Matendo ya Mitume Mlango 6 Acts

Matendo ya Mitume 6:1

Hata siku zile wanafunzi walipokuwa wakiongezeka hesabu yao, palikuwa na manung'uniko ya Wayahudi wa Kiyunani juu ya Waebrania kwa sababu wajane wao walisahauliwa katika huduma ya kila siku.

Matendo ya Mitume 6:2

Wale Thenashara wakawaita jamii ya wanafunzi, wakasema, Haipendezi sisi kuliacha neno la Mungu na kuhudumu mezani.

Matendo ya Mitume 6:3

Basi ndugu, chagueni watu saba miongoni mwenu, walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho, na hekima, ili tuwaweke juu ya jambo hili;

Matendo ya Mitume 6:4

na sisi tutadumu katika kuomba na kulihudumia lile Neno.

Matendo ya Mitume 6:5

Neno hili likapendeza machoni pa mkutano wote; wakamchagua Stefano, mtu aliyejaa imani na Roho Mtakatifu, na Filipo, na Prokoro, na Nikanori, na Timoni, na Parmena, na Nikolao mwongofu wa Antiokia;

Matendo ya Mitume 6:6

ambao wakawaweka mbele ya mitume, na walipokwisha kuomba wakaweka mikono yao juu yao.

Matendo ya Mitume 6:7

Neno la Mungu likaenea; na hesabu ya wanafunzi ikazidi sana katika Yerusalemu; jamii kubwa ya makuhani wakaitii ile Imani.

Matendo ya Mitume 6:8

Na Stefano, akijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu.

Matendo ya Mitume 6:9

Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano;

Matendo ya Mitume 6:10

lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye.

Matendo ya Mitume 6:11

Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu.

Matendo ya Mitume 6:12

Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza.

Matendo ya Mitume 6:13

Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati;

Matendo ya Mitume 6:14

maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa.

Matendo ya Mitume 6:15

Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika.