni; bali ikiwa Baali ni Mungu, haya! Mfuateni yeye. Wale watu hawakumjibu neno.

1 Wafalme 18:22

Ndipo Eliya akawaambia watu, Mimi nimesalia, mimi peke yangu, nabii wa Bwana; lakini manabii wa Baali ni watu mia nne na hamsini.

1 Wafalme 18:23

Kwa hiyo na watutolee ng'ombe wawili; wao na wajichagulie ng'ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeza huyo ng'ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini.

1 Wafalme 18:24

Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la Bwana; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. Watu wote wakajibu wakasema, Maneno haya ni mazuri.

1 Wafalme 18:25

Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng'ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini.

1 Wafalme 18:26

Wakamtwaa yule ng'ombe waliyepewa, wakamtengeza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri, wakisema, Ee Baali, utusikie. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu. Nao wakaruka-ruka juu ya madhabahu waliyoifanya.

1 Wafalme 18:27

Ikawa, wakati wa adhuhuri, Eliya akawafanyia dhihaka, akasema, Mwiteni kwa sauti kuu; maana ni mungu huyo; labda anazungumza, au ana shughuli, au anasafiri, au labda amelala, sharti aamshwe.

1 Wafalme 18:28

Wakapiga kelele, wakajikata-kata kwa visu na vyembe kama ilivyo desturi yao, hata damu ikawachuruzika.

1 Wafalme 18:29

Ikawa, wakati wa adhuhuri ulipopita, walitabiri hata wakati wa kutoa dhabihu ya jioni; lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.

1 Wafalme 18:30

Kisha Eliya akawaambia watu wote, Nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya Bwana iliyovunjika.

1 Wafalme 18:31

Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo, aliyejiliwa na neno la Bwana na kuambiwa, Jina lako litakuwa Israeli.

1 Wafalme 18:32

Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la Bwana; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu.

1 Wafalme 18:33

Kisha akazipanga zile kuni, akamkata yule ng'ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni. Akasema, Jazeni mapipa manne maji, mkayamwage juu ya sadaka ya kuteketezwa, na juu ya kuni.

1 Wafalme 18:34

Akasema, Fanyeni mara ya pili. Wakafanya mara ya pili. Akasema, Fanyeni mara ya tatu. Wakafanya mara ya tatu.

1 Wafalme 18:35

Yale maji yakaizunguka madhabahu; akaujaza mfereji maji.

1 Wafalme 18:36

Ikawa, wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, Eliya nabii akakaribia, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Ibrahimu, na wa Isaka, na wa Israeli, na ijulikane leo ya kuwa wewe ndiwe Mungu katika Israeli, na ya kuwa mimi ni mtumishi wako, na ya kuwa nimefanya mambo haya yote kwa neno lako.

1 Wafalme 18:37

Unisikie, Ee Bwana, unisikie, ili watu hawa wajue ya kuwa wewe, Bwana, ndiwe Mungu, na ya kuwa wewe umewageuza moyo wakurudie.

1 Wafalme 18:38

Ndipo moto wa Bwana ukashuka, ukaiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na kuni, na mawe, na mavumbi, ukayaramba yale maji yaliyokuwamo katika mfereji.

1 Wafalme 18:39

Na watu wote walipoona, wakaanguka kifudifudi; wakasema, Bwana ndiye Mungu, Bwana ndiye Mungu.

1 Wafalme 18:40

Eliya akawaambia, Wakamateni hao manabii wa Baali, asiokoke hata mmoja. Wakawakamata; na Eliya akawachukua mpaka kijito cha Kishoni, akawaua huko.

1 Wafalme 18:41

Naye Eliya akamwambia Ahabu, Haya! Inuka, ule, unywe; kwani pana sauti ya mvua tele.

1 Wafalme 18:42

Basi Ahabu akainuka ili ale na kunywa. Naye Eliya akapanda juu mpaka kilele cha Karmeli; akasujudu kifudifudi, akainama uso mpaka magotini.

1 Wafalme 18:43

Akamwambia mtumishi wake, Kwea sasa, utazame upande wa bahari. Akakwea, akatazama, na kusema, Hakuna kitu. Naye akanena, Enenda tena mara saba.

1 Wafalme 18:44

Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie.

1 Wafalme 18:45

Ikawa, muda si muda, mbingu zikawa nyeusi kwa mawingu na upepo, ikanyesha mvua nyingi. Ahabu akapanda garini, akaenda zake Yezreeli.

1 Wafalme 18:46

Mkono wa Bwana ulikuwa juu ya Eliya; akajikaza viuno, akapiga mbio mbele ya Ahabu mpaka kuiingia Yezreeli.