Matendo ya Mitume Mlango 21 Acts

Matendo ya Mitume 21:1

Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na kuabiri, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara,

Matendo ya Mitume 21:2

tukapata merikebu itakayovuka mpaka Foinike tukapanda tukatweka.

Matendo ya Mitume 21:3

Na tulipoona Kipro tukaiacha upande wa kushoto; tukasafiri mpaka Shamu tukashuka Tiro. Kwa maana huko ndiko merikebu yetu itakakoshusha shehena yake.

Matendo ya Mitume 21:4

Tukiisha kuwaona wanafunzi tukakaa huko siku saba, nao wakamwambia Paulo kwa uweza wa Roho asipande kwenda Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 21:5

Hata tulipotimiza siku zile tukaondoka tukaenda zetu, na watu wote, pamoja na wake zao na watoto wao, wakatusindikiza mpake nje ya mji, tukapiga magoti pwani tukaomba;

Matendo ya Mitume 21:6

na baada ya kuagana tukapanda merikebuni, nao wakarudi kwao.

Matendo ya Mitume 21:7

Hata tulipomaliza safari yetu kutoka Tiro tukafika Tolemai, tukawaamkua ndugu tukakaa kwao siku moja.

Matendo ya Mitume 21:8

Asubuhi yake tukaondoka, tukafika Kaisaria, tukaingia nyumbani mwa Filipo, mhubiri wa Injili, aliyekuwa mmoja wa wale saba, tukakaa kwake.

Matendo ya Mitume 21:9

Mtu huyu alikuwa na binti wanne, mabikira, waliokuwa wakitabiri.

Matendo ya Mitume 21:10

Basi tulipokuwa tukikaa huko siku nyingi, nabii mmoja jina lake Agabo akashuka kutoka Uyahudi.

Matendo ya Mitume 21:11

Alipotufikia akautwaa mshipi wa Paulo, akajifunga miguu na mikono, akasema, Roho Mtakatifu asema hivi, Hivyo ndivyo Wayahudi wa Yerusalemu watakavyomfunga mtu mwenye mshipi huu, nao watamtia katika mikono ya watu wa Mataifa.

Matendo ya Mitume 21:12

Basi tuliposikia haya, sisi na watu wa mahali pale, tukamsihi asipande kwenda Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 21:13

Ndipo Paulo alipojibu, Mnafanya nini, kulia na kunivunja moyo? Kwa maana mimi, licha ya kufungwa, ni tayari hata kuuawa katika Yerusalemu kwa ajili ya jina lake Bwana Yesu.

Matendo ya Mitume 21:14

Alipokataa shauri letu, tukanyamaza tukisema, Mapenzi ya Bwana na yatendeke.

Matendo ya Mitume 21:15

Baada ya siku zile tukachukua vyombo vyetu tukapanda kwenda Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 21:16

Baadhi ya wanafunzi wa Kaisaria wakafuatana na sisi, wakamchukua na Mnasoni, mtu wa Kipro, mwanafunzi wa zamani ambaye ndiye tutakayekaa kwake.

Matendo ya Mitume 21:17

Tulipofika Yerusalemu wale ndugu wakatukaribisha kwa furaha.

Matendo ya Mitume 21:18

Hata siku ya pili yake Paulo akaingia kwa Yakobo pamoja nasi, na wazee wote walikuwako.

Matendo ya Mitume 21:19

Na baada ya kuwaamkua, akawaeleza mambo yote moja moja Mungu aliyoyatenda katika Mataifa kwa huduma yake.

Matendo ya Mitume 21:20

Nao waliposikia wakamtukuza Mungu, wakamwambia, Ndugu yetu, unaona jinsi Wayahudi walioamini walivyo elfu nyingi, nao wote wana wivu sana kwa ajili ya torati.

Matendo ya Mitume 21:21

Nao wameambiwa habari zako, ya kwamba unawafundisha Wayahudi wote wakaao katika Mataifa kumwacha Musa, ukiwaambia wasiwatahiri watoto wao, wala wasizifuate desturi.

Matendo ya Mitume 21:22

Basi, ni nini? Bila shaka watasikia kwamba umekuja.

Matendo ya Mitume 21:23

Basi fanya neno hili tunalokuambia. Wako kwetu watu wanne waliofungwa na nadhiri.

Matendo ya Mitume 21:24

Wachukue watu hao, ujitakase pamoja nao, na kuwagharimia ili wanyoe vichwa vyao, watu wote wapate kujua ya kuwa habari zile walizoambiwa juu yako si kitu, bali wewe mwenyewe unaenenda vizuri na kuishika torati.

Matendo ya Mitume 21:25

Lakini kwa habari za watu wa Mataifa walioamini, tuliandika na kutoa hukumu yetu ya wao kujilinda nafsi zao na vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na damu, na kitu kilichosongolewa, na uasherati.

Matendo ya Mitume 21:26

Ndipo Paulo akawatwaa wanaume wale, na siku ya pili yake akajitakasa nafsi yake pamoja nao, akaingia ndani ya hekalu, akitangaza habari ya kutimiza siku za utakaso, hata sadaka itolewe kwa ajili ya kila mmoja wao.

Matendo ya Mitume 21:27

Basi zile siku saba zilipokuwa karibu kutimia, Wayahudi waliotoka Asia wakamwona ndani ya hekalu, wakawataharakisha watu wote, wakamkamata,

Matendo ya Mitume 21:28

wakapiga kelele, na kusema, Enyi wanaume wa Israeli, tusaidieni. Huyu ndiye mtu yule afundishaye watu wote kila mahali kinyume cha taifa letu na torati na mahali hapa. Tena, zaidi ya haya, amewaingiza Wayunani katika hekalu, akapatia unajisi mahali hapa patakatifu.

Matendo ya Mitume 21:29

Kwa maana walikuwa wamemwona Trofimo, Mwefeso, pamoja naye mjini, ambaye walidhania ya kuwa Paulo amemwingiza katika hekalu.

Matendo ya Mitume 21:30

Mji wote ukataharuki, watu wakakutanika mbio mbio, wakamkamata Paulo, wakamkokota, wakamtoa hekaluni; mara milango ikafungwa.

Matendo ya Mitume 21:31

Na walipokuwa wakitafuta njia ya kumwua, habari zikamfikilia jemadari wa kikosi ya kwamba Yerusalemu imechafuka, mji mzima.

Matendo ya Mitume 21:32

Mara akatwaa askari na maakida, akawashukia mbio. Nao walipomwona jemadari na askari wakaacha kumpiga Paulo.

Matendo ya Mitume 21:33

Kisha jemadari akakaribia, akamshika, akaamuru afungwe kwa minyororo miwili; akauliza, Nani huyu? Tena, amefanya nini?

Matendo ya Mitume 21:34

Wengine katika makutano wakapiga kelele wakisema hivi, na wengine hivi. Basi alipokuwa hawezi kupata hakika ya habari kwa sababu ya zile kelele, akatoa amri aletwe ndani ya ngome.

Matendo ya Mitume 21:35

Basi Paulo alipofika darajani ilikuwa kuchukuliwa na askari kwa sababu ya nguvu ya makutano.

Matendo ya Mitume 21:36

Maana kundi kubwa la watu wakamfuata, wakipiga kelele, na kusema, Mwondoe huyu.

Matendo ya Mitume 21:37

Naye alipokuwa analetwa ndani ya ngome, Paulo akamwambia jemadari, Nina ruhusa nikuambie neno? Naye akasema, Je! Unajua Kiyunani?

Matendo ya Mitume 21:38

Wewe si yule Mmisri ambaye kabla ya siku hizi aliwafitinisha wale watu elfu nne, walioitwa Wauaji, akawaongoza jangwani?

Matendo ya Mitume 21:39

Paulo akasema, Mimi ni mtu wa Kiyahudi, mtu wa Tarso, mji wa Kilikia, mwenyeji wa mji usiokuwa mnyonge. Nakuomba, nipe ruhusa niseme na wenyeji hawa.

Matendo ya Mitume 21:40

Basi, alipompa ruhusa, Paulo akasimama madarajani, akawapungia mkono wale wenyeji; na ilipokuwa kimya kabisa, akanena nao kwa lugha ya Kiebrania, akisema,