Wagalatia Mlango 4 Galatians

Wagalatia 4:1

Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote;

Wagalatia 4:2

bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba.

Wagalatia 4:3

Kadhalika na sisi, tulipokuwa watoto, tulikuwa tukitumikishwa na kawaida za kwanza za dunia.

Wagalatia 4:4

Hata ulipowadia utimilifu wa wakati, Mungu alimtuma Mwanawe ambaye amezaliwa na mwanamke, amezaliwa chini ya sheria,

Wagalatia 4:5

kusudi awakomboe hao waliokuwa chini ya sheria, ili sisi tupate kupokea hali ya kuwa wana.

Wagalatia 4:6

Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanawe mioyoni mwetu, aliaye, Aba, yaani, Baba.

Wagalatia 4:7

Kama ni hivyo, wewe si mtumwa tena bali u mwana; na kama u mwana, basi, u mrithi kwa Mungu.

Wagalatia 4:8

Lakini wakati ule, kwa kuwa hamkumjua Mungu, mliwatumikia wao ambao kwa asili si miungu.

Wagalatia 4:9

Bali sasa mkiisha kumjua Mungu, au zaidi kujulikana na Mungu, kwa nini kuyarejea tena mafundisho ya kwanza yaliyo manyonge, yenye upungufu, ambayo mnataka kuyatumikia tena?

Wagalatia 4:10

Mnashika siku, na miezi, na nyakati, na miaka.

Wagalatia 4:11

Nawachelea, isiwe labda nimejitaabisha bure kwa ajili yenu.

Wagalatia 4:12

Ndugu zangu, nawasihi, iweni kama mimi, maana mimi ni kama ninyi. Hamkunidhulumu kwa lo lote.

Wagalatia 4:13

Lakini mwajua ya kuwa naliwahubiri Injili mara ya kwanza kwa sababu ya udhaifu wa mwili;

Wagalatia 4:14

na jaribu lililowapata katika mwili wangu hamkulidharau wala kulikataa, bali mlinipokea kama malaika wa Mungu, kama Kristo Yesu.

Wagalatia 4:15

Ku wapi, basi, kule kujiita heri? Maana nawashuhudu kwamba, kama ingaliwezekana, mngaling'oa macho yenu, mkanipa mimi.

Wagalatia 4:16

Je! Nimekuwa adui wenu kwa sababu nawaambia yaliyo kweli?

Wagalatia 4:17

Hao wana shauku nanyi, lakini si kwa njia nzuri, bali wanataka kuwafungia nje, ili kwamba ninyi mwaonee wao shauku.

Wagalatia 4:18

Navyo ni vizuri kuonewa shauku katika neno jema sikuzote, wala si wakati nikiwapo mimi pamoja nanyi tu.

Wagalatia 4:19

Vitoto vyangu, ambao kwamba nawaonea utungu tena mpaka Kristo aumbike ndani yenu;

Wagalatia 4:20

laiti ningekuwapo pamoja nanyi sasa, na kuigeuza sauti yangu! Maana naona shaka kwa ajili yenu.

Wagalatia 4:21

Niambieni, ninyi mnaotaka kuwa chini ya sheria, je! Hamwisikii sheria?

Wagalatia 4:22

Kwa maana imeandikwa ya kuwa, Ibrahimu alikuwa na wana wawili mmoja kwa mjakazi, na mmoja kwa mwungwana.

Wagalatia 4:23

Lakini yule wa mjakazi alizaliwa kwa mwili, yule wa mwungwana kwa ahadi.

Wagalatia 4:24

Mambo haya husemwa kwa mfano; kwa maana hawa ndio kama maagano mawili, moja kutoka mlima Sinai, lizaalo kwa utumwa, ambalo ni Hajiri.

Wagalatia 4:25

Maana Hajiri ni kama mlima Sinai ulioko Arabuni, umelingana na Yerusalemu wa sasa; kwa kuwa anatumika pamoja na watoto.

Wagalatia 4:26

Bali Yerusalemu wa juu ni mwungwana, naye ndiye mama yetu sisi.

Wagalatia 4:27

Kwa maana imeandikwa, Furahi, wewe uliye tasa, usiyezaa; Paza sauti, ulie, wewe usiye na utungu; Maana watoto wake aliyeachwa pekee ni wengi Kuliko wa huyo aliye na mume.

Wagalatia 4:28

Basi, ndugu zangu, kama Isaka sisi tu watoto wa ahadi.

Wagalatia 4:29

Lakini kama vile siku zile yule aliyezaliwa kwa mwili alivyomwudhi yule aliyezaliwa kwa Roho, ndivyo ilivyo na sasa.

Wagalatia 4:30

Lakini lasemaje andiko? Mfukuze mjakazi na mwanawe, kwa maana mwana wa mjakazi hatarithi kabisa pamoja na mwana wa mwungwana.

Wagalatia 4:31

Ndiposa, ndugu zangu, sisi si watoto wa mjakazi, bali tu watoto wa huyo aliye mwungwana.