Matendo ya Mitume Mlango 13 Acts

Matendo ya Mitume 13:1

Na huko Antiokia katika kanisa lililokuwako palikuwa na manabii na waalimu, nao ni Barnaba, na Simeoni aitwaye Nigeri, na Lukio Mkirene, na Manaeni aliyekuwa ndugu wa kunyonya wa mfalme Herode, na Sauli.

Matendo ya Mitume 13:2

Basi hawa walipokuwa wakimfanyia Bwana ibada na kufunga, Roho Mtakatifu akasema, Nitengeeni Barnaba na Sauli kwa kazi ile niliyowaitia.

Matendo ya Mitume 13:3

Ndipo wakiisha kufunga na kuomba, wakaweka mikono yao juu yao, wakawaacha waende zao.

Matendo ya Mitume 13:4

Basi watu hao, wakiisha kupelekwa na Roho Mtakatifu wakatelemkia Seleukia, na kutoka huko wakasafiri baharini hata Kipro.

Matendo ya Mitume 13:5

Na walipokuwa katika Salami wakalihubiri neno la Mungu katika masinagogi ya Wayahudi, nao walikuwa naye Yohana kuwa mtumishi wao.

Matendo ya Mitume 13:6

Walipokwisha kupita katikati ya kisiwa chote mpaka Pafo, wakaona mtu mmoja, mchawi, nabii wa uongo, Myahudi jina lake Bar-Yesu;

Matendo ya Mitume 13:7

mtu huyu alikuwa pamoja na liwali Sergio Paulo, mtu mwenye akili. Yeye liwali akawaita Barnaba na Sauli waje kwake, akataka kulisikia neno la Mungu.

Matendo ya Mitume 13:8

Lakini Elima, yule mchawi (maana ndiyo tafsiri ya jina lake), akashindana nao, akitaka kumtia yule liwali moyo wa kuiacha ile imani.

Matendo ya Mitume 13:9

Lakini Sauli, ambaye ndiye Paulo, akijaa Roho Mtakatifu, akamkazia macho,

Matendo ya Mitume 13:10

akasema, Ewe mwenye kujaa hila na uovu wote, mwana wa Ibilisi, adui wa haki yote, huachi kuzipotoa njia za Bwana zilizonyoka?

Matendo ya Mitume 13:11

Basi, angalia, mkono wa Bwana u juu yako, nawe utakuwa kipofu, usilione jua kwa muda. Mara kiwi kikamwangukia na giza, akazunguka-zunguka na kumtafuta mtu wa kumshika mkono na kumwongoza.

Matendo ya Mitume 13:12

Ndipo yule liwali, alipoyaona yaliyotendeka, akaamini, akiyastaajabia mafundisho ya Bwana.

Matendo ya Mitume 13:13

Kisha Paulo na wenziwe wakang'oa nanga wakasafiri kutoka Pafo, wakafika Perge katika Pamfilia. Yohana akawaacha akarejea Yerusalemu.

Matendo ya Mitume 13:14

Lakini wao wakatoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia, wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi.

Matendo ya Mitume 13:15

Kisha, baada ya kusomwa torati na chuo cha manabii, wakuu wa sinagogi wakatuma mtu kwao, na kuwaambia, Ndugu, kama mkiwa na neno la kuwafaa watu hawa, lisemeni.

Matendo ya Mitume 13:16

Paulo akasimama, akawapungia mkono, akasema, Enyi waume wa Israeli, nanyi mnaomcha Mungu, sikilizeni.

Matendo ya Mitume 13:17

Mungu wa watu hawa Israeli aliwachagua baba zetu, akawatukuza watu hao, walipokuwa wakikaa kama wageni katika nchi ya Misri, na kwa mkono ulioinuliwa akawatoa, akawaongoza.

Matendo ya Mitume 13:18

Na kwa muda wa miaka kama arobaini akawavumilia katika jangwa.

Matendo ya Mitume 13:19

Na alipokwisha kuwaharibu mataifa saba katika nchi ya Kanaani akawapa nchi yao iwe urithi kwa muda wa miaka kama mia nne na hamsini;

Matendo ya Mitume 13:20

baada ya hayo akawapa waamuzi hata zamani za nabii Samweli.

Matendo ya Mitume 13:21

Hatimaye wakaomba kupewa mfalme; Mungu akawapa Sauli mwana wa Kishi, mtu wa kabila ya Benyamini, kwa muda wa miaka arobaini.

Matendo ya Mitume 13:22

Na alipokwisha kumwondoa huyo, akamwinua Daudi awe mfalme wao ambaye alimshuhudia, akisema, Nimemwona Daudi, mwana wa Yese, mtu anayeupendeza moyo wangu, atakayefanya mapenzi yangu yote.

Matendo ya Mitume 13:23

Katika uzao wake mtu huyo Mungu amewaletea Israeli Mwokozi, yaani, Yesu, kama alivyoahidi;

Matendo ya Mitume 13:24

Yohana alipokuwa amekwisha kuwahubiri watu wote wa Israeli habari za ubatizo wa toba, kabla ya kuja kwake.

Matendo ya Mitume 13:25

Naye Yohana alipokuwa akimaliza mwendo wake alinena, Mwanidhani mimi kuwa nani? Mimi siye. Lakini, angalieni, anakuja mmoja nyuma yangu ambaye mimi sistahili kumlegezea viatu vya miguu yake.

Matendo ya Mitume 13:26

Ndugu zangu, wana wa ukoo wa Ibrahimu, na hao miongoni mwenu wanaomcha Mungu, kwetu sisi neno la wokovu huu limepelekwa.

Matendo ya Mitume 13:27

Kwa maana wakaao Yerusalemu, na wakuu wao, kwa kuwa hawakumjua yeye, wala maneno ya manabii yanayosomwa kila sabato, wameyatimiza kwa kumhukumu.

Matendo ya Mitume 13:28

Na ijapokuwa hawakuona sababu ya kumfisha wakamwomba Pilato auawe.

Matendo ya Mitume 13:29

Hata walipokwisha kumaliza yote aliyoandikiwa, wakamtelemsha katika ule mti, wakamweka kaburini.

Matendo ya Mitume 13:30

Lakini Mungu akamfufua katika wafu;

Matendo ya Mitume 13:31

akaonekana siku nyingi na wale waliopanda naye kutoka Galilaya hata Yerusalemu, ambao sasa ndio walio mashahidi wake mbele ya watu.

Matendo ya Mitume 13:32

Na sisi tunawahubiri habari njema ya ahadi ile waliyopewa mababa,

Matendo ya Mitume 13:33

ya kwamba Mungu amewatimizia watoto wetu ahadi hiyo, kwa kumfufua Yesu; kama ilivyoandikwa katika Zaburi ya pili, Wewe ndiwe Mwanangu, mimi leo nimekuzaa.

Matendo ya Mitume 13:34

Tena ya kuwa alimfufua katika wafu, asipate kurudia uharibifu, amenena hivi, Nitawapa ninyi mambo matakatifu ya Daudi yaliyo amini.

Matendo ya Mitume 13:35

Kwa hiyo anena na pengine, Hutamwachia Mtakatifu wako kuona uharibifu,

Matendo ya Mitume 13:36

Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake, akaona uharibifu.

Matendo ya Mitume 13:37

Bali huyu aliyefufuliwa na Mungu hakuona uharibifu.

Matendo ya Mitume 13:38

Basi, na ijulikane kwenu, ndugu zangu, ya kuwa kwa huyo mnahubiriwa msamaha wa dhambi;

Matendo ya Mitume 13:39

na kwa yeye kila amwaminiye huhesabiwa haki katika mambo yale yote asiyoweza kuhesabiwa haki kwa torati ya Musa.

Matendo ya Mitume 13:40

Angalieni, basi, isiwajilie habari ile iliyonenwa katika manabii.

Matendo ya Mitume 13:41

Tazameni, enyi mnaodharau, kastaajabuni, mkatoweke; kwa kuwa natenda kazi mimi siku zenu, kazi ambayo msingeisadiki kabisa, ijapo mtu akiwasimulia sana.

Matendo ya Mitume 13:42

Na walipokuwa wakitoka, wakawasihi waambiwe maneno haya sabato ya pili.

Matendo ya Mitume 13:43

Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika neema ya Mungu.

Matendo ya Mitume 13:44

Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno la Mungu.

Matendo ya Mitume 13:45

Bali Wayahudi, walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na Paulo, wakibisha na kutukana.

Matendo ya Mitume 13:46

Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa.

Matendo ya Mitume 13:47

Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia.

Matendo ya Mitume 13:48

Mataifa waliposikia hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.

Matendo ya Mitume 13:49

Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote.

Matendo ya Mitume 13:50

Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika mipaka yao.

Matendo ya Mitume 13:51

Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio.

Matendo ya Mitume 13:52

Na wanafunzi walijaa furaha na Roho Mtakatifu.