Waefeso Mlango 4 Ephesians

Waefeso 4:1

Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa;

Waefeso 4:2

kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo;

Waefeso 4:3

na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa Roho katika kifungo cha amani.

Waefeso 4:4

Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu.

Waefeso 4:5

Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja.

Waefeso 4:6

Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.

Waefeso 4:7

Lakini kila mmoja wetu alipewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa chake Kristo.

Waefeso 4:8

Hivyo husema, Alipopaa juu aliteka mateka, Akawapa wanadamu vipawa.

Waefeso 4:9

Basi neno hilo, Alipaa, maana yake nini kama siyo kusema kwamba yeye naye alishuka mpaka pande zilizo chini za nchi?

Waefeso 4:10

Naye aliyeshuka ndiye yeye aliyepaa juu sana kupita mbingu zote, ili avijaze vitu vyote.

Waefeso 4:11

Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu;

Waefeso 4:12

kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe;

Waefeso 4:13

hata na sisi sote tutakapoufikia umoja wa imani na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo;

Waefeso 4:14

ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu.

Waefeso 4:15

Lakini tuishike kweli katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.

Waefeso 4:16

Katika yeye mwili wote ukiungamanishwa na kushikanishwa kwa msaada wa kila kiungo, kwa kadiri ya utendaji wa kila sehemu moja moja, huukuza mwili upate kujijenga wenyewe katika upendo.

Waefeso 4:17

Basi nasema neno hili, tena nashuhudia katika Bwana, tangu sasa msienende kama Mataifa waenendavyo, katika ubatili wa nia zao;

Waefeso 4:18

ambao; akili zao zimetiwa giza, nao wamefarikishwa na uzima wa Mungu, kwa sababu ya ujinga uliomo ndani yao, kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao;

Waefeso 4:19

ambao wakiisha kufa ganzi wanajitia katika mambo ya ufisadi wapate kufanyiza kila namna ya uchafu kwa kutamani.

Waefeso 4:20

Bali ninyi, sivyo mlivyojifunza Kristo;

Waefeso 4:21

ikiwa mlimsikia mkafundishwa katika yeye, kama kweli ilivyo katika Yesu,

Waefeso 4:22

mvue kwa habari ya mwenendo wa kwanza utu wa zamani, unaoharibika kwa kuzifuata tamaa zenye kudanganya;

Waefeso 4:23

na mfanywe wapya katika roho ya nia zenu;

Waefeso 4:24

mkavae utu mpya, ulioumbwa kwa namna ya Mungu katika haki na utakatifu wa kweli.

Waefeso 4:25

Basi uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake; kwa maana tu viungo, kila mmoja kiungo cha wenzake.

Waefeso 4:26

Mwe na hasira, ila msitende dhambi; jua lisichwe na uchungu wenu bado haujawatoka;

Waefeso 4:27

wala msimpe Ibilisi nafasi.

Waefeso 4:28

Mwibaji asiibe tena; bali afadhali afanye juhudi, akitenda kazi iliyo nzuri kwa mikono yake mwenyewe, apate kuwa na kitu cha kumgawia mhitaji.

Waefeso 4:29

Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia.

Waefeso 4:30

Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.

Waefeso 4:31

Uchungu wote na ghadhabu na hasira na kelele na matukano yaondoke kwenu, pamoja na kila namna ya ubaya;

Waefeso 4:32

tena iweni wafadhili ninyi kwa ninyi, wenye huruma, mkasameheane kama na Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.