Maombolezo Mlango 4 Lamentations

Maombolezo 4:1

Jinsi dhahabu ilivyoacha kung'aa, Na dhahabu iliyo safi ilivyobadilika! Mawe ya patakatifu yametupwa Mwanzo wa kila njia.

Maombolezo 4:2

Wana wa Sayuni wenye thamani, Walinganao na dhahabu safi, Jinsi wanavyodhaniwa kuwa vyombo vya udongo, Kazi ya mikono ya mfinyanzi!

Maombolezo 4:3

Hata mbwa-mwitu hutoa matiti, Huwanyonyesha watoto wao; Binti ya watu wangu amekuwa mkali, Mfano wa mbuni jangwani.

Maombolezo 4:4

Ulimi wa mtoto anyonyaye Wagandamana na kaakaa lake kwa kiu; Watoto wachanga waomba chakula, Wala hakuna hata mmoja awamegeaye.

Maombolezo 4:5

Wale waliokula vitu vya anasa Wameachwa peke yao njiani; Wale waliokuzwa kuvaa nguo nyekundu Wakumbatia jaa.

Maombolezo 4:6

Maana uovu wa binti ya watu wangu ni mkubwa Kuliko dhambi ya Sodoma, Uliopinduliwa kama katika dakika moja, Wala mikono haikuwekwa juu yake.

Maombolezo 4:7

Wakuu wake walikuwa safi kuliko theluji, Walikuwa weupe kuliko maziwa; Miili yao, walikuwa wekundu kuliko marijani, Na umbo lao kama yakuti samawi.

Maombolezo 4:8

Nyuso zao ni nyeusi kuliko makaa; Hawajulikani katika njia kuu; Ngozi yao yagandamana na mifupa yao Imekauka, imekuwa kama mti.

Maombolezo 4:9

Heri wale waliouawa kwa upanga Kuliko wao waliouawa kwa njaa; Maana hao husinyaa, wakichomwa Kwa kukosa matunda ya mashamba.

Maombolezo 4:10

Mikono ya wanawake wenye huruma Imewatokosa watoto wao wenyewe; Walikuwa ndio chakula chao Katika uharibifu wa binti ya watu wangu.

Maombolezo 4:11

Bwana ameitimiza kani yake, Ameimimina hasira yake kali; Naye amewasha moto katika Sayuni Ulioiteketeza misingi yake.

Maombolezo 4:12

Wafalme wa dunia hawakusadiki, Wala wote wakaao duniani, Ya kwamba mtesi na adui wangeingia Katika malango ya Yerusalemu.

Maombolezo 4:13

Ni kwa sababu ya dhambi za manabii wake Na maovu ya makuhani wake, Walioimwaga damu ya wenye haki Katikati yake.

Maombolezo 4:14

Hutanga-tanga njiani kama vipofu, Wametiwa unajisi kwa damu; Hata ikawa watu wasiweze Kuyagusa mavazi yao.

Maombolezo 4:15

Watu waliwapigia kelele, Ondokeni, Uchafu, Ondokeni, ondokeni, msiguse; Walipokimbia na kutanga-tanga, watu walisema kati ya mataifa, Hawatakaa hapa tena.

Maombolezo 4:16

Hasira ya Bwana imewatenga, Yeye hatawaangalia tena; Hawakujali nafsi za wale makuhani, Hawakuwaheshimu wazee wao.

Maombolezo 4:17

Macho yetu yamechoka Kwa kuutazamia bure msaada wetu; Katika kungoja kwetu tumengojea taifa Lisiloweza kutuokoa.

Maombolezo 4:18

Wanatuvizia hatua zetu, Hata hatuwezi kwenda katika njia zetu; Mwisho wetu umekaribia, siku zetu zimetimia; Maana mwisho wetu umefika.

Maombolezo 4:19

Waliotufuatia ni wepesi Kuliko tai za mbinguni; Hao walitufuatia milimani, Nao walituotea jangwani.

Maombolezo 4:20

Pumzi ya mianzi ya pua zetu, masihi wa BWANA, Alikamatwa katika marima yao;Ambaye kwa habari zake tulisema,Chini ya kivuli chake tukakaa kati ya mataifa.

Maombolezo 4:21

Furahi, ushangilie, Ee binti Edomu, Ukaaye katika nchi ya Usi; Hata kwako kikombe kitapita, Utalewa, na kujifanya uchi.

Maombolezo 4:22

Uovu wako umetimia, Ee binti Sayuni; Hatakuhamisha tena; Atapatiliza uovu wako, Ee binti Edomu; Atazivumbua dhambi zako.