Wagalatia Mlango 1 Galatians

Wagalatia 1:1

Paulo, mtume, (si mtume wa wanadamu, wala kutumwa na mwanadamu, bali na Yesu Kristo, na Mungu Baba aliyemfufua kutoka kwa wafu),

Wagalatia 1:2

na ndugu wote walio pamoja nami, kwa makanisa ya Galatia;

Wagalatia 1:3

Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana wetu Yesu Kristo;

Wagalatia 1:4

ambaye alijitoa nafsi yake kwa ajili ya dhambi zetu, ili atuokoe na dunia hii mbovu iliyopo sasa, kama alivyopenda Mungu, Baba yetu.

Wagalatia 1:5

Utukufu una yeye milele na milele, Amina.

Wagalatia 1:6

Nastaajabu kwa kuwa mnamwacha upesi hivi yeye aliyewaita katika neema ya Kristo, na kugeukia injili ya namna nyingine.

Wagalatia 1:7

Wala si nyingine; lakini wapo watu wawataabishao na kutaka kuigeuza injili ya Kristo.

Wagalatia 1:8

Lakini ijapokuwa sisi au malaika wa mbinguni atawahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo tuliyowahubiri, na alaaniwe.

Wagalatia 1:9

Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.

Wagalatia 1:10

Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.

Wagalatia 1:11

Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu.

Wagalatia 1:12

Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.

Wagalatia 1:13

Maana mmesikia habari za mwenendo wangu zamani katika dini ya Kiyahudi, kwamba naliliudhi kanisa la Mungu kupita kiasi, nikaliharibu.

Wagalatia 1:14

Nami naliendelea katika dini ya Kiyahudi kuliko wengi walio hirimu zangu katika kabila yangu, nikajitahidi sana katika kuyashika mapokeo ya baba zangu.

Wagalatia 1:15

Lakini Mungu, aliyenitenga tangu tumboni mwa mama yangu, akaniita kwa neema yake,

Wagalatia 1:16

alipoona vema kumdhihirisha Mwanawe ndani yangu, ili niwahubiri Mataifa habari zake; mara sikufanya shauri na watu wenye mwili na damu;

Wagalatia 1:17

wala sikupanda kwenda Yerusalemu kwa hao waliokuwa mitume kabla yangu; bali nalikwenda zangu Arabuni, kisha nikarudi tena Dameski.

Wagalatia 1:18

Kisha, baada ya miaka mitatu, nalipanda kwenda Yerusalemu ili nionane na Kefa, nikakaa kwake siku kumi na tano.

Wagalatia 1:19

Lakini sikumwona mtume mwingine, ila Yakobo, ndugu yake Bwana.

Wagalatia 1:20

Na hayo ninayowaandikia, angalieni, mbele za Mungu, sisemi uongo.

Wagalatia 1:21

Baadaye nalikwenda pande za Shamu na Kilikia.

Wagalatia 1:22

Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo;

Wagalatia 1:23

ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani.

Wagalatia 1:24

Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.