Nehemia Mlango 6 Nehemiah

Nehemia 6:1

Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);

Nehemia 6:2

Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.

Nehemia 6:3

Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?

Nehemia 6:4

Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.

Nehemia 6:5

Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;

Nehemia 6:6

nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.

Nehemia 6:7

Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja.

Nehemia 6:8

Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.

Nehemia 6:9

Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.

Nehemia 6:10

Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.

Nehemia 6:11

Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.

Nehemia 6:12

Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.

Nehemia 6:13

Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.

Nehemia 6:14

Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati sawasawa na hayo matendo yao, na yule nabii mke Noadia, na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.

Nehemia 6:15

Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.

Nehemia 6:16

Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo makafiri wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.

Nehemia 6:17

Tena siku zile wakuu wa Yuda walimletea Tobia nyaraka nyingi, nazo nyaraka za Tobia zikawafikilia.

Nehemia 6:18

Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.

Nehemia 6:19

Tena waliyanena mema yake mbele yangu, nayo maneno yangu humwambia yeye. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofisha.