Amosi Mlango 5 Amos

Amosi 5:1

Lisikieni neno hili nilitamkalo liwe maombolezo juu yenu, enyi nyumba ya Israeli.

Amosi 5:2

Bikira wa Israeli ameanguka; hatainuka tena; Ameangushwa katika nchi yake; hakuna mtu wa kumwinua.

Amosi 5:3

Kwa kuwa Bwana MUNGU asema hivi; Mji uliotoka nje wenye watu elfu, utasaziwa watu mia, na mji uliotoka wenye watu mia, utasaziwa watu kumi, kwa nyumba ya Israeli.

Amosi 5:4

Maana Bwana awaambia hivi nyumba ya Israeli, Nitafuteni mimi, nanyi mtaishi;

Amosi 5:5

bali msitafute Betheli, wala msiingie Gilgali, wala msipite kwenda Beer-sheba; kwani Gilgali hakika yake itakwenda utumwani, na Betheli itakuwa ubatili.

Amosi 5:6

Mtafuteni Bwana, nanyi mtaishi; asije akawaka kama moto katika nyumba ya Yusufu, nao ukateketeza, asiwepo mtu awezaye kuuzima katika Betheli.

Amosi 5:7

Ninyi mnaogeuza hukumu kuwa uchungu, na kuiangusha haki chini,

Amosi 5:8

mtafuteni yeye afanyaye Kilimia na Orioni, na kukigeuza kivuli cha mauti kuwa asubuhi, na kuufanya mchana kuwa giza kwa usiku; yeye ayaitaye maji ya bahari, na kuyamwaga juu ya uso wa nchi; Bwana, ndilo jina lake;

Amosi 5:9

yeye aletaye uharibifu wa ghafula juu yao walio hodari, hata uharibifu uipate ngome.

Amosi 5:10

Wao humchukia yeye akemeaye langoni, nao humzira anenaye maneno ya adili.

Amosi 5:11

Basi, kwa kuwa mnamkanyaga maskini, na kumtoza ngano; ninyi mmejenga nyumba za mawe yaliyochongwa, lakini hamtakaa ndani yake; ninyi mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu, lakini hamtakunywa divai yake.

Amosi 5:12

Maana mimi najua jinsi maasi yenu yalivyo mengi, na jinsi dhambi zenu zilivyo kubwa; ninyi mnaowaonea wenye haki, mnaopokea rushwa, na kuwageuza wahitaji langoni wasipate haki yao.

Amosi 5:13

Kwa ajili ya hayo mwenye busara atanyamaza kimya wakati kama huo; kwa kuwa ni wakati mbaya.

Amosi 5:14

Tafuteni mema, wala si mabaya, mpate kuishi; hivyo Bwana, Mungu wa majeshi, atakuwa pamoja nanyi, kama msemavyo.

Amosi 5:15

Yachukieni mabaya; yapendeni mema; mkaithibitishe haki langoni; yamkini kwamba Bwana, Mungu wa majeshi, atawafanyia fadhili mabaki ya Yusufu.

Amosi 5:16

Kwa ajili ya hayo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, aliye Bwana; Kutakuwako maombolezo katika njia kuu zote; nao watasema katika njia zote, Ole! Ole! Nao watamwita mkulima aje kuombolea, na hao walio hodari wa kulia waje kuomboleza.

Amosi 5:17

Tena katika mashamba yote ya mizabibu kutakuwako kulia; kwa maana mimi nitapita katikati yako, asema Bwana.

Amosi 5:18

Ole wenu! Ninyi mnaoitamani siku ya Bwana; kwani kuitamani siku ya Bwana? Ni giza, wala si nuru.

Amosi 5:19

Ni kama mtu aliyemkimbia simba, akakutana na dubu; au aliingia katika nyumba akauegemeza mkono wake ukutani, nyoka akamwuma.

Amosi 5:20

Je! Siku ya Bwana haitakuwa giza, wala si nuru? Naam, yenye giza sana, wala haina mwanga.

Amosi 5:21

Mimi nazichukia sikukuu zenu, nazidharau, nami sitapendezwa na makutano yenu ya dini.

Amosi 5:22

Naam, ijapokuwa mnanitolea sadaka zenu za kuteketezwa na sadaka zenu za unga, sitazikubali; wala sitaziangalia sadaka zenu za amani, na za wanyama walionona.

Amosi 5:23

Niondoleeni kelele za nyimbo zenu; kwa maana sitaki kuzisikia sauti za vinanda vyenu.

Amosi 5:24

Lakini hukumu na itelemke kama maji, na haki kama maji makuu.

Amosi 5:25

Je! Mliniletea dhabihu na sadaka jangwani muda wa miaka arobaini, enyi nyumba ya Israeli?

Amosi 5:26

Naam, mtamchukua Sikuthi, mfalme wenu, na Kiuni, sanamu zenu, nyota ya mungu wenu, mliojifanyizia wenyewe.

Amosi 5:27

Kwa sababu hiyo nitawahamisha, hali ya kufungwa, mwende mbali kupita Dameski, asema Bwana, ambaye jina lake ni Mungu wa majeshi.