Yoshua Mlango 23 Joshua

Yoshua 23:1

Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana,

Yoshua 23:2

Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu;

Yoshua 23:3

nanyi mmeona mambo yote ambayo Bwana, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi.

Yoshua 23:4

Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua.

Yoshua 23:5

Yeye Bwana, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama Bwana Mungu wenu, alivyowaambia.

Yoshua 23:6

Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto.

Yoshua 23:7

Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao;

Yoshua 23:8

bali shikamaneni na Bwana, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo.

Yoshua 23:9

Maana Bwana amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo.

Yoshua 23:10

Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana Bwana, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia.

Yoshua 23:11

Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu.

Yoshua 23:12

Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu;

Yoshua 23:13

jueni hakika ya kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi.

Yoshua 23:14

Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena Bwana, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa.

Yoshua 23:15

Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, Bwana, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika Bwana atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, Bwana Mungu wenu, aliyowapa.

Yoshua 23:16

Hapo mtakapolivunja agano la Bwana, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya Bwana itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.