Matendo ya Mitume Mlango 20 Acts

Matendo ya Mitume 20:1

Kishindo kile kilipokoma, Paulo akatuma kuwaita wanafunzi akawaonya, akaagana nao, kisha akaondoka aende zake mpaka Makedonia.

Matendo ya Mitume 20:2

Naye akiisha kupita pande zile na kuwafariji kwa maneno mengi, akafika Uyunani.

Matendo ya Mitume 20:3

Alipokwisha kukaa huko miezi mitatu, na Wayahudi kumfanyia vitimvi, alipotaka kwenda Shamu kwa njia ya bahari; basi akaazimu kurejea kwa njia ya Makedonia.

Matendo ya Mitume 20:4

Watu hawa wakafuatana naye, Sopatro Mberoya, mwana wa Piro, na Aristarko na Sekundo, watu wa Thesalonike; na Gayo mtu wa Derbe, na Timotheo; na Tikiko na Trofimo watu wa Asia.

Matendo ya Mitume 20:5

Ila watu hao wamekwisha kutangulia wakamngojea Troa.

Matendo ya Mitume 20:6

Sisi tukatweka baada ya siku za mikate isiyotiwa chachu, tukatoka Filipi, tukawafikia Troa, safari ya siku tano, tukakaa huko siku saba.

Matendo ya Mitume 20:7

Hata siku ya kwanza ya juma, tulipokuwa tumekutana ili kumega mkate, Paulo akawahutubu, akiazimu kusafiri siku ya pili yake, naye akafuliza maneno yake hata usiku wa manane.

Matendo ya Mitume 20:8

Palikuwa na taa nyingi katika orofa ile tulipokuwa tumekusanyika.

Matendo ya Mitume 20:9

Kijana mmoja, jina lake Eutiko, alikuwa ameketi dirishani, akalemewa na usingizi sana; hata Paulo alipoendelea sana kuhubiri, akazidiwa na usingizi wake akaanguka toka orofa ya tatu; akainuliwa amekwisha kufa.

Matendo ya Mitume 20:10

Paulo akashuka, akamwangukia, akamkumbatia, akasema, Msifanye ghasia, maana uzima wake ungalimo ndani yake.

Matendo ya Mitume 20:11

Akapanda juu tena, akamega mkate, akala, akazidi kuongea nao hata alfajiri, ndipo akaenda zake.

Matendo ya Mitume 20:12

Wakamleta yule kijana, yu mzima, wakafarijika faraja kubwa sana.

Matendo ya Mitume 20:13

Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni, tukaabiri kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu.

Matendo ya Mitume 20:14

Alipotufikia huko Aso, tukampakia, kisha tukafika Mitilene.

Matendo ya Mitume 20:15

Tukatweka kutoka huko, na siku ya pili tukafika mahali panapokabili Kio; siku ya tatu tukawasili Samo, tukakaa Trogilio, siku ya nne tukafika Mileto.

Matendo ya Mitume 20:16

Kwa sababu Paulo amekusudia kupita Efeso merikebuni, asije akakawia katika Asia; kwa maana alikuwa na haraka, akitaka kuwahi Yerusalemu siku ya Pentekoste, kama ikiwezekana.

Matendo ya Mitume 20:17

Toka Mileto Paulo akatuma watu kwenda Efeso, akawaita wazee wa kanisa.

Matendo ya Mitume 20:18

Walipofika kwake, akawaambia, Ninyi wenyewe mnajua tangu siku ya kwanza nilipokanyaga hapa Asia, jinsi nilivyokuwa kwenu wakati wote,

Matendo ya Mitume 20:19

nikimtumikia Bwana kwa unyenyekevu wote, na kwa machozi, na majaribu yaliyonipata kwa hila za Wayahudi;

Matendo ya Mitume 20:20

ya kuwa sikujiepusha katika kuwatangazia neno lo lote liwezalo kuwafaa bali naliwafundisha waziwazi, na nyumba kwa nyumba,

Matendo ya Mitume 20:21

nikiwashuhudia Wayahudi na Wayunani wamtubie Mungu, na kumwamini Bwana wetu Yesu Kristo.

Matendo ya Mitume 20:22

Basi sasa, angalieni, nashika njia kwenda Yerusalemu hali nimefungwa rohoni, nisiyajue mambo yatakayonikuta huko;

Matendo ya Mitume 20:23

isipokuwa Roho Mtakatifu mji kwa mji hunishuhudia akisema, ya kwamba vifungo na dhiki vyaningoja.

Matendo ya Mitume 20:24

Lakini siyahesabu maisha yangu kuwa kitu cha thamani kwangu kama kuumaliza mwendo wangu na huduma ile niliyopokea kwa Bwana Yesu, kuishuhudia Habari Njema ya neema ya Mungu.

Matendo ya Mitume 20:25

Na sasa, tazameni, mimi najua ya kuwa ninyi nyote niliowahubiria ufalme wa Mungu, nikienda huko na huko, hamtaniona uso tena.

Matendo ya Mitume 20:26

Kwa hiyo nawashuhudia wote siku hii ya leo, ya kuwa mimi sina hatia kwa damu ya mtu awaye yote.

Matendo ya Mitume 20:27

Kwa maana sikujiepusha na kuwahubiria habari ya kusudi lote la Mungu.

Matendo ya Mitume 20:28

Jitunzeni nafsi zenu, na lile kundi lote nalo, ambalo Roho Mtakatifu amewaweka ninyi kuwa waangalizi ndani yake, mpate kulilisha kanisa lake Mungu, alilolinunua kwa damu yake mwenyewe.

Matendo ya Mitume 20:29

Najua mimi ya kuwa baada ya kuondoka kwangu mbwa-mwitu wakali wataingia kwenu, wasilihurumie kundi;

Matendo ya Mitume 20:30

tena katika ninyi wenyewe watainuka watu wakisema mapotovu, wawavute hao wanafunzi wawaandamie wao.

Matendo ya Mitume 20:31

Kwa hiyo kesheni, mkikumbuka ya kwamba miaka mitatu, usiku na mchana, sikuacha kumwonya kila mtu kwa machozi.

Matendo ya Mitume 20:32

Basi, sasa nawaweka katika mikono ya Mungu, na kwa neno la neema yake, ambalo laweza kuwajenga na kuwapa urithi pamoja nao wote waliotakaswa.

Matendo ya Mitume 20:33

Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.

Matendo ya Mitume 20:34

Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.

Matendo ya Mitume 20:35

Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, na kuyakumbuka maneno ya Bwana Yesu, jinsi alivyosema mwenyewe, Ni heri kutoa kuliko kupokea.

Matendo ya Mitume 20:36

Alipokwisha kunena haya akapiga magoti, akaomba pamoja nao wote.

Matendo ya Mitume 20:37

Wakalia sana wote, wakamwangukia Paulo shingoni, wakambusu-busu,

Matendo ya Mitume 20:38

wakihuzunika zaidi kwa sababu ya neno lile alilosema, ya kwamba hawatamwona uso tena. Wakamsindikiza hata merikebuni.