Wagalatia Mlango 6 Galatians

Wagalatia 6:1

Ndugu zangu, mtu akighafilika katika kosa lo lote, ninyi mlio wa Roho mrejezeni upya mtu kama huyo kwa roho ya upole, ukijiangalia nafsi yako usije ukajaribiwa wewe mwenyewe.

Wagalatia 6:2

Mchukuliane mizigo na kuitimiza hivyo sheria ya Kristo.

Wagalatia 6:3

Maana mtu akijiona kuwa ni kitu, naye si kitu, ajidanganya nafsi yake.

Wagalatia 6:4

Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo atakapokuwa na sababu ya kujisifu ndani ya nafsi yake tu, wala si kwa mwenzake.

Wagalatia 6:5

Maana kila mtu atalichukua furushi lake mwenyewe.

Wagalatia 6:6

Mwanafunzi na amshirikishe mkufunzi wake katika mema yote.

Wagalatia 6:7

Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi; kwa kuwa cho chote apandacho mtu, ndicho atakachovuna.

Wagalatia 6:8

Maana yeye apandaye kwa mwili wake, katika mwili wake atavuna uharibifu; bali yeye apandaye kwa Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele.

Wagalatia 6:9

Tena tusichoke katika kutenda mema; maana tutavuna kwa wakati wake, tusipozimia roho.

Wagalatia 6:10

Kwa hiyo kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema; na hasa jamaa ya waaminio.

Wagalatia 6:11

Tazameni ni kwa herufi gani kubwa nimewaandikia kwa mkono wangu mimi mwenyewe!

Wagalatia 6:12

Wote watakao kuonekana ni wazuri kwa mambo ya mwili, ndio wanaowashurutisha kutahiriwa; makusudi wasiudhiwe kwa ajili ya msalaba wa Kristo, hilo tu.

Wagalatia 6:13

Kwa maana hata wao wenyewe waliotahiriwa hawaishiki sheria; bali wanataka ninyi mtahiriwe, wapate kuona fahari katika miili yenu.

Wagalatia 6:14

Lakini mimi, hasha, nisione fahari juu ya kitu cho chote ila msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambao kwa huo ulimwengu umesulibishwa kwangu, na mimi kwa ulimwengu.

Wagalatia 6:15

Kwa sababu kutahiriwa si kitu, wala kutokutahiriwa, bali kiumbe kipya.

Wagalatia 6:16

Na wote watakaoenenda kwa kanuni hiyo, amani na iwe kwao na rehema, naam, kwa Israeli wa Mungu.

Wagalatia 6:17

Tangu sasa mtu asinitaabishe; kwa maana ninachukua mwilini mwangu chapa zake Yesu.

Wagalatia 6:18

Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu. Amina.