Matendo ya Mitume Mlango 23 Acts

Matendo ya Mitume 23:1

Paulo akawakazia macho watu wa baraza, akasema, Ndugu zangu, mimi kwa dhamiri safi kabisa nimeishi mbele za Mungu hata leo hivi.

Matendo ya Mitume 23:2

Kuhani Mkuu Anania akawaamuru wale waliosimama karibu naye wampige kinywa chake.

Matendo ya Mitume 23:3

Ndipo Paulo akamwambia, Mungu atakupiga wewe, ukuta uliopakwa chokaa. Wewe umeketi kunihukumu sawasawa na sheria, nawe unaamuru nipigwe kinyume cha sheria?

Matendo ya Mitume 23:4

Wale waliosimama karibu wakasema, Je! Unamtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?

Matendo ya Mitume 23:5

Paulo akasema, Sikujua, ndugu zangu, ya kuwa yeye ni Kuhani Mkuu; maana imeandikwa, Usimnenee mabaya mkuu wa watu wako.

Matendo ya Mitume 23:6

Paulo alipotambua ya kuwa sehemu moja ni Masadukayo, na sehemu ya pili ni Mafarisayo, akapaza sauti yake katika ile baraza, Ndugu zangu, mimi ni Farisayo mwana wa Farisayo; mimi ninahukumiwa kwa ajili ya tumaini la ufufuo wa wafu.

Matendo ya Mitume 23:7

Alipokwisha kunena hayo palikuwa na mashindano baina ya Mafarisayo na Masadukayo, mkutano ukafarakana.

Matendo ya Mitume 23:8

Kwa maana Masadukayo husema ya kwamba hakuna kiyama wala malaika wala roho; bali Mafarisayo hukiri yote.

Matendo ya Mitume 23:9

Pakawa na makelele mengi. Waandishi wengine wa upande wa Mafarisayo wakasimama, wakateta, wakisema, Hatuoni uovu wo wote katika mtu huyu; bali ikiwa roho au malaika amesema naye, ni nini?

Matendo ya Mitume 23:10

Ugomvi mkubwa ulipotokea, yule jemadari akachelea Paulo asije akararuliwa nao, akaamuru askari washuke na kumwondoa kwa nguvu mikononi mwao, na kumleta ndani ya ngome.

Matendo ya Mitume 23:11

Usiku ule Bwana akasimama karibu naye, akasema, Uwe na moyo mkuu; kwa sababu, kama ulivyonishuhudia habari zangu Yerusalemu, imekupasa kunishuhudia vivyo hivyo Rumi nako.

Matendo ya Mitume 23:12

Kulipopambauka, Wayahudi wakafanya mapatano, wakajifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala hawatakunywa hata wamwue Paulo.

Matendo ya Mitume 23:13

Na hao walioapiana hivyo walipata zaidi ya watu arobaini.

Matendo ya Mitume 23:14

Nao wakaenda kwa wakuu wa makuhani na wazee, wakasema, Tumejifunga kwa kiapo tusionje kitu hata tumwue Paulo.

Matendo ya Mitume 23:15

Basi sasa ninyi pamoja na wazee wa baraza mwambieni jemadari amlete chini kwenu, kana kwamba mnataka kujua habari zake vizuri zaidi; na sisi tu tayari kumwua kabla hajakaribia.

Matendo ya Mitume 23:16

Mjomba wake Paulo akasikia habari za kuotea kwao, akaenda akaingia ndani ya ngome akampasha Paulo habari.

Matendo ya Mitume 23:17

Paulo akamwita akida mmoja, akasema, Mchukue kijana huyu kwa jemadari; maana ana neno la kumwarifu.

Matendo ya Mitume 23:18

Basi akamchukua, akampeleka kwa jemadari, akamwambia, Paulo, yule mfungwa, aliniita akataka nikuletee kijana huyu kwa kuwa ana neno la kukuambia.

Matendo ya Mitume 23:19

Yule jemadari akamshika mkono akajitenga pamoja naye kando, akamwuliza kwa faragha, Una neno gani utakalo kuniarifu?

Matendo ya Mitume 23:20

Akasema Wayahudi wamepatana kukuomba umlete Paulo chini kesho, ukamweke mbele ya baraza, kana kwamba wanataka kupata habari zake kwa usahihi zaidi.

Matendo ya Mitume 23:21

Basi wewe usikubali; kwa maana watu zaidi ya arobaini wanamwotea, wamejifunga kwa kiapo wasile wala wasinywe hata watakapomwua; nao sasa wako tayari, wakiitazamia ahadi kwako.

Matendo ya Mitume 23:22

Basi yule jemadari akamwacha kijana aende zake, akimwagiza, Usimwambie mtu awaye yote ya kwamba umeniarifu haya.

Matendo ya Mitume 23:23

Akawaita maakida wawili, akasema, Wekeni tayari askari mia mbili kwenda Kaisaria, na askari wapanda farasi sabini, na wenye mikuki mia mbili, kwa saa tatu ya usiku.

Matendo ya Mitume 23:24

Akawaambia kuweka wanyama tayari wampandishe Paulo, na kumchukua salama kwa Feliki liwali.

Matendo ya Mitume 23:25

Akaandika barua, kwa namna hii,

Matendo ya Mitume 23:26

Klaudio Lisia kwa liwali mtukufu Feliki, Salamu!

Matendo ya Mitume 23:27

Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi, wakawa karibu kumwua, ndipo nikaenda pamoja na kikosi cha askari nikamwokoa, nilipopata habari ya kuwa yeye ni Mrumi.

Matendo ya Mitume 23:28

Nami nikitaka kulijua lile neno walilomshitakia, nikamtelemsha nikamweka mbele ya baraza;

Matendo ya Mitume 23:29

nikaona kwamba ameshitakiwa kwa ajili ya maswali ya sheria yao, wala hakushitakiwa neno lo lote la kustahili kuuawa wala kufungwa.

Matendo ya Mitume 23:30

Hata nilipopewa habari kwamba patakuwa na vitimvi juu ya mtu huyu, mara nikampeleka kwako, nikawaagiza na wale waliomshitaki, wanene habari zake mbele yako. Wasalamu.

Matendo ya Mitume 23:31

Basi, wale askari wakamchukua Paulo kama walivyoamriwa, wakampeleka hata Antipatri usiku;

Matendo ya Mitume 23:32

hata asubuhi wakawaacha wale wapanda farasi waende pamoja naye, nao wakarudi zao ngomeni.

Matendo ya Mitume 23:33

Na wale walipofika Kaisaria, na kumpa liwali ile barua, wakamweka Paulo mbele yake.

Matendo ya Mitume 23:34

Naye alipokwisha kuisoma, akawauliza, Mtu huyu ni wa jimbo gani? Alipoarifiwa ya kuwa ni mtu wa Kilikia,

Matendo ya Mitume 23:35

akasema, Nitakusikia wewe watakapokuja wale waliokushitaki; akaamuru alindwe katika nyumba ya uliwali ya Herode.