Matendo ya Mitume Mlango 18 Acts

Matendo ya Mitume 18:1

Baada ya mambo hayo, Paulo akatoka Athene akafika Korintho.

Matendo ya Mitume 18:2

Akamwona Myahudi mmoja, jina lake Akila, mzalia wa Ponto; naye amekuja kutoka nchi ya Italia siku za karibu, pamoja na Prisila mkewe, kwa sababu Klaudio amewaamuru Wayahudi wote watoke Rumi, naye akafikilia kwao;

Matendo ya Mitume 18:3

na kwa kuwa kazi yao ya ufundi ilikuwa moja, akakaa kwao, wakafanya kazi pamoja, kwa maana walikuwa mafundi wa kushona hema.

Matendo ya Mitume 18:4

Akatoa hoja zake katika sinagogi kila sabato, akajaribu kuwavuta Wayahudi na Wayunani.

Matendo ya Mitume 18:5

Hata Sila na Timotheo walipotelemka kutoka Makedonia, Paulo akasongwa sana na lile neno, akiwashuhudia Wayahudi ya kwamba Yesu ni Kristo.

Matendo ya Mitume 18:6

Walipopingamana naye na kumtukana Mungu, akakung'uta mavazi yake, akawaambia, Damu yenu na iwe juu ya vichwa vyenu; mimi ni safi; tangu sasa nitakwenda kwa watu wa Mataifa.

Matendo ya Mitume 18:7

Akaondoka huko akaingia katika nyumba ya mtu mmoja jina lake Tito Yusto, mcha Mungu, ambaye nyumba yake ilikuwa mpaka mmoja na sinagogi.

Matendo ya Mitume 18:8

Na Krispo, mkuu wa sinagogi, akamwamini Bwana pamoja na nyumba yake yote. Wakorintho wengi waliposikia, waliamini, wakabatizwa.

Matendo ya Mitume 18:9

Bwana akamwambia Paulo kwa maono usiku, Usiogope, bali nena, wala usinyamaze,

Matendo ya Mitume 18:10

kwa kuwa mimi ni pamoja nawe, wala hapana mtu atakayekushambulia ili kukudhuru; kwa maana mimi nina watu wengi katika mji huu.

Matendo ya Mitume 18:11

Akakaa huko muda wa mwaka mmoja na miezi sita akifundisha kati yao neno la Mungu.

Matendo ya Mitume 18:12

Hata Galio alipokuwa liwali wa Akaya, Wayahudi wakamwinukia Paulo kwa nia moja, wakamleta mbele ya kiti cha hukumu,

Matendo ya Mitume 18:13

wakisema Mtu huyu huwavuta watu ili wamwabudu Mungu kinyume cha sheria.

Matendo ya Mitume 18:14

Na Paulo alipotaka kufunua kinywa chake, Galio akawaambia Wayahudi, Kama lingekuwa jambo la dhuluma au la hila mbaya, enyi Wayahudi, ingekuwa haki mimi kuchukuliana nanyi;

Matendo ya Mitume 18:15

bali ikiwa ni hoja juu ya maneno na majina na sheria yenu, liangalieni ninyi wenyewe, maana mimi sitaki kuwa mwamuzi wa mambo hayo.

Matendo ya Mitume 18:16

Akawafukuza waondoke mbele ya kiti cha hukumu.

Matendo ya Mitume 18:17

Nao wote wakamshika Sosthene, mkuu wa sinagogi, wakampiga mbele ya kiti cha hukumu. Wala Galio hakuyaona mambo hayo kuwa ni kitu.

Matendo ya Mitume 18:18

Baada ya hayo Paulo akazidi kukaa huko siku nyingi, kisha akaagana na ndugu akaabiri kwenda Shamu; na Prisila na Akila wakaenda pamoja naye, alipokwisha kunyoa kichwa chake huko Kenkrea; maana alikuwa ana nadhiri.

Matendo ya Mitume 18:19

Wakafika Efeso, akawaacha huko. Yeye mwenyewe akaingia katika sinagogi, akahojiana na Wayahudi.

Matendo ya Mitume 18:20

Walipomtaka akae wakati mwingi zaidi, hakukubali;

Matendo ya Mitume 18:21

bali aliagana nao, akisema, Nitarejea kwenu tena, Mungu akinijalia. Akatweka, akatoka Efeso,

Matendo ya Mitume 18:22

na alipokwisha kushuka Kaisaria, akapanda juu, akawasalimu kanisa, kisha akatelemkia Antiokia.

Matendo ya Mitume 18:23

Hata akiisha kukaa huko siku kadha wa kadha akaondoka, akapita kati ya nchi ya Galatia na Frigia, mji kwa mji, akiwathibitisha wanafunzi.

Matendo ya Mitume 18:24

Basi Myahudi mmoja, jina lake Apolo, mzalia wa Iskanderia, mtu wa elimu, akafika Efeso; naye alikuwa hodari katika maandiko.

Matendo ya Mitume 18:25

Mtu huyo alikuwa amefundishwa njia ya Bwana; na kwa kuwa roho yake ilikuwa ikimwaka, alianza kunena na kufundisha kwa usahihi habari za Yesu; naye alijua ubatizo wa Yohana tu.

Matendo ya Mitume 18:26

Akaanza kunena kwa ujasiri katika sinagogi; hata Prisila na Akila walipomsikia wakamchukua kwao, wakamweleza njia ya Bwana kwa usahihi zaidi.

Matendo ya Mitume 18:27

Na alipotaka kuvuka bahari aende mpaka Akaya, ndugu wakamhimiza, wakawaandikia wale wanafunzi wamkaribishe, naye alipofika akawasaidia sana wale waliokwisha kuamini kwa neema ya Mungu.

Matendo ya Mitume 18:28

Kwa maana aliwashinda Wayahudi kabisa kabisa mbele ya watu wote, akionyesha kwa maneno ya maandiko ya kuwa Yesu ni Kristo.