Waebrania Mlango 13 Hebrews

Waebrania 13:1

Upendano wa ndugu na udumu.

Waebrania 13:2

Msisahau kuwafadhili wageni; maana kwa njia hii wengine wamewakaribisha malaika pasipo kujua.

Waebrania 13:3

Wakumbukeni hao waliofungwa kana kwamba mmefungwa pamoja nao; na hao wanaodhulumiwa, kwa vile ninyi nanyi mlivyo katika mwili.

Waebrania 13:4

Ndoa na iheshimiwe na watu wote, na malazi yawe safi; kwa maana waasherati na wazinzi Mungu atawahukumia adhabu.

Waebrania 13:5

Msiwe na tabia ya kupenda fedha; mwe radhi na vitu mlivyo navyo; kwa kuwa yeye mwenyewe amesema, Sitakupungukia kabisa, wala sitakuacha kabisa.

Waebrania 13:6

Hata twathubutu kusema, Bwana ndiye anisaidiaye, sitaogopa; Mwanadamu atanitenda nini?

Waebrania 13:7

Wakumbukeni wale waliokuwa wakiwaongoza, waliowaambia neno la Mungu; tena, kwa kuuchunguza sana mwisho wa mwenendo wao, iigeni imani yao.

Waebrania 13:8

Yesu Kristo ni yeye yule, jana na leo na hata milele.

Waebrania 13:9

Msichukuliwe na mafundisho ya namna nyingine nyingine, na ya kigeni; maana ni vizuri moyo ufanywe imara kwa neema, wala si kwa vyakula, ambavyo wao waliokwenda navyo hawakupata faida.

Waebrania 13:10

Tuna madhabahu ambayo wale waihudumiao ile hema hawana ruhusa kula vitu vyake.

Waebrania 13:11

Maana wanyama wale ambao damu yao huletwa ndani ya patakatifu na kuhani mkuu kwa ajili ya dhambi, viwiliwili vyao huteketezwa nje ya kambi.

Waebrania 13:12

Kwa ajili hii Yesu naye, ili awatakase watu kwa damu yake mwenyewe, aliteswa nje ya lango.

Waebrania 13:13

Basi na tutoke tumwendee nje ya kambi, tukichukua shutumu lake.

Waebrania 13:14

Maana hapa hatuna mji udumuo, bali twautafuta ule ujao.

Waebrania 13:15

Basi, kwa njia yake yeye, na tumpe Mungu dhabihu ya sifa daima, yaani, tunda la midomo iliungamayo jina lake.

Waebrania 13:16

Lakini msisahau kutenda mema na kushirikiana; maana sadaka kama hizi ndizo zimpendezazo Mungu.

Waebrania 13:17

Watiini wenye kuwaongoza, na kuwanyenyekea; maana wao wanakesha kwa ajili ya roho zenu, kama watu watakaotoa hesabu, ili kwamba wafanye hivyo kwa furaha wala si kwa kuugua; maana isingewafaa ninyi.

Waebrania 13:18

Tuombeeni; maana tunaamini kwamba tuna dhamiri njema, tukitaka kuwa na mwenendo mwema katika mambo yote.

Waebrania 13:19

Nami nawasihi zaidi sana kufanya hayo ili nirudishwe kwenu upesi.

Waebrania 13:20

Basi, Mungu wa amani aliyemleta tena kutoka kwa wafu Mchungaji Mkuu wa kondoo, kwa damu ya agano la milele, yeye Bwana wetu Yesu,

Waebrania 13:21

awafanye ninyi kuwa wakamilifu katika kila tendo jema, mpate kuyafanya mapenzi yake, naye akifanya ndani yetu lipendezalo mbele zake, kwa Yesu Kristo; utukufu una yeye milele na milele. Amina.

Waebrania 13:22

Lakini nawasihi, ndugu, mchukuliane na neno hili lenye maonyo maana nimewaandikia kwa maneno machache.

Waebrania 13:23

Jueni ya kuwa ndugu yetu Timotheo amekwisha kufunguliwa; ambaye, akija upesi, nitaonana nanyi pamoja naye.

Waebrania 13:24

Wasalimuni wote wenye kuwaongoza, na watakatifu wote; hao walio wa Italia wanawasalimu.

Waebrania 13:25

Neema na iwe nanyi nyote.