Matendo ya Mitume Mlango 11 Acts

Matendo ya Mitume 11:1

Basi mitume na ndugu waliokuwako katika Uyahudi wakapata habari ya kwamba watu wa Mataifa nao wamelipokea neno la Mungu.

Matendo ya Mitume 11:2

Na Petro alipopanda kwenda Yerusalemu, wale walio wa tohara wakashindana naye,

Matendo ya Mitume 11:3

wakisema, Uliingia kwa watu wasiotahiriwa ukala nao.

Matendo ya Mitume 11:4

Petro akaanza kuwaeleza kwa taratibu, akasema,

Matendo ya Mitume 11:5

Nalikuwa katika mji wa Yafa, nikiomba, roho yangu ikazimia, nikaona maono; chombo kinashuka, kama nguo kubwa inatelemshwa kutoka mbinguni kwa pembe zake nne, kikanifikilia.

Matendo ya Mitume 11:6

Nikakitazama sana, nikifikiri, nikaona wanyama wa nchi wenye miguu minne, na wanyama wa mwituni, nao watambaao, na ndege wa angani.

Matendo ya Mitume 11:7

Nikasikia na sauti ikiniambia, Ondoka, Petro, ukachinje ule.

Matendo ya Mitume 11:8

Nikasema, Hasha, Bwana, kwa maana kitu kilicho kichafu au kilicho najisi hakijaingia kabisa kinywani mwangu.

Matendo ya Mitume 11:9

Sauti ikanijibu mara ya pili kutoka mbinguni, Alivyovitakasa Mungu, usivinene wewe najisi.

Matendo ya Mitume 11:10

Jambo hili likatendeka mara tatu, kisha vitu vyote vikavutwa tena juu mbinguni.

Matendo ya Mitume 11:11

Na tazama, mara hiyo watu watatu wakasimama mbele ya nyumba tuliyokuwamo, waliotumwa kwangu kutoka Kaisaria.

Matendo ya Mitume 11:12

Roho akaniambia nifuatane nao, nisione tashwishi. Ndugu hawa sita nao wakaenda pamoja nami, tukaingia katika nyumba ya mtu yule;

Matendo ya Mitume 11:13

akatueleza jinsi alivyomwona malaika aliyesimama nyumbani mwake na kumwambia, Tuma watu kwenda Yafa ukamwite Simoni aitwaye Petro,

Matendo ya Mitume 11:14

atakayekuambia maneno ambayo yatakuokoa, wewe na nyumba yako yote.

Matendo ya Mitume 11:15

Ikawa nilipoanza kunena, Roho Mtakatifu akawashukia kama alivyotushukia sisi mwanzo.

Matendo ya Mitume 11:16

Nikalikumbuka neno lile la Bwana, jinsi alivyosema, Yohana alibatiza kwa maji kweli, bali ninyi mtabatizwa kwa Roho Mtakatifu.

Matendo ya Mitume 11:17

Basi ikiwa Mwenyezi Mungu amewapa wao karama ile ile aliyotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu Kristo, mimi ni nani niweze kumpinga Mungu?

Matendo ya Mitume 11:18

Waliposikia maneno haya wakanyamaza, wakamtukuza Mungu, wakisema, Basi, Mungu amewajalia hata mataifa nao toba liletalo uzima.

Matendo ya Mitume 11:19

Basi wale waliotawanyika kwa sababu ya ile dhiki iliyotukia kwa habari ya Stefano, wakasafiri hata Foinike na Kipro na Antiokia, wasilihubiri lile neno ila kwa Wayahudi peke yao.

Matendo ya Mitume 11:20

Lakini baadhi ya hao walikuwa watu wa Kipro na Kirene, nao walipofika Antiokia wakasema na Wayahudi wa Kiyunani, wakihubiri habari njema za Bwana Yesu.

Matendo ya Mitume 11:21

Mkono wa Bwana ukawa pamoja nao, watu wengi wakaamini, wakamwelekea Bwana.

Matendo ya Mitume 11:22

Habari hizo za watu hao zikafika masikioni mwa kanisa lililokuwako katika Yerusalemu; wakamtuma Barnaba, aende hata Antiokia.

Matendo ya Mitume 11:23

Naye, alipokwisha kufika na kuiona neema ya Mungu akafurahi, akawasihi wote waambatane na Bwana kwa kusudi la moyo.

Matendo ya Mitume 11:24

Maana alikuwa mtu mwema amejaa Roho Mtakatifu na imani; watu wengi wakaongezeka upande wa Bwana.

Matendo ya Mitume 11:25

Kisha akatoka akaenda Tarso kumtafuta Sauli;

Matendo ya Mitume 11:26

hata alipokwisha kumwona akamleta Antiokia. Ikawa kwa muda wa mwaka mzima wakakusanyika pamoja na kanisa na kuwafundisha watu wengi. Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia.

Matendo ya Mitume 11:27

Siku zizo hizo manabii walitelemka kutoka Yerusalemu hata Antiokia.

Matendo ya Mitume 11:28

Na tulipokusanyika akasimama mmoja wao, jina lake Agabo, akaonyesha kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itakuja karibu katika dunia nzima, nayo ikatukia katika siku za Klaudio.

Matendo ya Mitume 11:29

Na wale wanafunzi, kila mtu kwa kadiri ya alivyofanikiwa, wakaazimu kupeleka msaada kwa ndugu zao waliokaa Uyahudi.

Matendo ya Mitume 11:30

Wakafanya hivyo, wakawapelekea wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.