Matendo ya Mitume Mlango 10 Acts

Matendo ya Mitume 10:1

Palikuwa na mtu Kaisaria, jina lake Kornelio, akida wa kikosi kilichoitwa Kiitalia,

Matendo ya Mitume 10:2

mtu mtauwa, mchaji wa Mungu, yeye na nyumba yake yote, naye alikuwa akiwapa watu sadaka nyingi, na kumwomba Mungu daima.

Matendo ya Mitume 10:3

Akaona katika maono waziwazi, kama saa tisa ya mchana, malaika wa Mungu, akimjia na kumwambia, Kornelio!

Matendo ya Mitume 10:4

Akamtazama sana, akaogopa akasema, Kuna nini, Bwana? Akamwambia, Sala zako na sadaka zako zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.

Matendo ya Mitume 10:5

Sasa basi, peleka watu Yafa, ukamwite Simoni, aitwaye Petro.

Matendo ya Mitume 10:6

Yeye ni mgeni wa mtu mmoja, jina lake Simoni, mtengenezaji wa ngozi, ambaye nyumba yake iko pwani, atakuambia yakupasayo kutenda.

Matendo ya Mitume 10:7

Na yule malaika aliyesema naye akiisha kuondoka, Kornelio akawaita wawili katika watumishi wake wa nyumbani, na askari mmoja, mtu mtauwa katika wale waliomhudumia daima;

Matendo ya Mitume 10:8

na alipokwisha kuwaeleza mambo yote akawatuma kwenda Yafa.

Matendo ya Mitume 10:9

Hata siku ya pili, walipokuwa wakisafiri na kuukaribia mji, Petro alipanda juu darini, kwenda kuomba, yapata saa sita ya mchana;

Matendo ya Mitume 10:10

akaumwa na njaa sana, akataka kula; lakini walipokuwa wakiandaa, roho yake ikazimia,

Matendo ya Mitume 10:11

akaona mbingu zimefunuka, na chombo kikishuka kama nguo kubwa, inatelemshwa kwa pembe zake nne hata nchi;

Matendo ya Mitume 10:12

ambayo ndani yake walikuwamo aina zote za wanyama wenye miguu minne, na hao watambaao, na ndege wa angani.

Matendo ya Mitume 10:13

Kisha sauti ikamjia, kusema, Ondoka, Petro, uchinje ule.

Matendo ya Mitume 10:14

Lakini Petro akasema, Hasha, Bwana, kwa maana sijakula kamwe kitu kilicho kichafu au najisi.

Matendo ya Mitume 10:15

Sauti ikamjia mara ya pili, ikimwambia, Vilivyotakaswa na Mungu, usiviite wewe najisi.

Matendo ya Mitume 10:16

Jambo hili likatendeka mara tatu; kisha kile chombo kikapokewa tena mbinguni.

Matendo ya Mitume 10:17

Hata Petro alipokuwa akiona shaka ndani ya nafsi yake, maana yake ni nini maono hayo aliyoyaona, wale watu waliotumwa na Kornelio, wakiisha kuiulizia nyumba ya Simoni, wakasimama mbele ya mlango,

Matendo ya Mitume 10:18

wakaita; wakauliza kwamba Simoni aitwaye Petro anakaa humo.

Matendo ya Mitume 10:19

Na Petro alikuwa akiyafikiri yale maono. Roho akamwambia, Wako watu watatu wanakutafuta.

Matendo ya Mitume 10:20

Basi ondoka ushuke ufuatane nao, usione tashwishi, kwa maana ni mimi niliyewatuma.

Matendo ya Mitume 10:21

Petro akawashukia wale watu, akanena, Mimi ndiye mnayemtafuta. Mmekuja kwa sababu gani?

Matendo ya Mitume 10:22

Wakasema, Kornelio akida, mtu mwenye haki, mchaji wa Mungu, aliye na sifa njema kwa taifa lote la Wayahudi, alionywa na malaika mtakatifu kutuma watu kwako, uende nyumbani kwake, apate kusikiliza maneno kwako.

Matendo ya Mitume 10:23

Akawakaribisha wawe wageni wake. Hata siku ya pili, Petro akaondoka akatoka pamoja nao, na baadhi ya ndugu waliokaa Yafa wakafuatana naye.

Matendo ya Mitume 10:24

Siku ya pili yake wakaingia Kaisaria. Na Kornelio alikuwa akiwangojea, hali amekusanya jamaa zake na rafiki zake.

Matendo ya Mitume 10:25

Petro alipokuwa akiingia Kornelio akatoka amlaki akamwangukia miguu, akamsujudia.

Matendo ya Mitume 10:26

Lakini Petro akamwinua, akasema, Simama, mimi nami ni mwanadamu.

Matendo ya Mitume 10:27

Na katika kusema naye akaingia ndani, akaona watu wengi wamekusanyika.

Matendo ya Mitume 10:28

Akawaambia, Ninyi mnajua ya kuwa si halali mtu aliye Myahudi ashikamane na mtu aliye wa taifa lingine wala kumwendea, lakini Mungu amenionya, nisimwite mtu awaye yote mchafu wala najisi.

Matendo ya Mitume 10:29

Kwa sababu hiyo nalikuja nilipoitwa, nisikatae; basi nawauliza, ni neno gani mliloniitia?

Matendo ya Mitume 10:30

Kornelio akasema, Siku tatu zilizopita, katika saa ii hii, yaani saa tisa, nilikuwa nikisali nyumbani mwangu; nikamwona mtu amesimama mbele yangu, mwenye nguo zing'arazo,

Matendo ya Mitume 10:31

akasema, Kornelio, kuomba kwako kumesikiwa, na sadaka zako zinakumbukwa mbele za Mungu.

Matendo ya Mitume 10:32

Basi, tuma watu kwenda Yafa, ukamwite Simoni aitwaye Petro, anakaa katika nyumba ya Simoni, mtengenezaji wa ngozi, karibu na pwani; naye akija atasema nawe.

Matendo ya Mitume 10:33

Mara nikatuma watu kwako, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tupo hapa mbele za Mungu, tupate kuyasikiliza maneno yote uliyoamriwa na Bwana.

Matendo ya Mitume 10:34

Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Hakika natambua ya kuwa Mungu hana upendeleo;

Matendo ya Mitume 10:35

bali katika kila taifa mtu amchaye na kutenda haki hukubaliwa na yeye.

Matendo ya Mitume 10:36

Neno lile alilowapelekea wana wa Israeli akihubiri habari njema ya amani kwa Yesu Kristo (ndiye Bwana wa wote),

Matendo ya Mitume 10:37

jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya ubatizo aliouhubiri Yohana;

Matendo ya Mitume 10:38

habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye.

Matendo ya Mitume 10:39

Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini.

Matendo ya Mitume 10:40

Huyo Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika,

Matendo ya Mitume 10:41

si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu.

Matendo ya Mitume 10:42

Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa walio hai na wafu.

Matendo ya Mitume 10:43

Huyo manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

Matendo ya Mitume 10:44

Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno.

Matendo ya Mitume 10:45

Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 10:46

Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

Matendo ya Mitume 10:47

Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

Matendo ya Mitume 10:48

Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha.