Waebrania Mlango 3 Hebrews

Waebrania 3:1

Kwa hiyo, ndugu watakatifu, wenye kuushiriki mwito wa mbinguni, mtafakarini sana Mtume na Kuhani Mkuu wa maungamo yetu, Yesu,

Waebrania 3:2

aliyekuwa mwaminifu kwake yeye aliyemweka, kama Musa naye alivyokuwa, katika nyumba yote ya Mungu.

Waebrania 3:3

Kwa maana huyo amehesabiwa kuwa amestahili utukufu zaidi kuliko Musa, kama vile yeye aitengenezaye nyumba alivyo na heshima zaidi ya hiyo nyumba.

Waebrania 3:4

Maana kila nyumba imetengenezwa na mtu; ila yeye aliyevitengeneza vitu vyote ni Mungu.

Waebrania 3:5

Na Musa kweli alikuwa mwaminifu katika nyumba yote ya Mungu kama mtumishi, awe ushuhuda wa mambo yatakayonenwa baadaye;

Waebrania 3:6

bali Kristo, kama mwana, juu ya nyumba ya Mungu; ambaye nyumba yake ni sisi, kama tukishikamana sana na ujasiri wetu na fahari ya taraja letu mpaka mwisho.

Waebrania 3:7

Kwa hiyo, kama anenavyo Roho Mtakatifu, Leo, kama mtaisikia sauti yake,

Waebrania 3:8

Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha, Siku ya kujaribiwa katika jangwa,

Waebrania 3:9

Hapo baba zenu waliponijaribu, wakanipima, Wakaona matendo yangu miaka arobaini.

Waebrania 3:10

Kwa hiyo nalichukizwa na kizazi hiki, Nikasema, Sikuzote ni watu waliopotoka mioyo hawa; Hawakuzijua njia zangu;

Waebrania 3:11

Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.

Waebrania 3:12

Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

Waebrania 3:13

Lakini mwonyane kila siku, maadamu iitwapo leo; ili mmoja wenu asifanywe mgumu kwa udanganyifu wa dhambi.

Waebrania 3:14

Kwa maana tumekuwa washirika wa Kristo, kama tukishikamana na mwanzo wa uthabiti wetu kwa nguvu mpaka mwisho;

Waebrania 3:15

hapo inenwapo, Leo, kama mtaisikia sauti yake, Msifanye migumu mioyo yenu, Kama wakati wa kukasirisha.

Waebrania 3:16

Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

Waebrania 3:17

Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

Waebrania 3:18

Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?

Waebrania 3:19

Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.