Wagalatia Mlango 3 Galatians

Wagalatia 3:1

Enyi Wagalatia msio na akili, ni nani aliyewaloga, ninyi ambao Yesu Kristo aliwekwa wazi mbele ya macho yenu ya kuwa amesulibiwa?

Wagalatia 3:2

Nataka kujifunza neno hili moja kwenu. Je! Mlipokea Roho kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

Wagalatia 3:3

Je! Mmekuwa wajinga namna hii? Baada ya kuanza katika Roho, mnataka kukamilishwa sasa katika mwili?

Wagalatia 3:4

Mmepatikana na mateso makubwa namna hii bure? Ikiwa ni bure kweli.

Wagalatia 3:5

Basi, yeye awapaye Roho na kufanya miujiza kati yenu, je! Afanya hayo kwa matendo ya sheria, au kwa kusikia kunakotokana na imani?

Wagalatia 3:6

Kama vile Ibrahimu alivyomwamini Mungu akahesabiwa haki.

Wagalatia 3:7

Fahamuni basi, ya kuwa wale walio wa imani, hao ndio wana wa Ibrahimu.

Wagalatia 3:8

Na andiko, kwa vile lilivyoona tangu zamani kwamba Mungu atawahesabia haki Mataifa kwa imani, lilimhubiri Ibrahimu habari njema zamani, kusema, Katika wewe Mataifa yote watabarikiwa.

Wagalatia 3:9

Basi hao walio wa imani hubarikiwa pamoja na Ibrahimu aliyekuwa mwenye imani.

Wagalatia 3:10

Kwa maana wale wote walio wa matendo ya sheria, wako chini ya laana; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu asiyedumu katika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati, ayafanye.

Wagalatia 3:11

Ni dhahiri ya kwamba hakuna mtu ahesabiwaye haki mbele za Mungu katika sheria; kwa sababu Mwenye haki ataishi kwa imani.

Wagalatia 3:12

Na torati haikuja kwa imani, bali, Ayatendaye hayo ataishi katika hayo.

Wagalatia 3:13

Kristo alitukomboa katika laana ya torati, kwa kuwa alifanywa laana kwa ajili yetu; maana imeandikwa, Amelaaniwa kila mtu aangikwaye juu ya mti;

Wagalatia 3:14

ili kwamba baraka ya Ibrahimu iwafikilie Mataifa katika Yesu Kristo, tupate kupokea ahadi ya Roho kwa njia ya imani.

Wagalatia 3:15

Ndugu zangu, nanena kwa jinsi ya kibinadamu. Lijapokuwa ni agano la mwanadamu, hata hivyo likiisha kuthibitika, hakuna mtu alibatilishaye, wala kuliongeza neno.

Wagalatia 3:16

Basi ahadi zilinenwa kwa Ibrahimu na kwa mzao wake. Hasemi, Kwa wazao, kana kwamba ni wengi, bali kana kwamba ni mmoja, Kwa mzao wako, yaani, Kristo.

Wagalatia 3:17

Nisemalo ni hili; agano lililothibitishwa kwanza na Mungu, torati iliyotokea miaka mia nne na thelathini baadaye hailitangui, hata kuibatilisha ile ahadi.

Wagalatia 3:18

Kwa maana urithi ukiwa kwa sheria, hauwi tena kwa ahadi; lakini Mungu alimkirimia Ibrahimu kwa njia ya ahadi.

Wagalatia 3:19

Torati ni nini basi? Iliingizwa kwa sababu ya makosa, hata aje huyo mzao aliyepewa ile ahadi; iliamriwa kwa utumishi wa malaika kwa mkono wa mjumbe.

Wagalatia 3:20

Basi aliye mjumbe si mjumbe wa mmoja; bali Mungu ni mmoja.

Wagalatia 3:21

Basi je! Torati haipatani na ahadi za Mungu? Hasha! Kwa kuwa, kama ingalitolewa sheria iwezayo kuhuisha, yakini haki ingalipatikana kwa sheria.

Wagalatia 3:22

Lakini andiko limeyafunga yote chini ya nguvu ya dhambi, makusudi hao waaminio wapewe ile ahadi kwa imani ya Yesu Kristo.

Wagalatia 3:23

Lakini kabla ya kuja ile imani tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa.

Wagalatia 3:24

Hivyo torati imekuwa kiongozi kutuleta kwa Kristo, ili tuhesabiwe haki kwa imani.

Wagalatia 3:25

Lakini, iwapo imani imekuja, hatupo tena chini ya kiongozi.

Wagalatia 3:26

Kwa kuwa ninyi nyote mmekuwa wana wa Mungu kwa njia ya imani katika Kristo Yesu.

Wagalatia 3:27

Maana ninyi nyote mliobatizwa katika Kristo mmemvaa Kristo.

Wagalatia 3:28

Hapana Myahudi wala Myunani. Hapana mtumwa wala huru. Hapana mtu mume wala mtu mke. Maana ninyi nyote mmekuwa mmoja katika Kristo Yesu.

Wagalatia 3:29

Na kama ninyi ni wa Kristo, basi, mmekuwa uzao wa Ibrahimu, na warithi sawasawa na ahadi.