Nahumu Mlango 1 Nahum

Nahumu 1:1

Ufunuo juu ya Ninawi. Kitabu cha maono aliyoyaona Nahumuu, Mwelkoshi.

Nahumu 1:2

Bwana ni Mungu mwenye wivu, naye hujilipiza kisasi; Bwana hujilipiza kisasi, naye ni mwingi wa hasira; Bwana hujilipiza kisasi juu ya adui zake, huwawekea adui zake akiba ya hasira.

Nahumu 1:3

Bwana si mwepesi wa hasira, ana uweza mwingi, wala hatamhesabia mtu mwovu kuwa hana hatia kamwe; Bwana ana njia yake katika kisulisuli na tufani, na mawingu ni mavumbi ya miguu yake.

Nahumu 1:4

Yeye huikemea bahari na kuikausha, pia huikausha mito yote; Bashani hulegea, na Karmeli; hulegea nalo ua la Lebanoni.

Nahumu 1:5

Milima hutetema mbele zake, navyo vilima huyeyuka; nayo dunia huinuliwa mbele za uso wake, naam, dunia na wote wakaao ndani yake.

Nahumu 1:6

Ni nani awezaye kusimama mbele za ghadhabu yake, naye ni nani awezaye kukaa katika ukali wa hasira yake? Hasira yake kali humwagwa kama moto, nayo majabali yapasuliwa na yeye.

Nahumu 1:7

Bwana ni mwema, ni ngome siku ya taabu; naye huwajua hao wamkimbiliao.

Nahumu 1:8

Lakini kwa gharika ifurikayo atapakomesha kabisa mahali pake, na kuwafuatia adui zake hata gizani.

Nahumu 1:9

Mnawaza nini juu ya Bwana? Yeye atakomesha kabisa; mateso hayatainuka mara ya pili.

Nahumu 1:10

Kwa maana wangawa kama miiba iliyotatana, na kunyweshwa kana kwamba ni katika kunywa kwao, wataliwa kabisa kama mabua makavu.

Nahumu 1:11

Ametoka mmoja kwako, aniaye mabaya juu ya Bwana, atoaye mashauri yasiyofaa kitu.

Nahumu 1:12

Bwana asema hivi, Ijapokuwa wana nguvu zilizo timilifu, ijapokuwa ni wengi, hata hivyo watakatwa, naye atapita na kwenda zake. Ingawa nimekutesa, sitakutesa tena.

Nahumu 1:13

Na sasa nitakuvunjia nira yake, nami nitakupasulia mafungo yako.

Nahumu 1:14

Tena Bwana ametoa amri katika habari zako, ya kwamba asipandwe tena mtu awaye yote mwenye jina lako; toka nyumba ya miungu yako nitakatilia mbali sanamu ya kuchora, na sanamu ya kuyeyusha; nitakufanyia kaburi lako; kwa maana u mbovu.

Nahumu 1:15

Tazama, juu ya milima iko miguu yake aletaye habari njema, atangazaye amani. Zishike sikukuu zako, Ee Yuda, uziondoe nadhiri zako; kwa maana yule asiyefaa kitu hatapita kati yako tena kamwe; amekwisha kukatiliwa mbali.