Maombolezo Mlango 3 Lamentations

Maombolezo 3:1

Mimi ni mtu aliyeona mateso Kwa fimbo ya ghadhabu yake.

Maombolezo 3:2

Ameniongoza na kuniendesha katika giza Wala si katika nuru.

Maombolezo 3:3

Hakika juu yangu augeuza mkono wake Mara kwa mara mchana wote.

Maombolezo 3:4

Amechakaza nyama yangu na ngozi yangu; Ameivunja mifupa yangu.

Maombolezo 3:5

Amejenga boma juu yangu, Na kunizungusha uchungu na uchovu.

Maombolezo 3:6

Amenikalisha penye giza, Kama watu waliokufa zamani.

Maombolezo 3:7

Amenizinga pande zote hata siwezi kutoka; Ameufanya mnyororo wangu mzito.

Maombolezo 3:8

Naam, nikilia na kuomba msaada, Huyapinga maombi yangu.

Maombolezo 3:9

Ameziziba njia zangu kwa mawe yaliyochongwa; Ameyapotosha mapito yangu.

Maombolezo 3:10

Alivyo kwangu ni kama dubu aoteaye, Kama simba aliye mafichoni.

Maombolezo 3:11

Amezigeuza njia zangu, na kunirarua-rarua; Amenifanya ukiwa.

Maombolezo 3:12

Ameupinda upinde wake, Na kunifanya niwe shabaha kwa mshale.

Maombolezo 3:13

Amenichoma viuno Kwa mishale ya podo lake.

Maombolezo 3:14

Nimekuwa dhihaka kwa watu wangu wote; Wimbo wao mchana kutwa.

Maombolezo 3:15

Amenijaza uchungu, Amenikinaisha kwa pakanga.

Maombolezo 3:16

Amenivunja meno kwa changarawe; Amenifunika majivu.

Maombolezo 3:17

Umeniweka nafsi yangu mbali na amani; Nikasahau kufanikiwa.

Maombolezo 3:18

Nikasema, Nguvu zangu zimepotea, Na tumaini langu kwa Bwana.

Maombolezo 3:19

Kumbuka mateso yangu, na msiba wangu, Pakanga na nyongo.

Maombolezo 3:20

Nafsi yangu ikali ikiyakumbuka hayo, Nayo imeinama ndani yangu.

Maombolezo 3:21

Najikumbusha neno hili, Kwa hiyo nina matumaini.

Maombolezo 3:22

Ni huruma za Bwana kwamba hatuangamii, Kwa kuwa rehema zake hazikomi.

Maombolezo 3:23

Ni mpya kila siku asubuhi; Uaminifu wako ni mkuu.

Maombolezo 3:24

Bwana ndiye fungu langu, husema nafsi yangu, Kwa hiyo nitamtumaini yeye.

Maombolezo 3:25

Bwana ni mwema kwa hao wamngojeao, Kwa hiyo nafsi imtafutayo.

Maombolezo 3:26

Ni vema mtu autarajie wokovu wa Bwana Na kumngojea kwa utulivu.

Maombolezo 3:27

Ni vema mwanadamu aichukue nira Wakati wa ujana wake.

Maombolezo 3:28

Na akae peke yake na kunyamaza kimya; Kwa sababu Bwana ameweka hayo juu yake.

Maombolezo 3:29

Na atie kinywa chake mavumbini; Ikiwa yamkini liko tumaini.

Maombolezo 3:30

Na amwelekezee yule ampigaye shavu lake; Ashibishwe mashutumu.

Maombolezo 3:31

Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.

Maombolezo 3:32

Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.

Maombolezo 3:33

Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha.

Maombolezo 3:34

Kuwaseta chini kwa miguu Wafungwa wote wa duniani,

Maombolezo 3:35

Kuipotosha hukumu ya mtu Mbele zake Aliye juu,

Maombolezo 3:36

Na kumnyima mtu haki yake, Hayo Bwana hayaridhii kabisa.

Maombolezo 3:37

Ni nani asemaye neno nalo likafanyika, Ikiwa Bwana hakuliagiza?

Maombolezo 3:38

Je! Katika kinywa chake Aliye juu Hayatoki maovu na mema?

Maombolezo 3:39

Mbona anung'unika mwanadamu aliye hai Mtu akiadhibiwa kwa dhambi zake?

Maombolezo 3:40

Na tuchunguze njia zetu na kuzijaribu, Na kumrudia Bwana tena.

Maombolezo 3:41

Na tumwinulie Mungu aliye mbinguni Mioyo yetu na mikono.

Maombolezo 3:42

Sisi tumekosa na kuasi; Wewe hukusamehe.

Maombolezo 3:43

Umetufunika kwa hasira na kutufuatia; Umeua, wala hukuona huruma.

Maombolezo 3:44

Umejifunika nafsi yako kwa wingu, Maombi yetu yasipite.

Maombolezo 3:45

Umetufanya kuwa takataka, na vifusi Katikati ya mataifa.

Maombolezo 3:46

Juu yetu adui zetu wote Wametupanulia vinywa vyao.

Maombolezo 3:47

Hofu imetujilia na shimo, Ukiwa na uharibifu.

Maombolezo 3:48

Jicho langu lachuruzika mito ya maji Kwa ajili ya uvunjifu wa binti ya watu wangu.

Maombolezo 3:49

Jicho langu latoka machozi lisikome, Wala haliachi;

Maombolezo 3:50

Hata Bwana atakapoangalia Na kutazama toka mbinguni.

Maombolezo 3:51

Jicho langu lanitia huzuni nafsini mwangu, Kwa sababu ya binti zote za mji wangu.

Maombolezo 3:52

Walio adui zangu bila sababu Wameniwinda sana kama ndege;

Maombolezo 3:53

Wameukatilia mbali uhai wangu gerezani, Na kutupa jiwe juu yangu.

Maombolezo 3:54

Maji mengi yalipita juu ya kichwa changu, Nikasema, Nimekatiliwa mbali.

Maombolezo 3:55

Naliliitia jina lako, Bwana, kutoka lile shimo Liendalo chini kabisa.

Maombolezo 3:56

Ukaisikia sauti yangu; usifiche sikio lako Ili usisikie pumzi yangu, kwa kilio changu.

Maombolezo 3:57

Ulinikaribia siku ile nilipokulilia; Ukasema, Usiogope.

Maombolezo 3:58

Ee Bwana umenitetea mateto ya nafsi yangu; Umeukomboa uhai wangu.

Maombolezo 3:59

Umekuona kudhulumiwa kwangu, Ee Bwana; Unihukumie neno langu.

Maombolezo 3:60

Umekiona kisasi chao chote, Na mashauri yao yote juu yangu.

Maombolezo 3:61

Ee Bwana, umeyasikia matukano yao, Na mashauri yao yote juu yangu;

Maombolezo 3:62

Midomo yao walioinuka juu yangu Na maazimio yao juu yangu mchana kutwa.

Maombolezo 3:63

Uangalie kuketi kwao, na kuinuka kwao; Wimbo wao ndio mimi.

Maombolezo 3:64

Utawalipa malipo, Ee Bwana, Sawasawa na kazi ya mikono yao.

Maombolezo 3:65

Utawapa ushupavu wa moyo; Laana yako juu yao.

Maombolezo 3:66

Utawafuatia kwa hasira, na kuwaangamiza Wasiwe tena chini ya mbingu za Bwana.