Waefeso Mlango 6 Ephesians

Waefeso 6:1

Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, maana hii ndiyo haki.

Waefeso 6:2

Waheshimu baba yako na mama yako; amri hii ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi,

Waefeso 6:3

Upate heri, ukae siku nyingi katika dunia.

Waefeso 6:4

Nanyi, akina baba, msiwachokoze watoto wenu; bali waleeni katika adabu na maonyo ya Bwana.

Waefeso 6:5

Enyi watumwa, watiini wao walio bwana zenu kwa jinsi ya mwili, kwa hofu na kutetemeka, kwa unyofu wa moyo, kana kwamba ni kumtii Kristo;

Waefeso 6:6

wala si kwa utumwa wa macho tu kama wajipendekazao kwa wanadamu bali kama watumwa wa Kristo, mkitenda yampendezayo Mungu kwa moyo;

Waefeso 6:7

kwa nia njema kama kumtumikia Bwana wala si mwanadamu;

Waefeso 6:8

mkijua ya kuwa kila neno jema alitendalo mtu atapewa lilo hilo na Bwana kwamba ni mtumwa au kwamba ni huru.

Waefeso 6:9

Nanyi, akina bwana, watendeeni wao yayo hayo, mkiacha kuwaogofya, huku mkijua ya kuwa yeye aliye Bwana wao na wenu yuko mbinguni, wala kwake hakuna upendeleo.

Waefeso 6:10

Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake.

Waefeso 6:11

Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.

Waefeso 6:12

Kwa maana kushindana kwetu sisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.

Waefeso 6:13

Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.

Waefeso 6:14

Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,

Waefeso 6:15

na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;

Waefeso 6:16

zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu.

Waefeso 6:17

Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;

Waefeso 6:18

kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;

Waefeso 6:19

pia na kwa ajili yangu mimi, nipewe usemi kwa kufumbua kinywa changu, ili niihubiri kwa ujasiri ile siri ya Injili;

Waefeso 6:20

ambayo kwa ajili yake mimi ni mjumbe katika minyororo; hata nipate ujasiri katika huyo kunena jinsi inipasavyo kunena.

Waefeso 6:21

Basi ninyi nanyi mpate kuzijua habari zangu, ni hali gani, Tikiko, ndugu mpendwa, mhudumu mwaminifu katika Bwana, atawajulisheni mambo yote;

Waefeso 6:22

ambaye nampeleka kwenu kwa kusudi lilo hilo mpate kuzijua habari zetu, naye awafariji mioyo yenu.

Waefeso 6:23

Amani na iwe kwa ndugu, na pendo, pamoja na imani, zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Bwana Yesu Kristo.

Waefeso 6:24

Neema na iwe pamoja na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo katika hali ya kutokuharibika.