Matendo ya Mitume Mlango 14 Acts

Matendo ya Mitume 14:1

Ikawa huko Ikonio wakaingia pamoja katika sinagogi la Wayahudi; na kwa vile walivyonena, kundi kubwa la Wayahudi na la Wayunani wakaamini.

Matendo ya Mitume 14:2

Walakini Wayahudi wasioamini wakawataharakisha watu wa Mataifa na kuwatia nia mbaya juu ya ndugu.

Matendo ya Mitume 14:3

Basi wakakaa huko wakati mwingi, wakinena kwa ushujaa katika Bwana, aliyelishuhudia neno la neema yake, akiwajalia ishara na maajabu yatendeke kwa mikono yao.

Matendo ya Mitume 14:4

Lakini jamii ya watu wa mjini wakafarakana; hawa walikuwa upande wa Wayahudi, na hawa upande wa Mitume.

Matendo ya Mitume 14:5

Hata palipotokea shambulio la watu wa Mataifa na Wayahudi pamoja na wakubwa wao juu yao, kuwatenda jeuri na kuwapiga kwa mawe,

Matendo ya Mitume 14:6

wao wakapata habari wakakimbilia Listra na Derbe, miji ya Likaonia, na nchi zilizo kando kando;

Matendo ya Mitume 14:7

wakakaa huko, wakiihubiri Injili.

Matendo ya Mitume 14:8

Na huko Listra palikuwa na mtu mmoja, dhaifu wa miguu, kiwete tangu tumboni mwa mamaye, ambaye hajaenda kabisa.

Matendo ya Mitume 14:9

Mtu huyo alimsikia Paulo alipokuwa akinena; ambaye akamkazia macho na kuona ya kuwa ana imani ya kuponywa,

Matendo ya Mitume 14:10

akasema kwa sauti kuu, Simama kwa miguu yako sawasawa. Akasimama upesi akaenda.

Matendo ya Mitume 14:11

Na makutano walipoona aliyoyafanya Paulo wakapaza sauti zao, wakisema kwa Kilikaonia, Miungu wametushukia kwa mifano ya wanadamu.

Matendo ya Mitume 14:12

Wakamwita Barnaba, Zeu, na Paulo, Herme, kwa sababu ndiye aliyekuwa mnenaji.

Matendo ya Mitume 14:13

Kuhani wa Zeu ambaye hekalu lake lilikuwa mbele ya mji, akaleta ng'ombe na taji za maua hata malangoni, akitaka kutoa dhabihu pamoja na makutano.

Matendo ya Mitume 14:14

Walakini mitume Barnaba na Paulo, walipopata habari, wakararua nguo zao, wakaenda mbio wakaingia katika makutano, wakipiga kelele,

Matendo ya Mitume 14:15

wakisema, Akina bwana, mbona mnafanya haya? Sisi nasi tu wanadamu hali moja na ninyi; twawahubiri habari njema, ili mgeuke na kuyaacha mambo haya ya ubatili na kumwelekea Mungu aliye hai, aliyeumba mbingu na nchi na bahari na vitu vyote vilivyomo;

Matendo ya Mitume 14:16

ambaye zamani zilizopita aliwaacha mataifa yote waende katika njia zao wenyewe.

Matendo ya Mitume 14:17

Lakini hakujiacha pasipo ushuhuda, kwa kuwa alitenda mema, akiwapeni mvua kutoka mbinguni, na nyakati za mavuno, akiwashibisha mioyo yenu chakula na furaha.

Matendo ya Mitume 14:18

Na kwa maneno hayo wakawazuia makutano kwa shida, wasiwatolee dhabihu.

Matendo ya Mitume 14:19

Lakini Wayahudi wakafika toka Antiokia na Ikonio, wakawashawishi makutano hata wakampiga kwa mawe Paulo, wakamburuta nje ya mji, wakidhania ya kuwa amekwisha kufa.

Matendo ya Mitume 14:20

Lakini wanafunzi walipokuwa wakimzunguka pande zote, akasimama, akaingia ndani ya mji; na siku ya pili yake akatoka, akaenda zake pamoja na Barnaba mpaka Derbe.

Matendo ya Mitume 14:21

Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra na Ikonio na Antiokia,

Matendo ya Mitume 14:22

wakifanya imara roho za wanafunzi na kuwaonya wakae katika ile Imani, na ya kwamba imetupasa kuingia katika ufalme wa Mungu kwa njia ya dhiki nyingi.

Matendo ya Mitume 14:23

Na walipokwisha kuwachagulia wazee katika kila kanisa, na kuomba pamoja na kufunga, wakawaweka katika mikono ya Bwana waliyemwamini.

Matendo ya Mitume 14:24

Wakapita kati ya Pisidia wakaingia Pamfilia.

Matendo ya Mitume 14:25

Na baada ya kuhubiri lile neno katika Perge wakatelemka mpaka Atalia.

Matendo ya Mitume 14:26

Na kutoka huko wakaabiri kwenda Antiokia. Huko ndiko walikoombewa neema ya Mungu kwa ile kazi waliyokwisha kuitimiza.

Matendo ya Mitume 14:27

Hata walipofika wakalikutanisha kanisa, wakawaeleza mambo yote aliyoyafanya Mungu pamoja nao, na ya kwamba amewafungulia Mataifa mlango wa imani.

Matendo ya Mitume 14:28

Wakaketi huko wakati usiokuwa mchache, pamoja na wanafunzi.