Nehemia Mlango 9 Nehemiah

Nehemia 9:1

Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani.

Nehemia 9:2

Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao.

Nehemia 9:3

Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha torati ya Bwana, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama, wakamwabudu Bwana, Mungu wao.

Nehemia 9:4

Ndipo wakasimama madarajani pa Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia Bwana, Mungu wao, kwa sauti kuu.

Nehemia 9:5

Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi Bwana, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.

Nehemia 9:6

Ezra akasema, Wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako; wewe ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe.

Nehemia 9:7

Wewe ndiwe Bwana, Mungu, uliyemchagua Abramu, na kumtoa katika Uri wa Wakaldayo, na kumpa jina la Ibrahimu;

Nehemia 9:8

nawe ukauona moyo wake kuwa mwaminifu mbele zako, ukafanya agano naye, kumpa nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Myebusi, na Mgirgashi, naam, kuwapa wazao wake; nawe umeyafikiliza maneno yako, kwa kuwa ndiwe mwenye haki.

Nehemia 9:9

Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya bahari ya Shamu;

Nehemia 9:10

nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao, na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo leo.

Nehemia 9:11

Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe katika maji makuu.

Nehemia 9:12

Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.

Nehemia 9:13

Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;

Nehemia 9:14

ukawajulisha sabato yako takatifu, na kuwaagiza maagizo, na amri, na sheria, kwa mkono wa mtumishi wako, Musa.

Nehemia 9:15

Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru kwamba waingie katika nchi na kuimiliki, ambayo umeinua mkono wako kuwapa.

Nehemia 9:16

Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,

Nehemia 9:17

ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.

Nehemia 9:18

Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;

Nehemia 9:19

hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.

Nehemia 9:20

Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.

Nehemia 9:21

Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.

Nehemia 9:22

Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.

Nehemia 9:23

Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.

Nehemia 9:24

Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.

Nehemia 9:25

Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.

Nehemia 9:26

Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.

Nehemia 9:27

Kwa sababu hiyo ukawatia katika mikono ya adui zao, waliowasumbua; na wakati wa shida yao, walipokulilia, uliwasikia kutoka mbinguni; na kwa wingi wa rehema zako ukawapa waokozi waliowaokoa katika mikono ya adui zao.

Nehemia 9:28

Lakini walipokuwa wamekwisha kustarehe, walitenda mabaya tena mbele zako; kwa hiyo ukawaacha katika mikono ya adui zao, nao wakawatawala; hata hivyo waliporejea na kukulilia, uliwasikia toka mbinguni; ukawaokoa mara nyingi kwa rehema zako;

Nehemia 9:29

ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakazihalifu hukumu zako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.

Nehemia 9:30

Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.

Nehemia 9:31

Ila kwa rehema zako nyingi hukuwakomesha kabisa, wala kuwaacha; kwa maana wewe u Mungu mwenye neema, mwenye rehema.

Nehemia 9:32

Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya, mwenye kushika maagano na rehema, mashaka yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote, tangu zamani za wafalme wa Ashuru hata leo, na yasihesabiwe kuwa ni madogo.

Nehemia 9:33

Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo mabaya;

Nehemia 9:34

na wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na baba zetu, hawakuishika sheria yako, wala hawakuzisikiliza amri zako na shuhuda zako, ulizowashuhudia.

Nehemia 9:35

Kwa kuwa hawakukutumikia wewe katika ufalme wao, na katika wema wako mkuu uliowapa, na katika nchi ile kubwa yenye neema uliyowapa mbele yao, wala hawakughairi na kuyaacha mabaya yao.

Nehemia 9:36

Tazama, sisi hapa tu watumwa leo, na katika habari ya nchi hii uliyowapa baba zetu, wapate kula matunda yake na mema yake, tazama, sisi hapa tu watumwa ndani yake.

Nehemia 9:37

Nayo yawapatia faida nyingi wafalme uliowaweka juu yetu kwa sababu ya dhambi zetu; tena wana mamlaka juu ya miili yetu, na juu ya wanyama wetu, kadiri wapendavyo, nasi tu katika dhiki kuu.

Nehemia 9:38

Na kwa sababu ya hayo yote sisi twafanya agano la hakika, na kuliandika; na wakuu wetu, na Walawi wetu, na makuhani wetu, wanalitilia muhuri.