Matendo ya Mitume Mlango 15 Acts

Matendo ya Mitume 15:1

Wakashuka watu waliotoka Uyahudi wakawafundisha wale ndugu ya kwamba, Msipotahiriwa kama desturi ya Musa hamwezi kuokoka.

Matendo ya Mitume 15:2

Basi baada ya Paulo na Barnaba kushindana na watu hawa na kuhojiana nao sana, ndugu wakaamuru kwamba Paulo na Barnaba na wengine miongoni mwao wapande kwenda Yerusalemu kwa mitume na wazee kwa habari ya swali hilo.

Matendo ya Mitume 15:3

Basi, wakisafirishwa na kanisa, wakapita kati ya nchi ya Foinike na Samaria, wakitangaza habari za kuongoka kwao Mataifa; wakawafurahisha ndugu sana.

Matendo ya Mitume 15:4

Walipofika Yerusalemu wakakaribishwa na kanisa na mitume na wazee, nao wakawaeleza mambo yote Mungu aliyoyafanya pamoja nao.

Matendo ya Mitume 15:5

Lakini baadhi ya madhehebu ya Mafarisayo walioamini wakasimama wakisema, Ni lazima kuwatahiri na kuwaagiza kuishika torati ya Musa.

Matendo ya Mitume 15:6

Mitume na wazee wakakusanyika wapate kulifikiri neno hilo.

Matendo ya Mitume 15:7

Na baada ya hoja nyingi Petro akasimama, akawaambia, Ndugu zangu, ninyi mnajua ya kuwa tangu siku za kwanza Mungu alichagua miongoni mwenu ya kwamba Mataifa walisikie neno la Injili kwa kinywa changu, na kuliamini.

Matendo ya Mitume 15:8

Na Mungu, ajuaye mioyo ya watu, akawashuhudia, akiwapa Roho Mtakatifu vile vile kama alivyotupa sisi;

Matendo ya Mitume 15:9

wala hakufanya tofauti kati yetu sisi na wao, akiwasafisha mioyo yao kwa imani.

Matendo ya Mitume 15:10

Basi sasa mbona mnamjaribu Mungu na kuweka kongwa juu ya shingo za wanafunzi, ambalo baba zetu wala sisi hatukuweza kulichukua.

Matendo ya Mitume 15:11

Bali twaamini kwamba tutaokoka kwa neema ya Bwana Yesu vile vile kama wao.

Matendo ya Mitume 15:12

Basi mkutano wote wakanyamaza, wakawasikiliza Barnaba na Paulo wakiwapasha habari za ishara na maajabu, ambayo Mungu aliyafanya kwa ujumbe wao katika Mataifa.

Matendo ya Mitume 15:13

Na hao walipokwisha kunyamaza Yakobo akajibu, akisema, Ndugu zangu, nisikilizeni.

Matendo ya Mitume 15:14

Simeoni ametueleza jinsi Mungu hapo kwanza alivyowaangalia Mataifa ili achague watu katika hao kwa ajili ya jina lake.

Matendo ya Mitume 15:15

Na maneno ya manabii yapatana na hayo, kama ilivyoandikwa,

Matendo ya Mitume 15:16

Baada ya mambo haya nitarejea, Nami nitaijenga tena nyumba ya Daudi iliyoanguka. Nitajenga tena maanguko yake, Nami nitaisimamisha;

Matendo ya Mitume 15:17

Ili wanadamu waliosalia wamtafute Bwana, Na mataifa yote ambao jina langu limetajwa kwao;

Matendo ya Mitume 15:18

Asema Bwana, ajulishaye hayo tangu milele.

Matendo ya Mitume 15:19

Kwa sababu hiyo mimi naamua hivi; Tusiwataabishe wale waliomgeukia Mungu katika Mataifa;

Matendo ya Mitume 15:20

bali tuwaandikie kwamba wajiepushe na unajisi wa sanamu, na uasherati, na nyama zilizosongolewa, na damu.

Matendo ya Mitume 15:21

Kwa maana tangu zamani za kale Musa anao watu wahubirio mambo yake; katika kila mji husomwa kila sabato katika masinagogi.

Matendo ya Mitume 15:22

Basi ikawapendeza mitume na wazee na kanisa lote kuwachagua watu miongoni mwao na kuwapeleka Antiokia pamoja na Paulo na Barnaba; nao ni hawa, Yuda aliyeitwa Barsaba, na Sila, waliokuwa watu wakuu katika ndugu. Wakaandika hivi na kupeleka kwa mikono yao,

Matendo ya Mitume 15:23

Mitume na ndugu wazee, kwa ndugu zetu walioko Antiokia na Shamu na Kilikia, walio wa Mataifa; Salamu.

Matendo ya Mitume 15:24

Kwa kuwa tumesikia ya kwamba watu waliotoka kwetu wamewasumbua kwa maneno yao, wakipotosha roho zenu, ambao sisi hatukuwaagiza;

Matendo ya Mitume 15:25

sisi tumeona vema, hali tumepatana kwa moyo mmoja, kuwachagua watu na kuwapeleka kwenu pamoja na wapendwa wetu Barnaba na Paulo,

Matendo ya Mitume 15:26

watu waliohatirisha maisha yao kwa ajili ya jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

Matendo ya Mitume 15:27

Basi tumewatuma Yuda na Sila, watakaowaambia wenyewe maneno yayo hayo kwa vinywa vyao.

Matendo ya Mitume 15:28

Kwa maana ilimpendeza Roho Mtakatifu na sisi, tusiwatwike mzigo ila hayo yaliyo lazima,

Matendo ya Mitume 15:29

yaani, mjiepushe na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na nyama zilizosongolewa, na uasherati. Mkijizuia na hayo, mtafanya vema. Wasalamu.

Matendo ya Mitume 15:30

Hata hao wakiisha kupewa ruhusa wakatelemkia Antiokia; na baada ya kuwakusanya jamii yote wakawapa ile barua.

Matendo ya Mitume 15:31

Nao walipokwisha kuisoma wakafurahi kwa ajili ya faraja ile.

Matendo ya Mitume 15:32

Tena Yuda na Sila, kwa kuwa wao wenyewe ni manabii, wakawausia ndugu kwa maneno mengi, wakawathibitisha.

Matendo ya Mitume 15:33

Na wakiisha kukaa huko muda, wakaruhusiwa na ndugu waende kwa amani kwa hao waliowatuma. [

Matendo ya Mitume 15:34

Lakini Sila akaona vema kukaa huko.]

Matendo ya Mitume 15:35

Na Paulo na Barnaba wakakaa huko Antiokia, wakifundisha na kulihubiri neno la Bwana, pamoja na watu wengine wengi.

Matendo ya Mitume 15:36

Baada ya siku kadha wa kadha Paulo akamwambia Barnaba, Haya! Mrejee sasa tukawaangalie hao ndugu katika kila mji tulipolihubiri neno la Bwana, wa hali gani.

Matendo ya Mitume 15:37

Barnaba akaazimu kumchukua Yohana aliyeitwa Marko pamoja nao.

Matendo ya Mitume 15:38

Bali Paulo hakuona vema kumchukua huyo aliyewaacha huko Pamfilia, asiende nao kazini.

Matendo ya Mitume 15:39

Basi palitokea mashindano baina yao hata wakatengana. Barnaba akamchukua Marko akatweka kwenda Kipro.

Matendo ya Mitume 15:40

Lakini Paulo akamchagua Sila, akaondoka, akiombewa na wale ndugu apewe neema ya Bwana.

Matendo ya Mitume 15:41

Akapita katika Shamu na Kilikia akiyathibitisha makanisa.