Maombolezo Mlango 2 Lamentations

Maombolezo 2:1

Jinsi Bwana alivyomfunika binti Sayuni Kwa wingu katika hasira yake! Ameutupa toka mbinguni hata nchi Huo uzuri wa Israeli; Wala hakukikumbuka kiti cha miguu yake Katika siku ya hasira yake.

Maombolezo 2:2

Bwana ameyameza makao yote ya Yakobo, Wala hakuona huruma; Ameziangusha ngome za binti Yuda Katika ghadhabu yake; Amezibomoa hata nchi Ameunajisi ufalme na wakuu wake.

Maombolezo 2:3

Ameikata pembe yote ya Israeli Katika hasira yake kali; Ameurudisha nyuma mkono wake wa kuume Mbele ya hao adui, Naye amemteketeza Yakobo kama moto uwakao, Ulao pande zote.

Maombolezo 2:4

Ameupinda upinde wake kama adui, Amesimama na mkono wake wa kuume kama mtesi; Naye amewaua hao wote Waliopendeza macho; Katika hema ya binti Sayuni Amemimina kani yake kama moto.

Maombolezo 2:5

Bwana amekuwa mfano wa adui, Amemmeza Israeli; Ameyameza majumba yake yote, Ameziharibu ngome zake; Tena amemzidishia binti Yuda Matanga na maombolezo.

Maombolezo 2:6

Naye ameondoa maskani yake kwa nguvu, Kana kwamba ni ya bustani tu; Ameziharibu sikukuu zake; Bwana amezisahauzisha katika Sayuni Sikukuu za makini na sabato; Naye amewadharau mfalme na kuhani Katika uchungu wa hasira yake.

Maombolezo 2:7

Bwana ameitupilia mbali madhabahu yake, Amepachukia patakatifu pake; Amezitia katika mikono ya hao adui Kuta za majumba yake; Wamepiga kelele ndani ya nyumba ya Bwana Kama katika siku ya kusanyiko la makini.

Maombolezo 2:8

Bwana amekusudia kuuharibu Ukuta wa binti Sayuni; Ameinyosha hiyo kamba, Hakuuzuia mkono wake usiangamize; Bali amefanya boma na ukuta kuomboleza; Zote pamoja hudhoofika.

Maombolezo 2:9

Malango yake yamezama katika nchi; Ameyaharibu makomeo yake na kuyavunja; Mfalme wake na wakuu wake wanakaa Kati ya mataifa wasio na sheria; Naam, manabii wake hawapati maono Yatokayo kwa Bwana.

Maombolezo 2:10

Wazee wa binti Sayuni huketi chini, Hunyamaza kimya; Wametupa mavumbi juu ya vichwa vyao, Wamejivika viunoni nguo za magunia; Wanawali wa Yerusalemu huinama vichwa vyao Kuielekea nchi.

Maombolezo 2:11

Macho yangu yamechoka kwa machozi, Mtima wangu umetaabika; Ini langu linamiminwa juu ya nchi Kwa uharibifu wa binti ya watu wangu; Kwa sababu watoto wachanga na wanyonyao, Huzimia katika mitaa ya mji.

Maombolezo 2:12

Wao huwauliza mama zao, Zi wapi nafaka na divai? Hapo wazimiapo kama waliojeruhiwa Katika mitaa ya mji, Hapo walipomiminika nafsi zao Vifuani mwa mama zao.

Maombolezo 2:13

Nikushuhudie nini? Nikufananishe na nini, Ee Binti Yerusalemu? Nikusawazishe na nini, nipate kukufariji, Ee bikira binti Sayuni? Kwa maana uvunjifu wako ni mkuu kama bahari, Ni nani awezaye kukuponya?

Maombolezo 2:14

Manabii wako wameona maono kwa ajili yako Ya ubatili na upumbavu Wala hawakufunua uovu wako, Wapate kurudisha kufungwa kwako; Bali wameona mabashiri ya ubatili kwa ajili yako Na sababu za kuhamishwa.

Maombolezo 2:15

Hao watu wote wapitao Hukupigia makofi; Humzomea binti Yerusalemu, Na kutikisa vichwa vyao; Je! Mji huu ndio ulioitwa, Ukamilifu wa uzuri, Furaha ya dunia yote?

Maombolezo 2:16

Juu yako adui zako wote Wamepanua vinywa vyao; Huzomea, husaga meno yao, Husema, Tumemmeza; Hakika siku hii ndiyo tuliyoitazamia; Tumeipata, tumeiona.

Maombolezo 2:17

Bwana ameyatenda aliyoyakusudia; amelitimiza neno lake, Aliloliamuru siku za kale; Ameangusha hata chini, Wala hakuona huruma; Naye amemfurahisha adui juu yako, Ameitukuza pembe ya watesi wako.

Maombolezo 2:18

Mioyo yao ilimlilia Bwana; Ee ukuta wa binti Sayuni! Machozi na yachuruzike kama mto Mchana na usiku; Usijipatie kupumzika; Mboni ya jicho lako isikome.

Maombolezo 2:19

Inuka, ulalamike usiku, Mwanzo wa makesha yake; Mimina moyo wako kama maji usoni pa Bwana; Umwinulie mikono yako; Kwa uhai wa watoto wako wachanga wazimiao kwa njaa, Mwanzo wa kila njia kuu.

Maombolezo 2:20

Tazama, Bwana, uangalie, Ni nani uliyemtenda hayo! Je! Wanawake wale mazao yao, Watoto waliowabeba? Je! Kuhani na nabii wauawe Katika patakatifu pa Bwana?

Maombolezo 2:21

Kijana na mzee hulala chini Katika njia kuu; Wasichana wangu na wavulana wangu Wameanguka kwa upanga; Umewaua katika siku ya hasira yako; Umeua, wala hukuona huruma.

Maombolezo 2:22

Umeziita kama katika siku ya mkutano wa makini; Hofu zangu zije pande zote; Wala hapana hata mmoja aliyepona wala kusalia Katika siku ya hasira ya Bwana; Hao niliowabeba na kuwalea Huyo adui yangu amewakomesha.