Amosi Mlango 8 Amos

Amosi 8:1

Haya ndiyo aliyonionyesha Bwana MUNGU; tazama, kikapu cha matunda ya wakati wa hari.

Amosi 8:2

Akaniambia, Amosii, unaona nini? Nikasema, Naona kikapu cha matunda ya wakati wa hari. Ndipo Bwana akaniambia, Mwisho wao umewajilia watu wangu Israeli; sitawapita tena kamwe.

Amosi 8:3

Tena nyimbo za hekaluni zitakuwa vilio siku ile, asema Bwana MUNGU; mizoga itakuwa mingi; kila mahali wataitupa, wakinyamaza kimya.

Amosi 8:4

Lisikieni hili, ninyi mnaopenda kuwameza wahitaji, na kuwakomesha maskini wa nchi,

Amosi 8:5

mkisema, Mwezi mpya utaondoka lini, tupate kuuza nafaka? Na sabato nayo, tupate kuandika ngano? Mkiipunguza efa na kuiongeza shekeli, mkidanganya watu kwa mizani ya udanganyifu;

Amosi 8:6

tupate kuwanunua maskini kwa fedha, na wahitaji kwa jozi ya viatu; na kuziuza takataka za ngano.

Amosi 8:7

Bwana ameapa kwa fahari ya Yakobo, Hakika sitazisahau kamwe kazi zao hata mojawapo.

Amosi 8:8

Kwa ajili ya hayo, je! Haitatetemeka nchi, na kuomboleza kila mtu akaaye ndani yake? Naam, itainuka yote pia kama huo Mto; nayo itataabika na kupwa tena kama Mto wa Misri.

Amosi 8:9

Tena itakuwa siku hiyo, asema Bwana MUNGU, nitalifanya jua litue wakati wa adhuhuri, nami nitaitia nchi giza wakati wa nuru ya mchana.

Amosi 8:10

Nami nitazigeuza sikukuu zenu kuwa maombolezo, na nyimbo zenu zote kuwa vilio; nami nitatia nguo za magunia katika viuno vyote, na upaa katika kila kichwa; nami nitayafanya haya kuwa kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, na mwisho wake kama siku ya uchungu.

Amosi 8:11

Angalia, siku zinakuja, asema Bwana MUNGU, ambazo nitaleta njaa katika nchi; si njaa ya kukosa chakula, wala kiu ya kukosa maji, bali ya kukosa kuyasikia maneno ya Bwana.

Amosi 8:12

Nao watatanga-tanga toka bahari hata bahari; na toka upande wa kaskazi hata upande wa mashariki; watapiga mbio, wakienda huko na huko, kulitafuta neno la Bwana, wasilione.

Amosi 8:13

Siku hiyo wanawali wazuri na wavulana watazimia kwa kiu.

Amosi 8:14

Na hao waapao kwa dhambi ya Samaria, na kusema, Kama aishivyo Mungu wako, Ee Dani, na, Kama iishivyo njia ya Beer-sheba, hao nao wataanguka, wasiinuke tena.