Matendo ya Mitume Mlango 24 Acts

Matendo ya Mitume 24:1

Baada ya siku tano, Anania, Kuhani Mkuu, akatelemka na baadhi ya wazee pamoja naye, na msemi mmoja, Tertulo, nao wakamweleza liwali habari za Paulo.

Matendo ya Mitume 24:2

Naye alipoitwa, Tertulo akaanza kumshitaki, akisema, Kwa kuwa mnapata amani nyingi chini yako, Feliki mtukufu, na kwa maangalizi yako mambo mabaya yanatengenezwa kwa ajili ya taifa hili,

Matendo ya Mitume 24:3

basi tunayapokea kila wakati na kila mahali, kwa shukrani yote.

Matendo ya Mitume 24:4

Lakini nisikuudhi zaidi, nakusihi utusikilize maneno machache kwa fadhili zako.

Matendo ya Mitume 24:5

Kwa maana tumemwona mtu huyu mkorofi, mwanzilishi wa fitina katika Wayahudi wote duniani, tena ni kichwa cha madhehebu ya Wanazorayo.

Matendo ya Mitume 24:6

Na tena alijaribu kulitia hekalu unajisi; tukamkamata; [tukataka kumhukumu kwa sheria yetu.

Matendo ya Mitume 24:7

Lakini Lisia jemadari akafika akamwondoa mikononi mwetu kwa nguvu,

Matendo ya Mitume 24:8

Akawaamuru wale waliomshitaki waje kwako.] Wewe mwenyewe kwa kumwuliza-uliza utaweza kupata habari ya mambo yale yote tunayomshitaki sisi.

Matendo ya Mitume 24:9

Wayahudi nao wakamshitaki, wakisema ya kuwa ndivyo yalivyo.

Matendo ya Mitume 24:10

Na liwali alipompungia mkono ili anene, Paulo akajibu, Kwa kuwa ninajua ya kwamba wewe umekuwa mwamuzi wa taifa hili kwa muda wa miaka mingi, najitetea mwenyewe kwa moyo wa furaha.

Matendo ya Mitume 24:11

Maana waweza kujua ya kuwa hazijapita siku zaidi ya kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu ili kuabudu.

Matendo ya Mitume 24:12

Watu hawa hawakuniona ndani ya hekalu, nikihojiana na mtu, au kufanya fujo katika mkutano, wala katika masinagogi wala ndani ya mji.

Matendo ya Mitume 24:13

Wala hawawezi kuyahakikisha mambo haya wanayonishitaki sasa.

Matendo ya Mitume 24:14

Ila neno hili naungama kwako ya kwamba kwa Njia ile ambayo waiita uzushi, ndivyo ninavyomwabudu Mungu wa baba zetu, nikiyaamini yote yanayopatana na torati na yaliyoandikwa katika vyuo vya manabii.

Matendo ya Mitume 24:15

Nina tumaini kwa Mungu, ambalo hata hao nao wanalitazamia, ya kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, wenye haki na wasio haki pia.

Matendo ya Mitume 24:16

Nami ninajizoeza katika neno hili niwe na dhamiri isiyo na hatia mbele za Mungu na mbele ya watu siku zote.

Matendo ya Mitume 24:17

Baada ya miaka mingi nalifika niwaletee watu wa taifa langu sadaka na matoleo.

Matendo ya Mitume 24:18

Wakaniona ndani ya hekalu nikishughulika na mambo haya, hali nimetakaswa, wala sikuwa na mkutano wala ghasia; lakini walikuwako baadhi ya Wayahudi waliotoka Asia,

Matendo ya Mitume 24:19

ambao imewapasa hao kuwapo hapa mbele yako na kunishitaki, kama wana neno lo lote juu yangu.

Matendo ya Mitume 24:20

Au watu hawa wenyewe na waseme, ni kosa gani waliloliona kwangu niliposimama mbele ya baraza,

Matendo ya Mitume 24:21

isipokuwa kwa ajili ya sauti hii moja, nilipolia nikisimama katikati yao, na kusema, Kwa ajili ya ufufuo wa wafu ninahukumiwa mbele yenu hivi leo.

Matendo ya Mitume 24:22

Basi Feliki aliwaahirisha, kwa sababu alijua habari za Njia ile kwa usahihi zaidi, akasema, Lisia jemadari atakapotelemka nitakata maneno yenu.

Matendo ya Mitume 24:23

Akamwamuru yule akida kwamba Paulo alindwe; ila awe na nafasi, wala asimkataze mmojawapo wa rafiki zake kumtumikia.

Matendo ya Mitume 24:24

Baada ya siku kadha wa kadha, Feliki akafika pamoja na Drusila mkewe aliyekuwa Myahudi, akatuma kumwita Paulo akamsikiliza habari za imani iliyo kwa Kristo Yesu.

Matendo ya Mitume 24:25

Na Paulo alipokuwa akitoa hoja zake katika habari ya haki, na kuwa na kiasi, na hukumu itakayokuja, Feliki akafanya hofu akajibu, Sasa enenda zako, nami nikipata nafasi nitakuita.

Matendo ya Mitume 24:26

Pamoja na hayo alitaraji kwamba atapewa fedha na Paulo; kwa hiyo alimwita mara nyingi akaongea naye.

Matendo ya Mitume 24:27

Na miaka miwili ilipotimia, Feliki akampokea Porkio Festo atawale badala yake. Na Feliki, akitaka kuwafanyia Wayahudi fadhili, akamwacha Paulo amefungwa.