Waefeso Mlango 3 Ephesians

Waefeso 3:1

Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa;

Waefeso 3:2

ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu;

Waefeso 3:3

ya kwamba kwa kufunuliwa nalijulishwa siri hiyo, kama nilivyotangulia kuandika kwa maneno machache.

Waefeso 3:4

Kwa hayo, myasomapo, mtaweza kuutambua ufahamu wangu katika siri yake Kristo.

Waefeso 3:5

Siri hiyo hawakujulishwa wanadamu katika vizazi vingine; kama walivyofunuliwa mitume wake watakatifu na manabii zamani hizi katika Roho;

Waefeso 3:6

ya kwamba Mataifa ni warithi pamoja nasi wa urithi mmoja, na wa mwili mmoja, na washiriki pamoja nasi wa ahadi yake iliyo katika Kristo Yesu kwa njia ya Injili;

Waefeso 3:7

Injili hiyo ambayo nalifanywa mhudumu wake, kwa kadiri ya kipawa cha neema ya Mungu niliyopewa kwa kadiri ya utendaji wa uweza wake.

Waefeso 3:8

Mimi, niliye mdogo kuliko yeye aliye mdogo wa watakatifu wote, nalipewa neema hii ya kuwahubiri Mataifa utajiri wake Kristo usiopimika;

Waefeso 3:9

na kuwaangaza watu wote wajue habari za madaraka ya siri hiyo, ambayo tangu zamani zote ilisitirika katika Mungu aliyeviumba vitu vyote;

Waefeso 3:10

ili sasa, kwa njia ya kanisa, hekima ya Mungu iliyo ya namna nyingi ijulikane na falme na mamlaka katika ulimwengu wa roho;

Waefeso 3:11

kwa kadiri ya kusudi la milele alilolikusudia katika Kristo Yesu Bwana wetu.

Waefeso 3:12

Katika yeye tunao ujasiri na uwezo wa kukaribia katika tumaini kwa njia ya kumwamini.

Waefeso 3:13

Basi naomba msikate tamaa kwa sababu ya dhiki zangu kwa ajili yenu, zilizo utukufu kwenu.

Waefeso 3:14

Kwa hiyo nampigia Baba magoti,

Waefeso 3:15

ambaye kwa jina lake ubaba wote wa mbinguni na wa duniani unaitwa,

Waefeso 3:16

awajalieni, kwa kadiri ya utajiri wa utukufu wake, kufanywa imara kwa nguvu, kwa kazi ya Roho wake katika utu wa ndani.

Waefeso 3:17

Kristo akae mioyoni mwenu kwa imani mkiwa na shina na msingi katika upendo;

Waefeso 3:18

ili mpate kufahamu pamoja na watakatifu wote jinsi ulivyo upana, na urefu, na kimo, na kina;

Waefeso 3:19

na kuujua upendo wake Kristo, upitao ufahamu kwa jinsi ulivyo mwingi, mpate kutimilika kwa utimilifu wote wa Mungu.

Waefeso 3:20

Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu;

Waefeso 3:21

naam, atukuzwe katika Kanisa na katika Kristo Yesu hata vizazi vyote vya milele na milele. Amina.