Matendo ya Mitume Mlango 26 Acts

Matendo ya Mitume 26:1

Agripa akamwambia Paulo, Una ruhusa kusema maneno yako. Ndipo Paulo akanyosha mkono wake, akajitetea,

Matendo ya Mitume 26:2

Najiona nafsi yangu kuwa na heri, Ee mfalme Agripa, kwa kuwa nitajitetea mbele yako leo, katika mambo yale yote niliyoshitakiwa na Wayahudi.

Matendo ya Mitume 26:3

Hasa kwa sababu wewe unajua sana desturi na maswali yote waliyo nayo Wayahudi; kwa sababu hiyo nakuomba unisikilize kwa uvumilivu.

Matendo ya Mitume 26:4

Kwa maana Wayahudi wote wanajua maisha yangu tangu ujana, yaliyokuwa tangu mwanzo katika taifa langu huko Yerusalemu,

Matendo ya Mitume 26:5

wakinijua sana tangu mwanzo, kama wakipenda kushuhudia, ya kwamba nalikuwa Farisayo kwa kuifuata madhehebu ya dini yetu iliyo sahihi kabisa.

Matendo ya Mitume 26:6

Na sasa ninasimama hapa nihukumiwe kwa ajili ya tumaini la ahadi baba zetu waliyopewa na Mungu,

Matendo ya Mitume 26:7

ambayo kabila zetu kumi na mbili wanataraji kuifikia, wakimwabudu Mungu kwa bidii mchana na usiku. Nami ninashitakiwa na Wayahudi kwa ajili ya tumaini hilo, Ee Mfalme.

Matendo ya Mitume 26:8

Kwa nini limedhaniwa kwenu kuwa ni neno lisilosadikika, kwamba Mungu awafufua wafu?

Matendo ya Mitume 26:9

Kweli, mimi mwenyewe naliona ndani ya nafsi yangu kwamba yanipasa kutenda mambo mengi yaliyopingamana na jina lake Yesu Mnazareti;

Matendo ya Mitume 26:10

nami nikayafanya hayo Yerusalemu; niliwafunga wengi miongoni mwa watakatifu ndani ya magereza, nikiisha kupewa amri na wakuu wa makuhani; na walipouawa nalitoa idhini yangu.

Matendo ya Mitume 26:11

Na mara nyingi katika masinagogi yote naliwaadhibu, nikawashurutisha kukufuru; nikawaonea hasira kama mwenye wazimu, nikawaudhi hata katika miji ya ugenini.

Matendo ya Mitume 26:12

Basi katika kazi hiyo nilipokuwa nikienda Dameski, mwenye mamlaka na maagizo ya wakuu wa makuhani;

Matendo ya Mitume 26:13

Ee Mfalme, ndipo wakati wa adhuhuri njiani naliona nuru inatoka mbinguni ipitayo mwangaza wa jua, ikinimulikia mimi, na wale waliofuatana nami pande zote.

Matendo ya Mitume 26:14

Tukaanguka nchi sote, nikasikia sauti ikisema nami kwa lugha ya kiebrania, Sauli! Sauli! Mbona waniudhi? Ni vigumu kwako kuupiga mateke mchokoo.

Matendo ya Mitume 26:15

Nami nikasema, Wewe u nani, Bwana? Bwana akaniambia, Mimi ni Yesu, ambaye wewe unaniudhi.

Matendo ya Mitume 26:16

Lakini inuka, usimame kwa miguu yako, maana nimekutokea kwa sababu hii, nikuweke wewe uwe mtumishi na shahidi wa mambo haya uliyoyaona, na wa mambo ambayo katika hayo nitajidhihirisha kwako;

Matendo ya Mitume 26:17

nikikuokoa na watu wako, na watu wa Mataifa, ambao nakutuma kwao;

Matendo ya Mitume 26:18

uwafumbue macho yao, na kuwageuza waiache giza na kuielekea nuru, waziache na nguvu za Shetani na kumwelekea Mungu; kisha wapate msamaha wa dhambi zao, na urithi miongoni mwao waliotakaswa kwa imani iliyo kwangu mimi.

Matendo ya Mitume 26:19

Kwa hiyo, Ee Mfalme Agripa, sikuyaasi yale maono ya mbinguni,

Matendo ya Mitume 26:20

bali kwanza niliwahubiri wale wa Dameski na Yerusalemu, na katika nchi yote ya Uyahudi, na watu wa Mataifa, kwamba watubu na kumwelekea Mungu, wakiyatenda matendo yanayopatana na kutubu kwao.

Matendo ya Mitume 26:21

Kwa sababu ya hayo Wayahudi wakanikamata ndani ya hekalu wakajaribu kuniua.

Matendo ya Mitume 26:22

Basi kwa kuwa nimeupata msaada utokao kwa Mungu nimesimama hata leo hivi nikiwashuhudia wadogo kwa wakubwa, wala sisemi neno ila yale ambayo manabii na Musa waliyasema, kwamba yatakuwa;

Matendo ya Mitume 26:23

ya kwamba Kristo hana budi kuteswa na ya kwamba yeye kwanza kwa kufufuliwa katika wafu atatangaza habari za nuru kwa watu wake na kwa watu wa Mataifa.

Matendo ya Mitume 26:24

Alipokuwa akijitetea hivi, Festo akasema kwa sauti kuu, Paulo, una wazimu, kusoma kwako kwingi kumekugeuza akili.

Matendo ya Mitume 26:25

Lakini Paulo akasema, Sina wazimu, Ee Festo mtukufu, bali nanena maneno ya kweli na ya akili kamili.

Matendo ya Mitume 26:26

Kwa maana mfalme anajua habari za mambo haya, nami naweza kusema naye kwa ujasiri, kwa sababu najua sana ya kuwa hapana neno moja katika hayo asilolijua; kwa maana jambo hilo halikutendeka pembeni.

Matendo ya Mitume 26:27

Mfalme Agripa, je! Wawaamini manabii? Najua ya kuwa wawaamini.

Matendo ya Mitume 26:28

Agripa akamwambia Paulo, Kwa maneno machache wadhani kunifanya mimi kuwa Mkristo.

Matendo ya Mitume 26:29

Paulo akamjibu, Namwomba Mungu kwamba, ikiwa kwa machache au ikiwa kwa mengi, si wewe tu ila na hao wote wanaonisikia leo wawe kama mimi, isipokuwa vifungo hivi.

Matendo ya Mitume 26:30

Mfalme na liwali na Bernike na wale walioketi pamoja nao wakasimama;

Matendo ya Mitume 26:31

hata walipoondoka wakasemezana, wakisema, Mtu huyu hatendi neno linalostahili kifo wala kufungwa.

Matendo ya Mitume 26:32

Agripa akamwambia Festo, Mtu huyo angeweza kufunguliwa, kama asingalitaka rufani kwa Kaisari.