Matendo ya Mitume Mlango 12 Acts

Matendo ya Mitume 12:1

Panapo majira yale yale Herode mfalme akanyosha mikono yake kuwatenda mabaya baadhi ya watu wa kanisa.

Matendo ya Mitume 12:2

Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana, kwa upanga.

Matendo ya Mitume 12:3

Na akiona ya kuwa imewapendeza Wayahudi akaendelea akamshika na Petro. Siku hizo zilikuwa siku za mikate isiyochachwa.

Matendo ya Mitume 12:4

Alipokwisha kumkamata, akamweka gerezani akamtia mikononi mwa vikosi vinne vya askari wanne wanne, wamlinde, akitaka baada ya Pasaka kumtoa na kumweka mbele ya watu.

Matendo ya Mitume 12:5

Basi Petro akalindwa gerezani, nalo kanisa likamwomba Mungu kwa juhudi kwa ajili yake.

Matendo ya Mitume 12:6

Hata wakati Herode alipotaka kumtoa, usiku ule ule Petro alikuwa analala katikati ya askari wawili, amefungwa minyororo miwili; walinzi mbele ya mlango wakailinda gereza.

Matendo ya Mitume 12:7

Mara malaika wa Bwana akasimama karibu naye, nuru ikamulika mle chumbani, akampiga Petro ubavuni, akamwamsha, akisema, Ondoka upesi. Minyororo yake ikamwanguka mikononi.

Matendo ya Mitume 12:8

Malaika akamwambia, Jifunge, kavae viatu vyako. Akafanya hivyo. Kisha akamwambia, Jivike nguo yako, ukanifuate.

Matendo ya Mitume 12:9

Akatoka nje, akamfuata; wala hakujua ya kuwa ni kweli yaliyofanywa na malaika; bali alidhani kwamba anaona maono.

Matendo ya Mitume 12:10

Na walipopita lindo la kwanza na la pili, wakaja hata mlango wa chuma wa kuingilia mjini, ukawafungukia wenyewe. Wakatoka nje, wakapita katika njia moja; mara malaika akamwacha.

Matendo ya Mitume 12:11

Hata Petro alipopata fahamu akasema, Sasa nimejua yakini ya kuwa Bwana amempeleka malaika wake na kunitoa katika mkono wa Herode na katika kutazamia kote kwa taifa la Wayahudi.

Matendo ya Mitume 12:12

Na alipokuwa akifikiri haya akafika nyumbani kwa Mariamu, mamaye Yohana, ambaye jina lake la pili ni Marko; na watu wengi walikuwa wamekutana humo wakiomba.

Matendo ya Mitume 12:13

Naye alipobisha kilango cha lango, kijakazi, jina lake Roda, akaja kusikiliza.

Matendo ya Mitume 12:14

Alipoitambua sauti ya Petro, hakukifungua lango, kwa ajili ya furaha, bali alipiga mbio, akaingia ndani akawaambia kwamba Petro anasimama mbele ya lango.

Matendo ya Mitume 12:15

Wakamwambia, Una wazimu. Lakini yeye akakaza sana, akasema ya kwamba ndivyo hivyo. Wakanena, Ni malaika wake.

Matendo ya Mitume 12:16

Petro akafuliza kugonga, hata walipokwisha kumfungulia wakamwona, wakastaajabu.

Matendo ya Mitume 12:17

Naye akawapungia mkono wanyamaze, akawaeleza jinsi Bwana alivyomtoa katika gereza. Akasema, Kampasheni Yakobo na wale ndugu habari hizi. Akaondoka, akaenda mahali pengine.

Matendo ya Mitume 12:18

Hata kulipopambauka askari wakaingiwa na fadhaa nyingi, amekuwaje Petro.

Matendo ya Mitume 12:19

Na Herode alipomtafuta, asimwone, aliwauliza-uliza wale walinzi, akaamuru wauawe. Kisha akatelemkia kutoka Uyahudi kwenda Kaisaria, akakaa huko.

Matendo ya Mitume 12:20

Naye Herode alikuwa amewakasirikia sana watu wa Tiro na Sidoni; wakamwendea kwa nia moja, na wakiisha kufanya urafiki na Blasto, mwenye kukitunza chumba cha mfalme cha kulalia, wakataka amani; kwa maana nchi yao ilipata riziki kwa nchi ya mfalme.

Matendo ya Mitume 12:21

Basi siku moja iliyoazimiwa, Herode akajivika mavazi ya kifalme, akaketi katika kiti cha enzi, akatoa hotuba mbele yao.

Matendo ya Mitume 12:22

Watu wakapiga kelele, wakisema, Ni sauti ya Mungu, si sauti ya mwanadamu.

Matendo ya Mitume 12:23

Mara malaika wa Bwana akampiga, kwa sababu hakumpa Mungu utukufu; akaliwa na chango, akatokwa na roho.

Matendo ya Mitume 12:24

Neno la Bwana likazidi na kuenea.

Matendo ya Mitume 12:25

Na Barnaba na Sauli, walipokwisha kutimiza huduma yao, wakarejea kutoka Yerusalemu, wakamchukua pamoja nao Yohana aitwaye Marko.