Maombolezo Mlango 1 Lamentations

Maombolezo 1:1

Jinsi mji huu ukaavyo ukiwa, Huo uliokuwa umejaa watu! Jinsi alivyokuwa kama mjane, Yeye aliyekuwa mkuu kati ya mataifa! Binti mfalme kati ya majimbo, Jinsi alivyoshikwa shokoa!

Maombolezo 1:2

Hulia sana wakati wa usiku, Na machozi yake yapo mashavuni; Miongoni mwa wote waliompenda Hakuna hata mmoja amfarijiye; Rafiki zake wote wamemtenda hila, Wamekuwa adui zake.

Maombolezo 1:3

Yuda amehamishwa kwa sababu ya kuonewa, Na kwa sababu ya utumwa mkuu; Anakaa kati ya makafiri, Haoni raha iwayo yote; Wote waliomfuata wamempata Katika dhiki yake.

Maombolezo 1:4

Njia za Sayuni zaomboleza, Kwa kuwa hakuna ajaye kwa sikukuu; Malango yake yote yamekuwa ukiwa, Makuhani wake hupiga kite; Wanawali wake wanahuzunika; Na yeye mwenyewe huona uchungu.

Maombolezo 1:5

Watesi wake wamekuwa kichwa, Adui zake hufanikiwa; Kwa kuwa Bwana amemtesa Kwa sababu ya wingi wa makosa yake; Watoto wake wadogo wamechukuliwa mateka Mbele yake huyo mtesi.

Maombolezo 1:6

Naye huyo binti Sayuni Enzi yake yote imemwacha; Wakuu wake wamekuwa kama ayala Wasioona malisho; Nao wamekwenda zao hawana nguvu Mbele yake anayewafuatia.

Maombolezo 1:7

Siku za mateso na misiba yake, Yerusalemu huyakumbuka matamaniko yake yote Yaliyokuwa tangu siku za kale; Hapo watu wake walipoanguka mikononi mwa mtesi, Wala hakuna hata mmoja wa kumsaidia; Hao watesi wake walimwona, Wakafanya sabato zake kuwa mzaha.

Maombolezo 1:8

Yerusalemu amefanya dhambi sana; Kwa hiyo amekuwa kama kitu kichafu; Wote waliomheshimu wanamdharau, Kwa sababu wameuona uchi wake; Naam, yeye anaugua, Na kujigeuza aende nyuma.

Maombolezo 1:9

Uchafu wake ulikuwa katika marinda yake; Hakukumbuka mwisho wake; Kwa hiyo ameshuka kwa ajabu; Yeye hana mtu wa kumfariji; Tazama, Bwana, teso langu; Maana huyo adui amejitukuza.

Maombolezo 1:10

Huyo mtesi amenyosha mkono wake Juu ya matamaniko yake yote; Maana ameona ya kuwa makafiri wameingia Ndani ya patakatifu pake; Ambao kwa habari zao wewe uliamuru Wasiingie katika kusanyiko lako.

Maombolezo 1:11

Watu wake wote hupiga kite, Wanatafuta chakula; Wameyatoa matamaniko yao wapate chakula Cha kuihuisha nafsi; Ee Bwana, tazama, uangalie; Kwa maana mimi nimekuwa mnyonge.

Maombolezo 1:12

Je! Si kitu kwenu, enyi nyote mpitao njia, Angalieni, mtazame Kama kuna majonzi yo yote mfano wa majonzi yangu, Niliyotendwa mimi, Ambayo Bwana amenihuzunisha kwa hayo Siku ya hasira yake iwakayo.

Maombolezo 1:13

Toka juu amepeleka moto mifupani mwangu, Nao umeishinda; Ametandika wavu aninase miguu, Amenirudisha nyuma; Amenifanya kuwa mtu wa pekee, Na mgonjwa mchana kutwa.

Maombolezo 1:14

Kongwa la makosa yangu limefungwa na mkono wake; Hayo yameshikamana; Yamepanda juu shingoni mwangu; Amezikomesha nguvu zangu;

Maombolezo 1:15

Bwana amenitia mikononi mwao, Ambao siwezi kupingamana nao. Bwana amewafanya mashujaa wangu wote Kuwa si kitu kati yangu; Ameita mkutano mkuu kinyume changu Ili kuwaponda vijana wangu; Bwana amemkanyaga kama shinikizoni Huyo bikira binti Yuda.

Maombolezo 1:16

Mimi ninayalilia mambo hayo; Jicho langu, jicho langu linachuruzika maji; Kwa kuwa mfariji yu mbali nami, Ambaye ilimpasa kunihuisha nafsi; Watoto wangu wameachwa peke yao, Kwa sababu huyo adui ameshinda.

Maombolezo 1:17

Sayuni huinyosha mikono yake; Hakuna hata mmoja wa kumfariji; Bwana ametoa amri juu ya Yakobo, Kwamba wamzungukao wawe watesi wake; Yerusalemu amekuwa kati yao Kama kitu kichafu.

Maombolezo 1:18

Bwana ndiye mwenye haki; Maana nimeiasi amri yake; Sikieni, nawasihi, enyi watu wote, Mkayatazame majonzi yangu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wamechukuliwa mateka.

Maombolezo 1:19

Naliwaita hao walionipenda Lakini walinidanganya; Makuhani wangu na wazee wangu Walifariki mjini; Hapo walipokuwa wakitafuta chakula ili kuzihuisha nafsi zao.

Maombolezo 1:20

Angalia, Ee Bwana; maana mimi ni katika dhiki; Mtima wangu umetaabika; Moyo wangu umegeuka ndani yangu; Maana nimeasi vibaya sana; Huko nje upanga hufisha watu; Nyumbani mna kama mauti.

Maombolezo 1:21

Wamesikia kwamba napiga kite; Hakuna hata mmoja wa kunifariji; Adui zangu wote wamesikia habari ya mashaka yaliyonipata; Hufurahi kwa kuwa umeyafanya hayo; Utaileta siku ile uliyoitangaza, Nao watakuwa kama mimi.

Maombolezo 1:22

Huo uovu wao wote Na uje mbele zako wewe; Ukawatende wao kama ulivyonitenda mimi Kwa dhambi zangu zote; Kwa maana mauguzi yangu ni mengi sana, Na moyo wangu umezimia.