Matendo ya Mitume Mlango 19 Acts

Matendo ya Mitume 19:1

Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;

Matendo ya Mitume 19:2

akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.

Matendo ya Mitume 19:3

Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.

Matendo ya Mitume 19:4

Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.

Matendo ya Mitume 19:5

Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.

Matendo ya Mitume 19:6

Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.

Matendo ya Mitume 19:7

Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili.

Matendo ya Mitume 19:8

Akaingia ndani ya sinagogi, akanena kwa ushujaa kwa muda wa miezi mitatu, akihojiana na watu, na kuwavuta katika mambo ya ufalme wa Mungu.

Matendo ya Mitume 19:9

Lakini wengine walikaidi, wakakataa kuamini, wakiitukana ile Njia mbele ya mkutano; basi, akaondoka akawaacha, akawatenga wanafunzi, akahojiana na watu kila siku katika darasa ya mtu mmoja, jina lake Tirano.

Matendo ya Mitume 19:10

Mambo haya yakaendelea kwa muda wa miaka miwili, hata wote waliokaa Asia wakalisikia neno la Bwana, Wayahudi kwa Wayunani.

Matendo ya Mitume 19:11

Mungu akafanya kwa mikono ya Paulo miujiza ya kupita kawaida;

Matendo ya Mitume 19:12

hata wagonjwa wakaletewa leso na nguo zilizotoka mwilini mwake, magonjwa yao yakawaondokea, pepo wachafu wakawatoka.

Matendo ya Mitume 19:13

Baadhi ya Wayahudi wenye kutanga-tanga, nao ni wapunga pepo, wakajaribu kutaja jina la Bwana Yesu juu yao waliopagawa na pepo wachafu, wakisema, Nawaapisha kwa Yesu, yule anayehubiriwa na Paulo.

Matendo ya Mitume 19:14

Walikuwako wana saba wa mtu mmoja Skewa, Myahudi, kuhani mkuu, waliofanya hivyo.

Matendo ya Mitume 19:15

Yule pepo mchafu akawajibu, akawaambia, Yesu namjua na Paulo namfahamu, lakini ninyi ni nani?

Matendo ya Mitume 19:16

Na yule mtu aliyepagawa na pepo mchafu akawarukia wawili, akawaweza, akawashinda, hata wakatoka mbio katika nyumba ile hali wa uchi na kujeruhiwa.

Matendo ya Mitume 19:17

Habari hii ikajulikana na Wayahudi wote na Wayunani waliokaa Efeso, hofu ikawaingia wote, na jina la Bwana Yesu likatukuzwa.

Matendo ya Mitume 19:18

Na wengi wa wale walioamini wakaja wakaungama, wakidhihirisha matendo yao.

Matendo ya Mitume 19:19

Na watu wengi katika wale waliotumia mambo ya uganga wakakusanya vitabu vyao, wakavichoma moto mbele ya watu wote; wakafanya hesabu ya thamani yake, wakaona ya kwamba yapata fedha hamsini elfu.

Matendo ya Mitume 19:20

Hivyo ndivyo neno la Bwana lilivyozidi na kushinda kwa nguvu.

Matendo ya Mitume 19:21

Mambo hayo yalipokwisha kumalizika, Paulo akaazimu rohoni mwake, akiisha kupita katika Makedonia na Akaya, aende Yerusalemu, akisema, Baada ya kuwako huko, yanipasa kuuona na Rumi pia.

Matendo ya Mitume 19:22

Akatuma watu wawili miongoni mwa wale waliomtumikia kwenda Makedonia, nao ni Timotheo na Erasto, yeye mwenyewe akakaa katika Asia kitambo.

Matendo ya Mitume 19:23

Wakati huo kukatukia ghasia si haba katika habari ya Njia ile.

Matendo ya Mitume 19:24

Kwa maana mtu mmoja, jina lake Demetrio, mfua fedha, aliyekuwa akifanya vihekalu vya fedha vya Artemi, alikuwa akiwapatia mafundi faida nyingi.

Matendo ya Mitume 19:25

Akawakusanya hao, pamoja na wengine wenye kazi ile ile, akasema, Enyi wanaume, mnajua ya kuwa utajiri wetu hutoka katika kazi hii.

Matendo ya Mitume 19:26

Tena mnaona na kusikia ya kwamba si katika Efeso tu, bali katika Asia yote pia Paulo huyo ameshawishi watu wengi na kuwageuza nia zao, akisema ya kwamba hiyo inayofanywa kwa mikono siyo miungu.

Matendo ya Mitume 19:27

Si kwamba kazi hii yetu ina hatari ya kudharauliwa tu; bali na hekalu la mungu mke aliye mkuu, Artemi, kuhesabiwa si kitu, na kuondolewa utukufu wake, ambaye Asia yote pia na walimwengu wote humwabudu.

Matendo ya Mitume 19:28

Waliposikia haya wakajaa ghadhabu, wakapiga kelele, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.

Matendo ya Mitume 19:29

Mji wote ukajaa ghasia, wakaenda mbio wakaingia mahali pa michezo kwa nia moja, wakiisha kuwakamata Gayo na Aristarko, watu wa Makedonia waliosafiri pamoja na Paulo.

Matendo ya Mitume 19:30

Na Paulo alipotaka kuingia kati ya watu, wanafunzi hawakumwacha aingie.

Matendo ya Mitume 19:31

Na baadhi ya wakuu wa Asia, walio rafiki zake, wakatuma watu kwake, wakimsihi asijihudhurishe nafsi yake ndani ya mahali pa michezo.

Matendo ya Mitume 19:32

Basi wengine walikuwa wakilia hivi na wengine hivi; kwa maana ule mkutano ulikuwa umechafuka-chafuka, na wengi wao hawakuijua sababu ya kukusanyika kwao pamoja.

Matendo ya Mitume 19:33

Wakamtoa Iskanda katika mkutano, Wayahudi wakimweka mbele ya watu. Iskanda akawapungia mkono, akitaka kujitetea mbele ya wale watu.

Matendo ya Mitume 19:34

Lakini walipotambua ya kuwa yeye ni Myahudi, wakapiga kelele wote pia kwa sauti moja kwa muda wa kama saa mbili, wakisema, Artemi wa Waefeso ni mkuu.

Matendo ya Mitume 19:35

Na karani wa mji alipokwisha kuwatuliza watu, akasema, Enyi wanaume wa Efeso, ni mtu gani asiyejua ya kuwa mji wa Efeso ni mtunzaji wa hekalu la Artemi, aliye mkuu, na wa kitu kile kilichoanguka kutoka mbinguni?

Matendo ya Mitume 19:36

Basi kwa kuwa mambo haya hayawezi kukanushwa, imewapasa kutulia; msifanye neno la haraka haraka.

Matendo ya Mitume 19:37

Kwa maana mmewaleta watu hawa, wasioiba vitu vya hekalu wala kumtukana mungu mke wetu.

Matendo ya Mitume 19:38

Basi ikiwa Demetrio na mafundi walio pamoja naye wana neno juu ya mtu, baraza ziko, na maliwali wako; na washitakiane.

Matendo ya Mitume 19:39

Bali mkitafuta neno lo lote katika mambo mengine, yatatengenezwa katika kusanyiko lililo halali.

Matendo ya Mitume 19:40

Kwa maana tuna hatari ya kushitakiwa kwa ajili ya matata haya ya leo, ambayo hayana sababu; na katika neno hilo, hatutaweza kujiudhuru kwa mkutano huu.

Matendo ya Mitume 19:41

Alipokwisha kusema haya akauvunja mkutano.