Waebrania Mlango 10 Hebrews

Waebrania 10:1

Basi torati, kwa kuwa ni kivuli cha mema yatakayokuwa, wala si sura yenyewe ya mambo hayo, kwa dhabihu zile zile wanazozitoa kila mwaka daima, haiwezi wakati wo wote kuwakamilisha wakaribiao.

Waebrania 10:2

Kama ndivyo, je! Dhabihu hazingekoma kutolewa; kwa maana waabuduo, wakiisha kusafishwa mara moja, wasingejiona tena kuwa na dhambi?

Waebrania 10:3

Lakini katika dhabihu hizo liko kumbukumbu la dhambi kila mwaka.

Waebrania 10:4

Maana haiwezekani damu ya mafahali na mbuzi kuondoa dhambi.

Waebrania 10:5

Kwa hiyo ajapo ulimwenguni, asema, Dhabihu na toleo hukutaka, Lakini mwili uliniwekea tayari;

Waebrania 10:6

Sadaka za kuteketezwa na sadaka za dhambi hukupendezwa nazo;

Waebrania 10:7

Ndipo niliposema, Tazama, nimekuja (katika gombo la chuo nimeandikiwa) Niyafanye mapenzi yako, Mungu.

Waebrania 10:8

Hapo juu asemapo, Dhabihu na matoleo na sadaka za kuteketezwa na hizo za dhambi hukuzitaka, wala hukupendezwa nazo (zitolewazo kama ilivyoamuru torati),

Waebrania 10:9

ndipo aliposema, Tazama, nimekuja niyafanye mapenzi yako. Aondoa la kwanza, ili kusudi alisimamishe la pili.

Waebrania 10:10

Katika mapenzi hayo mmepata utakaso, kwa kutolewa mwili wa Yesu Kristo mara moja tu.

Waebrania 10:11

Na kila kuhani husimama kila siku akifanya ibada, na kutoa dhabihu zile zile mara nyingi; ambazo haziwezi kabisa kuondoa dhambi.

Waebrania 10:12

Lakini huyu, alipokwisha kutoa kwa ajili ya dhambi dhabihu moja idumuyo hata milele, aliketi mkono wa kuume wa Mungu;

Waebrania 10:13

tangu hapo akingojea hata adui zake wawekwe kuwa chini ya miguu yake.

Waebrania 10:14

Maana kwa toleo moja amewakamilisha hata milele hao wanaotakaswa.

Waebrania 10:15

Na Roho Mtakatifu naye amshuhudia; kwa maana, baada ya kusema,

Waebrania 10:16

Hili ni agano nitakaloagana nao baada ya siku zile, anena Bwana, Nitatia sheria zangu mioyoni mwao, Na katika nia zao nitaziandika; ndipo anenapo,

Waebrania 10:17

Dhambi zao na uasi wao sitaukumbuka tena kabisa.

Waebrania 10:18

Basi, ondoleo la hayo likiwapo, hapana toleo tena kwa ajili ya dhambi.

Waebrania 10:19

Basi, ndugu, kwa kuwa tuna ujasiri wa kupaingia patakatifu kwa damu ya Yesu,

Waebrania 10:20

njia ile aliyotuanzia iliyo mpya, iliyo hai, ipitayo katika pazia, yaani, mwili wake;

Waebrania 10:21

na kuwa na kuhani mkuu juu ya nyumba ya Mungu;

Waebrania 10:22

na tukaribie wenye moyo wa kweli, kwa utimilifu wa imani, hali tumenyunyiziwa mioyo tuache dhamiri mbaya, tumeoshwa miili kwa maji safi.

Waebrania 10:23

Na mlishike sana ungamo la tumaini letu, lisigeuke; maana yeye aliyeahidi ni mwaminifu;

Waebrania 10:24

tukaangaliane sisi kwa sisi na kuhimizana katika upendo na kazi nzuri;

Waebrania 10:25

wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia.

Waebrania 10:26

Maana, kama tukifanya dhambi kusudi baada ya kuupokea ujuzi wa ile kweli, haibaki tena dhabihu kwa ajili ya dhambi;

Waebrania 10:27

bali kuna kuitazamia hukumu yenye kutisha, na ukali wa moto ulio tayari kuwala wao wapingao.

Waebrania 10:28

Mtu aliyeidharau sheria ya Musa hufa pasipo huruma, kwa neno la mashahidi wawili au watatu.

Waebrania 10:29

Mwaonaje? Haikumpasa adhabu iliyo kubwa zaidi mtu yule aliyemkanyaga Mwana wa Mungu, na kuihesabu damu ya agano aliyotakaswa kwayo kuwa ni kitu ovyo, na kumfanyia jeuri Roho wa neema?

Waebrania 10:30

Maana twamjua yeye aliyesema, Kupatiliza kisasi ni juu yangu, mimi nitalipa. Na tena, Bwana atawahukumu watu wake.

Waebrania 10:31

Ni jambo la kutisha kuanguka katika mikono ya Mungu aliye hai.

Waebrania 10:32

Lakini zikumbukeni siku za kwanza, ambazo, mlipokwisha kutiwa nuru, mlistahimili mashindano makubwa ya maumivu;

Waebrania 10:33

pindi mlipotwezwa kwa mashutumu na dhiki, na pindi mliposhirikiana na wale waliotendewa hayo.

Waebrania 10:34

Maana mliwaonea huruma wale waliokuwa katika vifungo, tena mkakubali kwa furaha kunyang'anywa mali zenu, mkijua kwamba nafsini mwenu mna mali iliyo njema zaidi, idumuyo.

Waebrania 10:35

Basi msiutupe ujasiri wenu, kwa maana una thawabu kuu.

Waebrania 10:36

Maana mnahitaji saburi, ili kwamba mkiisha kuyafanya mapenzi ya Mungu mpate ile ahadi.

Waebrania 10:37

Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia.

Waebrania 10:38

Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye.

Waebrania 10:39

Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.